Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu amesema kambi hiyo
haitaongoza kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za
Serikali za Mitaa (Laac) hadi ofisi ya Spika itakapobadilisha uteuzi wa
wajumbe wa kamati hizo.
Kwa mujibu wa mabunge ya Jumuiya za
Madola, kamati hizo huongozwa na wapinzani, lakini tangu Spika wa Bunge,
Job Ndugai afanye uteuzi wa wajumbe, kambi hiyo imesusia kushiriki
uchaguzi kwa kile wanachokiita “kupangiwa wajumbe”.
Jana, Kaimu
Katibu wa Bunge, John Joel alisema mazungumzo kati ya ofisi ya spika na
kambi hiyo bado yanaendelea na kusisitiza kwamba uteuzi huo unaweza
kutenguliwa au kuachwa kama ulivyo.
Katika maelezo yake, Lissu alisema
licha ya kambi hiyo kuwa katika mazungumzo na ofisi ya spika, suluhisho
halijapatikana na kusisitiza kuwa msimamo wao upo palepale.
“Hatujafika
popote. Msimamo wetu uko palepale na hatutakubali kuchaguliwa viongozi
wa hizo kamati na CCM, kama wanafikiria ni lazima iwe wanavyotaka sisi
hatutakubali,” alisema.
Joel aliwahi kunukuliwa na na vyombo vya habari
akisema kuwa kama kambi hiyo itasusia uchaguzi, shughuli za kamati
zitafanywa na makamu wenyeviti ambao wanatokea CCM.
“Ni bora
tusiziongoze kabisa kamati hizi. Ukifuatilia utabaini kuwa katika PAC na
Laac tuna wajumbe sita kila kamati kati ya wajumbe 23, wakati huohuo
kamati ya Ukimwi tumepewa wajumbe 12 kati ya wote 23,” alisema Lissu.
Alisema
wajumbe sita waliopo katika kamati ya Laac na PAC wameteuliwa na CCM na
kama kamati hizo zinaongozwa na upinzani ni lazima wapinzani
wajichagulie wajumbe wao, wakiwamo watakaochaguliwa kuwa wenyeviti.
Alisema wabunge wana haki sawa, lakini hawana uwezo sawa.
Lissu
ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema uamuzi wa
spika kuwapangia wajumbe katika kamati hizo hauna nia nzuri na kwamba,
huenda ni mkakati wa ofisi hiyo kuifanya Serikali iwe inapitisha mambo
yasiyofaa bungeni.
Februari Mosi mwaka huu, Kambi ya Upinzani
bungeni ilisusia uchaguzi wa viongozi wa kamati hizo kwa maelezo kuwa
Spika Ndugai alifanya uteuzi ‘kiholela’ na kuahidi kutoshiriki mpaka
pale watakapopewa idhini ya kupendekeza wenyeviti.
Credit;Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment