Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HATUA ya kutoonekana kwa Rais Dk. John Magufuli katika sherehe ya
kutakiana heri ya mwaka mpya na wanadiplomasia (Sherry Party), imezua
mjadala mzito miongoni mwa Watanzania.
Kutokana na kutokuwapo kwa rais katika sherehe hiyo iliyofanyika juzi
Ikulu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga,
alimwakilisha na alisoma hotuba kwa niaba yake.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, alisema ilikuwa ni sahihi kwa
Rais Magufuli kuwakilishwa na Waziri Mahiga katika sherehe hiyo.
Alisema hatua hiyo ilitokana na Rais Magufuli kuwa nje ya Dar es
Salaam, ambapo asipokuwapo huwakilishwa na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu
au Waziri wa Mambo ya Nje.
“Rais alikuwa nje ya Dar es Salaam ndiyo maana akawakilishwa na
Waziri wa Mambo ya Nje na ‘Sherry Party’ ni hafla ya kutakiana heri ya
mwaka mpya na wanadiplomasia.
“Na Cocktail (mchapalo) hufanyika kila mwaka na huwa ya muda mfupi
ambao wanadiplomasia husikiliza hotuba ya rais kuhusu sera yake ya mambo
ya nje. Hivyo kwa kuwa Rais Magufuli hakuwepo, hotuba yake ilisomwa na
Waziri Mahiga jambo ambalo ni sahihi na hakuna kosa lolote,” alisema
Msigwa.
Akizungumza suala la mabalozi hao kuwekewa makatarasi chini, alisema
si karatasi za kawaida, huwa zimeandikwa jina la balozi au nchi
anayowakilisha ambapo hutakiwa kusimama katika eneo lake husika
alilopangiwa.
“Suala la kuwekewa karatasi mbele si geni, huwa linafanyika kila
mwaka na pindi zinapowekwa huandikwa jina na cheo cha mwanadiplomasia
anayewakilisha nchi husika, na baada ya kusomwa hotuba hupita mbele na
kumpa mkono kiongozi.
“Na kwa jana (juzi), aliyesimama mbele alikuwa ni Mheshimiwa Waziri
Dk. Mahiga, naibu waziri pamoja na mkuu wa itifaki, na walifanya hivyo
kwa sababu walikuwa wakimwakilisha Rais Magufuli katika hafla,” alisema.
Balozi Cisco atoa maoni
Aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Falme za Kiarabu,
Abdul Cisco Mtiro, alisema alichofanya Rais Magufuli kutuma mwakilishi
katika hafla hiyo haijawahi kutokea tangu Serikali ya awamu ya kwanza
hadi ya nne.
“Ni kweli Rais Magufuli ndiye kwa mara ya kwanza amefanya kitu
tofauti na marais wote waliomtangulia kutuma mtu kwa niaba yake, hiyo
haijawahi kutokea,” alisema Balozi Mtiro.
Balozi Mtiro ambaye ni mwanadipomasia aliyebobea, alisema hafla hizo
ambazo hufanyika kila mwaka humwezesha rais husika kutoa mwelekeo wa
nchi yake katika sera ya Serikali kuhusu mambo ya nje.
“Sherry Party ni Standard Party na kwa kawaida huchukua dakika
zisizozidi 30 ambapo rais hatoa ‘speech’ (hotuba) ya dakika tano
kuelezea mwelekeo wa sera ya nchi yake kuhusu mambo ya nje na baadaye
hupeana mkono na mabalozi na kuondoka.
“Sherry Party ni hafla ambazo hufanyika kila mwaka ambapo ambapo rais
anakutana na mabalozi, hakuna viti, ndiyo maana uliona vile vikaratasi
vya majina ya mabalozi kuwekwa pale ingawa utaratibu ni kwamba mabalozi
wenyewe wanajua utaratibu kwamba nani alitangulia kutoa hati za
utambulisho katika lile kundi, ndiyo wanafuata wengine kadiri
walivyoingia nchini.
“Ni utamaduni wa nchi za Jumuiya ya Madola, na Uingereza ambako ndiko
tulichukua utamaduni huo, zamani ilitumika soda na maji, lakini miaka
ya karibuni vinawekwa pia vinywaji vikali,” alisema.
PROFESA LIPUMBA
Akizungumza hali hiyo katika moja za makala zake, Mwenyekiti mstaafu
wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema mabalozi
wengi waliopo hapa nchini na ambao nchi zao zinaisaidia Tanzania
wameomba fursa ya kukutana na Rais Magufuli lakini wamekwama.
Kutokana na hali hiyo alisema kiongozi huyo wa nchi ameendelea
kuwabeza mabalozi waliopo hapa nchini kwa kutohudhuria sherehe maalumu
‘Sherry Party’ ambayo rais huwaandalia mabalozi na kuwaeleza sera na
malengo yake ya kuboresha uhusiano wa Tanzania na mataifa ya nje.
“Katika Sherry Party ya mwaka huu, rais kawakilishwa na Dk. Mahiga,
Waziri wa Mambo ya Nje. Kwa kuwa Rais Magufuli ndiyo kaingia madarakani,
mabalozi wengi walikuwa na shauku ya kumuona na kumsikiliza,” alisema.
HOTUBA YA MAGUFULI
Katika hotuba yake kwa wanadiplomasia hao iliyosomwa na Waziri Mahiga
juzi, Rais Magufuli alisema hatua ya kurudia uchaguzi Zanzibar ndiyo
njia sahihi ya kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani humo.
Alisema kufanyika uchaguzi huo wa marudio kutasaidia kuondoa mvutano
wa kisiasa uliopo na kusisitiza kuwa mazungumzo kati ya vyama vya siasa
yaliyoanza Novemba mwaka jana, hayakufikia mwafaka wa namna ya kutatua
tatizo hilo.
“Zanzibar ina mfumo wake wa siasa, ina Katiba na ina Tume Huru ya
Uchaguzi. Hatua ya kufanya uchaguzi ndiyo njia sahihi katika hali ya
sasa katika kumaliza tatizo hilo.
“Chama kikuu cha upinzani (CUF) wanadai wameshinda, lakini chama
tawala na vyama vingine vinaona haja ya kufanya uchaguzi wa marudio ili
kuondoa kasoro,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema mlango wa mazungumzo juu ya namna ya kufanya uchaguzi wa
marudio kuwa huru na haki na kufuata taratibu za kimataifa uko wazi na
kuwa ni imani yake nchi marafiki wa Zanzibar na Tanzania wataunga mkono
juhudi hizo.
“Kama ilivyo kwa Watanzania wengi wanavyoona, njia ya kuthibitisha
ushindi ni boksi la kura na kukataa kushiriki ni kukataa kufikia mwafaka
na Serikali na kujinyima haki ya miaka mitano ijayo,” alisema Rais
Magufuli.
Alisema bado kuna siku 40 ambazo zinatosha kuwa na mazungumzo ya kuja na suluhisho la tatizo hilo.
Zanzibar inatarajia kufanya uchaguzi wa marudio Machi 20 kutokana na
uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mabalozi waliopo nchini, ambaye pia ni
Balozi wa Zimbabwe, Edzai Chimonyo, alisema mgogoro wa Zanzibar unaweza
kumalizwa kwa mazungumzo ya pamoja visiwani humo.
Alisema wananchi wa Zanzibar wanapaswa kuweka tofauti zao pembeni na kujali masilahi ya nchi kwa masilahi yao na taifa lao.
Chanzo Mtanzania.
Tuesday, 9 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment