Rais wa Bolivia Evo
Morales ameshindwa kwenye kura ya maamuzi ya kumruhusu kuwania urais
kwa muhula wa nne, utafiti wa matokeo unaashiria.
Kura moja ya
matokeo inaonesha asilimia 52.3 ya wapiga kura wamepinga jaribio la
kufanyia marekebisho katiba, huku kura nyingine ikionesha asilimia 51
wamepinga jaribio hilo.Utafiti huo hufanywa kwa kuwauliza watu wamepiga kura upande upi baada yao kupiga kura.
Mabadiliko hayo kwenye katiba yangemruhusu Bw Morales, anayesema kwamba anahitaji muda zaidi kutekeleza mageuzi, kusalia madarakani hadi 2025.
Wafuasi wa upinzani wamekuwa wakisherehekea matokeo ya kura hiyo ya maamuzi katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu La Paz.
Bw Morales, anatoka jamii asili ya Aymara, na alichukua mamlaka Januari 2006.
Muhula wake wa sasa unamalizika 2020.
Bado anaungwa mkono na watu wengi, moja ya sababu ikiwa kwamba ni kiongozi wa kwanza wa nchi kutoka jamii asilia na pia kwamba uchumi umeimarika katika mwongo mmoja uliopita, Mhariri wa BBC Amerika Leonardo Rocha, anasema.
Lakini wengi walidhani Morales hafai kuruhusiwa kuongoza kwa miaka 19 mtawalia, mhariri huyo anasema.
Makamu wa rais Alvaro Garcia Linera ametoa wito kwa watu wasubiri matokeo rasmi.
“Kura za maoni, na hasa utafiti wa matokeo ya awali, wakati mwingine hukosea,” amewaambia wanahabari.
“Hawajazingatia kura kutoka nje ya nchi. Huwa hawaendi maeneo yasiyofikika kwa urahisi ambapo chama chetu kinaungwa mkono sana.
"Kuna uwezekano mkubwa kwamba matokeo ya kura hizo ni tofauti na hali halisi.”
Chanzo BBC Swahili.
0 comments:
Post a Comment