Friday, 26 February 2016

Tagged Under:

Kila la heri Yanga

By: Unknown On: 22:27
  • Share The Gag


  • WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa ngazi ya klabu, timu ya soka ya Yanga leo itashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikipeperusha bendera ya nchi.
    Yanga itakuwa kibaruani kuoneshana umwamba na timu ya Cercle de Joachim ya Mauritius katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika ugenini, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, hivyo leo inahitaji ushindi ama sare tu itakuwa imesonga mbele.
    Watanzania sote tunajua umuhimu wa mchezo huu, tunatambua namna gani nchi yetu itapata sifa kama Yanga itaibuka kidedea. Tunaitakia kila la heri Yanga, huku tukiamini watawapa mashabiki furaha na si karaha kwani ndoto yao ni kufika mafanikio makubwa zaidi.
    Ni vyema mashabiki sote bila kuangalia klabu gani wanayoipenda hapa nchini, tushirikiane kuitakia heri Yanga na kwa wale watakaopata fursa waende wakaishangilie na wengine waiombee dua tunaamini zitafika. Hakuna haja ya kuiona Yanga kama timu ya nchi nyingine, hivyo kuitakia mabaya kwa kisingizio chochote kile.
    Tuna kila sababu ya kuona mchezo wa leo una umuhimu mkubwa kwetu sisi Watanzania hasa kipindi hiki tunachohaha kujaribu kuinua soka letu. Kwa upande wa wachezaji wenyewe nao lazima wahakikishe wanapigana kufa au kupona ili ushindi upatikane.
    Tunaamini wachezaji wa Yanga wamejiandaa vya kutosha, wamepewa kila aina ya hamasa na pia wamelipwa vizuri ili wasiwe na malalamiko badala yake wawe na kazi moja tu ya kuhakikisha wanaleta ushindi.
    Tuweke akilini kuwa kwa vile wenzetu tuliwafunga kwao bao 1-0, hata wao wanaweza pia kutufunga kwetu, hivyo tusibweteke badala yake tuone kama nasi tuna deni kubwa. Tunasema wachezaji wa Yanga watambue umuhimu wa mchezo wa marudiano na nafasi yao ya kuzidi kuwatangaza kimataifa.
    Ni imani yetu kwamba benchi la ufundi la Yanga likiongozwa na Hans Pluijm litakuwa imara kuhakikisha wachezaji wanacheza kwa ushirikiano na uelewano dimbani. Kikubwa ni kwamba tunakutana na timu ambayo si mara ya kwanza kukutana nao, tumecheza nao kwao, tunawafahamu vizuri, lakini zaidi ni Waafrika wenzetu na tuliwafunga kwao.
    Wanaocheza uwanjani ni wachezaji 11 kila upande, hivyo hatudhani kama tuna haja ya kuingia tukiwa wanyonge, wala hatuna sababu ya kuhofia chochote. Tupo nyumbani tupate ushindi mnono.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment