KESI za kupinga matokeo ya uchaguzi kwa nafasi za ubunge katika
majimbo matatu ya Nyamagana koa wa Mwanza, Longido mkoani Arusha na
Kigoma Kusini, zimeanza kunguruma mahakamani, huku mbili zikiahirishwa
kwa sababu mbalimbali na nyingine ikipangwa kuanza wiki ijayo.
Katika Jimbo la Kigoma Kusini, kesi hiyo imeshindwa kusikilizwa jana
kutokana na sababu za kisheria na imepangwa Machi 9 mwaka huu.
Aidha katika Jimbo la Longido, kesi ilikuwa ianze jana, lakini
iliahirishwa hadi keshokutwa kumpa Jaji husika nafasi kupitia jalada.
Kesi katika Jimbo la Nyamagana, imepangwa kuanza kusikilizwa Februari 29
mwaka huu.
Jimbo la Longido
Jana, kesi hiyo katika Jimbo la Longido iliahirishwa kwa siku tatu
baada ya Jaji Mfawidhi Kanda ya Bukoba, Sivangilwa Mwangesi aliyepangiwa
kuisikiliza, kutaka muda apitie jalada la kesi kufahamu hoja za msingi
katika kesi hiyo ya kwanza ya uchaguzi mkoani Arusha.
Jaji Mwangesi alisema hayo mbele ya Mahakama hiyo na kueleza kuwa
ameingia jijini Arusha juzi jioni, hivyo hajui kilichomo ndani ya jalada
hilo. Aliomba mawakili wampe siku tatu, kulisoma na kujiridhisha
kilichomo ndani na keshokutwa atoe mwongozo wa kesi hiyo.
“Ninawaomba mawakili wote mnipe siku tatu kulipitia jalada hili kubwa
mno ili niweze kulisoma na kujua kilichomo na Alhamisi wiki hii nitatoa
namna ya kuendesha kesi hii mpaka imalizike kwani niko hapa kwa ajili
ya kesi hii tu ya uchaguzi,” alisema Jaji Mwangesi.
Kutokana na ombi hilo, mawakili wote walikubaliana na hoja ya Jaji
Mwangesi ya kukutana keshokutwa kufahamu mwongozo wa uendeshaji wa kesi
hiyo. Ilielezwa pia kuwa huenda kesi hiyo ikasikilizwa mfululizo kuanzia
Februari 29 hadi itakapomalizika.
Mawakili wa aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Dk
Stephen Kiruswa, wametoa sababu 10 za kutaka matokeo ya uchaguzi huo
yatenguliwe. Mawakili hao ni Dk Masumbuko Lamwai, Edmund Ngemera na
Daudi Haraka.
Ilidaiwa kuwa miongoni mwa sababu ni kwamba baadhi ya watu waliopiga
kura katika jimbo hilo na kumchagua Onesmo Ole Nangole (Chadema),
walitoka nchi jirani ya Kenya.
Wakili
Haraka alidai sababu nyingine ni pamoja na masanduku ya kura kubebwa
na magari ya wafuasi wa Chadema na kura kutojumlishwa vizuri . Wanadai
siku ya kuhesabu kura, wagombea wote walitolewa, lakini mgombea wa
Chadema alibaki ndani ya chumba cha kuhesabu kura.
Sababu nyingine ni pamoja na wafuasi wa Chadema na mgombea wao,
kufanya siku ya kupiga kura wakati wakifahamu wazi kuwa ni kinyume na
utaratibu wa uchaguzi nchini . Inadaiwa mgombea wa Chadema, alitumia
lugha isiyokuwa na staha kipindi cha kampeni, ikiwemo matusi na
kumdhalilisha mgombea wa CCM.
Kutokana na sababu hizo, mawakili hao walimwomba Jaji kutengua ubunge
wa Nangole, kwa kuwa mgombea huyo aliyetangazwa kuwa mshindi wa jimbo
hilo, alikiuka taratibu zote za uchaguzi. Katika kesi hiyo, mjibu maombi
wa kwanza, Nangole anatetewa na mawakili wawili, ambao ni Method
Kimomogolo na Faustin Materu .
Mjibu maombi namba mbili ni msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Longido na
wa tatu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanaowakilishwa na Wakili
Mfawidhi Arusha, Juma Ramadhani na Fortunatus Mhalila.
Jimboni Nyamagana
Katika Jimbo la Nyamagana, kesi hiyo iliyofunguliwa na aliyekuwa
mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Ezekia Wenje dhidi ya Stanslaus
Mabula wa CCM, aliyetangazwa mshindi. Kesi imepangwa kusikilizwa kuanzia
Februari 29 mwaka huu.
Akizungumza jana na mawakili wa pande mbili na wananchi waliokwenda
mahakamani, kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Robert Makaramba alisema kesi hiyo
itaanza kusikilizwa kuanzia Februari 29.
Alisema jaji atakayesikiliza kesi hiyo, amepangwa na Jaji Kiongozi na
kesi hiyo itasikilizwa mfululizo. “Mimi siyo Jaji niliyepangiwa
kusikiliza kesi hii, Jaji aliyepangiwa anatarajiwa kuwasili leo (jana)
jioni hapa jijini Mwanza, haina haja ya kumjua kwa sasa”, alisema Jaji
Makaramba.
Alisema Serikali imepanga majaji kusikiliza kesi hizo za uchaguzi kwa
uharaka zimalizike kwa wakati. Alisema jaji huyo atakapowasili jijini
Mwanza, atakutana na mawakili wa pande zote kupanga utaratibu wa
kusikiliza kesi hizo.
“Jaji Kiongozi ndiye aliyemteua jaji wa kusikiliza kesi hii, na mara
baada ya kuwasili atakutana na mawakili wa pande zote mbili ili wapange
namna ya kusikiliza kesi hizi kwa haraka,” alisema Jaji Makaramba.
Aliwataka mawakili hao kuangalia ratiba za utendaji kazi wao kwa kile
alichosema, kesi hiyo itakapoanza itakuwa na vikao vya mfululizo hadi
kufikia uamuzi wa kutolewa kwa hukumu.
Katika kesi hiyo, Wenje anatetewa na mawakili wawili; Deya Outa na
Elias Hezron huku Mabula akitetewa na mawakili wawili, ambao ni
Constantino Mtalemwa na Faustine Malongo.
Serikali katika kesi hiyo, inawakilishwa na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Bilishanga. Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi,
ilifunguliwa na Wenje akipinga ushindi wa Mabula kwa madai kuwa uchaguzi
huo haukuwa wa huru na haki. Wenje anadai alipokonywa ushindi wake
katika uchaguzi huo.
Jimbo la Kigoma
Kusini Ilielezwa kuwa, kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi Namba
2 ya mwaka 2015, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi
ya NCCR –Mageuzi, David Kafulila katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda
ya Tabora, ilishindwa kuanza kusikilizwa kutokana na sababu za kisheria.
Imeahirishwa hadi Machi 9 mwaka huu.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Mkoa Kigoma, Silvestre Kainda, alisema kuwa kuahirishwa
kuanza kusikilizwa kwa kesi kunatokana na pande zote mbili kukubaliana
kurekebisha dosari za kisheria zilizojitokeza.
Kainda alitaka wananchi watulie na kesi itasikilizwa tarehe hiyo kama ilivyopangwa.
Akizungumza kuhusu kuahirishwa kwa kesi hiyo, Profesa Abdallah Safari
ambaye ni Wakili wa Kafulila, alidai kumetokana na kutofika mahakamani
kwa wadau muhimu ambao kisheria wanapasa kuwepo mahakamani.
Aliwataja walioshindwa kufika mahakamani ni Mwakilishi wa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Wakili wa Msimamizi wa Uchaguzi na Wakili wa
mlalamikiwa, Kennedy Fungamtama ambao kisheria wanapaswa wawepo
mahakamani wakati shauri hilo likianza kusikilizwa.
Kwa upande wake, Kafulila alisema kuwa kuahirishwa kwa kesi hiyo
kunarudisha nyuma maagizo ya Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi ya kutaka kesi
hizo za uchaguzi , zisikilizwe haraka na kumalizika katika muda mfupi.
Kesi hiyo iliyo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Ferdinand Wambari,
Kafulila anaitaka Mahakama imtangaze mshindi kwa madai kwamba,
aliyetangazwa kupitia CCM, Husna Mwilima, hakuwa halali.
Imeandikwa na Fadhili Abdallah, Kigoma, Nashon Kennedy, Mwanza na John Mhala, Longido.
Credit; HabariLeo.
Monday, 22 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment