MASHAURI 13 ya uchaguzi wa wabunge yanatarajiwa kuanza kunguruma leo katika kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania nchini.
Miongoni mwa mashauri yatakayonguruma ni yale yaliyofunguliwa na
aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila, aliyekuwa mgombea
ubunge Iringa Mjini Fredrick Mwakalebela, aliyekuwa Mbunge wa Kahama
James Lembeli, aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje na aliyekuwa
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugetta wiki
iliyopita, mashauri hayo yataanza kusikilizwa kwa njia ya vikao vya
Mahakama Kuu katika vituo mbalimbali vya Mahakama hiyo nchini.
Mugetta alizitaja kesi zitakazoanza kusikilizwa kuwa ni kesi ya
kupinga matokeo ya ubunge wa Longido yaliyompa ushindi Onesmo ole
Nangole (Chadema) iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Stephen
Kiruswa.
Itasikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha. Aidha, alisema kesi
nyingine ni ile ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na
Benedicto Mutungirehi (Chadema) dhidi ya mshindi wa ubunge katika Jimbo
la Kyerwa, Innocent Bitakwate (CCM). Kesi hiyo itasikilizwa Bukoba.
Mkoani Iringa, pia kutakuwa na kesi iliyofunguliwa na Mwakalebela ya
kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi wa ubunge katika Jimbo
la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Alitaja kesi nyingine kuwa ni ya kupinga matokeo ya ubunge
inayomkabili Mbunge wa Njombe, Edward Mwalongo (CCM) iliyofunguliwa na
Emmanuel Godfrey (Chadema).
Kesi nyingine ni ile ya kupinga matokeo ya ubunge katika Jimbo la
Mafinga, iliyofunguliwa na William Mungai (Chadema) dhidi ya mbunge wa
jimbo hilo, Cosato Chumi wa CCM.
Pia kesi iliyofunguliwa na Zella Abraham ya kupinga matokeo ya ubunge
Mbeya Vijijini dhidi ya Oran Njeza nayo itasikilizwa na kesi nyingine
ni iliyofunguliwa na Fanuel Mkisi dhidi ya ushindi wa ubunge katika
Jimbo la Vwawa wa Japhet Hasunga. Kesi hizi zitasikilizwa Mbeya.
Aidha, kesi nyingine zitakazoanza kusikilizwa siku hiyo ni pamoja na
kesi dhidi ya Mbunge wa Newala, George Mkuchika iliyofunguliwa na Juma
Manguya anayepinga ushindi wa mbunge huyo na kesi iliyofunguliwa na
Mangungu dhidi ya ushindi wa matokeo ya ubunge Kilwa yaliyompatia
ushindi Vedastor Ngombale wa CUF.
Pia Msajili huyo alisema kesi nyingine ni ile iliyofunguliwa na Wenje
ya kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Stanslaus Mabula (CCM)
itakayosikilizwa Mwanza wakati kesi iliyofunguliwa na Lembeli ya kupinga
matokeo ya ubunge Kahama yaliyompatia ushindi Jumanne Kishimba
itasikilizwa Shinyanga.
Kesi nyingine zilizopangwa kusikilizwa ni iliyofunguliwa na Kafulila
kupinga matokeo ya ubunge Kigoma Kusini yaliyompatia ushindi Husna
Mwilima wa CCM na kesi yao itasikilizwa Tabora wakati kesi
iliyofunguliwa na Amina Mwidau kupinga matokeo ya ubunge Pangani
yaliyompatia ushindi Jumaa Aweso wa CCM itasikilizwa Tanga.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo mbali na washindi wa ubunge ni
pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi katika
Jimbo husika.
Hivi karibuni, Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman alisema tayari
Mahakama hiyo imejipanga kumaliza kesi zote za uchaguzi hadi Juni mwaka
huu, na imejipanga kusikiliza kesi 20 za wabunge.
Tangu uchaguzi huo umalizike Oktoba mwaka jana, jumla ya kesi 221
zilifunguliwa kati ya hizo 53 ni za ubunge na 173 madiwani na jumla ya
Sh bilioni tatu zinahitajika kukamilisha usikilizaji wake.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 21 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment