Mwnyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Tanzania Standard(Newspaper) Ltd. inayochapicha magazeti ya Serikali ya Daily News, Sunday News,
HabariLeo na SpotiLeo, Profesa Moses Warioba, (kushoto) akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana.
VIGOGO wa Chuo cha Utumishi wa Umma na wa Kampuni ya Magazeti ya
Tanzania Standard (Newspapers) Limited (TSN), wamesimamishwa kazi kwa
tuhuma za utendaji usioridhisha.
Uamuzi dhidi ya mabosi hao wa taasisi za serikali, ulichukuliwa jana
na mamlaka zenye dhamana, huku upande wa Chuo cha Utumishi wa Umma,
akiwa amesimamishwa Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Said Nassoro na
kwa TSN akisimamishwa Mhariri Mtendaji, Gabriel Nderumaki.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela
Kairuki alimsimamisha Mkuu huyo wa Chuo, Nassoro, kwa madai ya kushindwa
kusimamia utendaji wa chuo na kusababishia Serikali hasara ya zaidi ya
Sh bilioni moja.
Kwa upande wa TSN, Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni hiyo imemsimamisha
kazi Mhariri Mtendaji wa taasisi, Gabriel Nderumaki kwa tuhuma ya
utendaji usioridhisha.
Vigogo Utumishi
Licha ya Waziri Kairuki kumsimamisha Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa
Umma, Nassoro, pia amewasimamisha kazi watumishi wengine wawili ambao ni
Mkuu wa Chuo hicho Kampasi ya Dar es Salaam , Joseph Mbwilo na
aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho Kampasi ya Tabora, Silvanus Ngata ambaye
amerejeshwa makao makuu ya utumishi wa umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kairuki
alisema kutokana na Nassoro kushindwa kusimamia, utendaji wa chuo hicho
umekuwa si wa kuridhisha hali iliyochangia baadhi ya watumishi wake
kujiingiza kwenye ubadhirifu wa mali ya umma.
“Chuo hiki ni muhimu sana katika kuleta ufanisi wa utendaji kwa
mtumishi wa umma, kutokana na utendaji huu usioridhisha umetoa mwanya
kwa baadhi ya watendaji kufanya ubadhirifu,” alisisitiza Kairuki.
Akizungumzia ubadhirifu huo, Kairuki alisema mwaka 2011 hadi 2013,
Ngata alijiongezea gharama za ujenzi wa jengo la chuo hicho tawi la
Mtwara tofauti na fedha iliyokuwa imepangwa.
“Cha kushangaza, huyu Mkuu wa Chuo ambaye ni Nassoro baada ya
kugundua kosa hilo, alishindwa kumwajibisha na badala yake alimhamishia
tawi la Chuo cha Tabora akiendelea tena kama Mkuu wa chuo hicho,”
alisema Waziri.
Aidha waziri huyo alisema amemsimamisha kazi Mbwilo kwa kitendo chake
cha kutumia vibaya Sh bilioni moja za chuo hicho katika mwaka wa fedha
wa 2013/3014 ambazo zilikuwa malipo ya ada.
Alisema licha ya ubadhirifu huo, Nassoro alimteua Mbwilo kuwa Kaimu
Mkuu wa Chuo kwa upande wa fedha Kampasi ya Dar es Salaam. Kairuki
alisema wizara yake itaendelea kusafisha watumishi wa umma wasio
waaminifu. “Sisi tulio hapa utumishi wa umma ndio tunaoweka mifumo na
miongozo mbalimbali ya utumishi. Ni lazima tuoneshe mfano,” alisisitiza.
Wakati Waziri Kairuki akitumbua majipu hayo, Mkuu huyo wa Chuo cha
Utumishi wa Umma, Nassoro alikuwepo kwenye mkutano huo na wanahabari,
hali ambayo ilionesha hakufahamu kitakachotokea.
Baada ya Waziri Kairuki kutoa taarifa hiyo, mtendaji huyo alisimama,
akainama kama ishara ya kutoa shukurani ya heshima na kutoka ukumbini
hapo akisindikizwa na watumishi wengine waliohudhuria mkutano huo.
Kuhusu TSN
Uamuzi wa kumsimamisha Mhariri Mtendaji wa TSN, Nderumaki, ulifanyika
muda mfupi baada ya ziara ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye aliyefika kwenye kampuni kuangalia utendaji na
namna ya kuboresha utendaji wa kampuni. Kabla ya uamuzi huo kufanyika,
Nape alizungumza na menejimenti katika kikao cha ndani na kisha akaitaka
Bodi ya Wakurugenzi wa TSN iliyo chini ya Mwenyekiti, Profesa Moses
Warioba kukaa kupitia hoja zilizoibuka kwenye kikao hicho.
“ Nimeiagiza bodi watafakari juu ya anayeongoza menejimenti ,
ukiangalia ripoti inaonekana kuna mgogoro mkubwa ndani ya menejimenti
yenyewe, na kumekuwapo na malalamiko ya wafanyakazi,” Nape aliwaambia
waandishi wa habari. Alisema, “Taarifa nilizokuwa nazo, niliiomba bodi
iwepo ili tupitie pamoja maeneo dhaifu ya utendaji kazi katika kampuni.
Naamini kuna uamuzi Bodi itayatengua.”
Waziri Nape alisema kutokana na ripoti, amebaini kuwapo matatizo
makubwa, ikiwemo kukosekana mawasiliano kati ya bodi na menejimenti. Pia
alibaini utendaji mbovu wa menejimenti, uliochangia kushusha ari ya
kazi ya wafanyakazi.
“Kuna baadhi maamuzi yamefanywa na menejimenti ambayo yangetakiwa
kufanywa na bodi na ili bodi iwe na maelekezo yake, na bahati mbaya
sehemu kubwa yamefanyika bila ushiriki wa bodi na inaonekana hakuna
mawasiliano mazuri kati ya bodi na menejimenti. Udhaifu huu umechangia
kushusha morali (ari) ya wafanyakazi, ukiangalia wafanyakazi wanaocha
kazi imeongezeka na ndiyo jambo ambalo limetushtua sana. Tunataka bodi
ikae ilitafakari hilo,” alisema.
Waziri Nape aliahidi Februari 29 mwaka huu atakutana na kuzungumza na wafanyakazi wa TSN.
Uamuzi wa Bodi
Baada ya kikao cha Bodi cha takribani saa mbili, Mwenyekiti wa Bodi ,
Warioba alisema wameamua kumsimamisha Nderumaki, kupisha uchunguzi
ambao utafanywa na Serikali.
“ Bodi imeamua kumsimamisha Mhariri Mtendaji ili kupisha uchunguzi
stahiki na hatimaye hatua stahiki zichukuliwe na mamlaka yake ya ajira.
Uchunguzi unafanywa kuangalia ni kwa nini hali imekuwa hivyo katika
kampuni,” alisema.
Katika kipindi cha uchunguzi, nafasi ya Mhariri Mtendaji itashikiliwa
na Tuma Abdallah ambaye kwa sasa ni Naibu Mhariri Mtendaji.
Uteuzi mwingine
Wakati huo huo, Bodi hiyo imetengua uteuzi uliofanywa na Mhariri
Mtendaji kwa Madiya Magesa, aliyekuwa Kaimu Meneja wa Kiwanda wakimtaka
arejee katika nafasi yake ya Uhasibu kutokana na kukosa sifa.
Magesa alipewa wadhifa huo kutokana na kusimamishwa kazi kwa Meneja
wa Kiwanda, John Mcharo. Hata hivyo Warioba alisema taratibu za
kisheria, zitafuata katika kumpata mtu atakayeshika wadhifa huo.
Pia, Bodi imetengua uteuzi wa Felix Mushi aliyeshikilia nafasi ya
Kaimu Meneja Mauzo na Masoko, ambaye alisema mbali na kutokuwa na sifa,
pia uadilifu wake unatiliwa shaka.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi, Warioba alisema Waziri Nape alitoa
maelekezo ya mambo mengi yaliyotakiwa kufanyiwa kazi, ikiwamo kutokuwapo
kwa maelewano kati ya manejimenti, wafanyakazi na Chama cha Wafanyakazi
(RAAWU).
Mengine ni, baadhi ya wafanyakazi kupewa majukumu ambayo hawana sifa,
kumsimamisha kazi meneja wa kiwanda bila kufuata taratibu na kuangalia
sababu za wafanyakazi zaidi ya 21 kuacha kazi katika kipindi cha muda
mfupi.
Chanzo HabariLeo.
Monday, 22 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment