Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya |
TUME ya Vyuo Vikuu (TCU), imefuta kibali kilichoanzisha Chuo Kikuu cha St Joseph tawi la Arusha na kuahidi kuhamishia wanafunzi 1,557 wa chuo hicho kwenda vyuo vingine.
Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya alisema, hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo migogoro ya muda mrefu baina ya uongozi wa chuo hicho na wanafunzi.
“TCU inapenda kuutaarifu umma kuwa imekifungia chuo hicho kwa kuwa hakina uwezo wa kutoa elimu ya juu na wanafunzi ndio waathirika wakuu,” alisema.
Kutokana na hatua hiyo, Profesa Mgaya alisema wameanza kuhamisha wanafunzi na kuwapeleka kwenye vyuo vingine na kuwataka wanafunzi hao kuangalia mtandao wa TCU kubaini vyuo walivyopangiwa na kabla ya kuhamia vyuo hivyo, wakamilishe taratibu zote.
Alisema, tume imekuwa ikifuatilia kwa karibu migogoro hiyo na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa uongozi wa chuo kurekebisha kasoro zinazosababisha migogoro chuoni hapo.
Katika kutekeleza azma hiyo, tume iliunda jopo la wataalamu kufanya ukaguzi wa kina katika chuo kikuu hicho na ripoti ya ukaguzi huo iliwasilishwa Februari 22 mwaka huu.
Baada ya kupokea ripoti hiyo na kuifanyia kazi, Profesa Mgaya alisema waliofikia uamuzi huo kwani uongozi wa chuo hicho, licha ya kushauriwa na TCU kurekebisha kasoro zilizopo, haukuchukua hatua husika.
Wiki hii wanafunzi 1,548 wa chuo hicho waligoma kuingia darasani kwa siku tatu na kukodi mabasi matatu kwa nia ya kutaka kufika Dar es Salaam kumwona Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Lengo la safari yao hiyo ya Dar es Salaam, ilikuwa ni kujua hatma yao baada ya TCU, kufungia chuo hicho tawi la Songea.
Hata hivyo, Profesa Mgaya aliwataka kuwa watulivu na kuahidi kuzungumzia hatma ya chuo hicho jana, baada ya tume hiyo kupitia mapendekezo ya wataalamu iliyoundwa mapema kwa ajili ya ukaguzi wa chuo hicho, tawi la Arusha.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment