Wednesday, 10 February 2016

Tagged Under:

Yanga yaipigia hesabu Simba

By: Unknown On: 22:30
  • Share The Gag
  • Kikosi cha Yanga

    MCHECHETO wa mechi ya Ligi Kuu kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga umeifanya Yanga kukodi ndege maalumu kwenda Mauritius kesho kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim utakaochezwa keshokutwa.
    Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema wameamua kukodi ndege maalumu kwa shughuli hiyo ambapo sasa wataondoka Ijumaa kwenda Mauritius badala ya jana kama ilivyoripotiwa awali.
    “Shirika la Ndege la Afrika Kusini limeshindwa kutupatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg kwenda Curepipe, Mauritius, badala yake timu ingelazimika kusubiri kwa saa saba na wakati wa kurudi badala ya kufika Jumapili tungefika Jumatatu, jambo ambalo lingefanya timu ikose siku tano za kujiandaa na michezo mitatu ambayo inatukabili mmojawapo ni wa Simba,” alisema Muro.
    Yanga inatarajia kucheza na Simba katika mechi ya ligi Februari 20, pia itakuwa na mechi dhidi ya Mtibwa na Azam.
    Pia Muro alikiri kukodi ndege binafsi ni gharama, lakini wamelazimika kufanya hivyo ili kukwepa hujuma ambazo wameona dalili zake na kumpa muda kocha kuendelea na programu yake kiufasaha na kuepuka uchovu kwa wachezaji.
    Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi saa 9:30 Alasiri katika Uwanja wa Curepipe na baada ya mchezo huo timu itaondoka na kufikia kambini Pemba kabla ya kuanza mazoezi Jumapili mapema.
    “Kocha ameendelea na programu yake leo (jana) na kesho (leo) na Ijumaa wataondoka na watafikia kwenye kambi maalumu ambayo tumeandaa ikiwa na wapishi wetu na baada ya mechi watapanda ndege kwani itakuwa inawasubiri tayari kurudi na watafikia kambini Pemba,” alisema Muro.
    Muro alisema Yanga wanakabiliwa na mchezo dhidi yao na Yanga, Mtibwa Sugar na Azam FC hivyo wanatakiwa kujiandaa vya kutosha kwani michezo muhimu na ligi imekuwa na ushindani.
    Wachezaji Benedicto Tinocco ambaye ni kipa namba tatu na mshambuliaji Matheo Anthony na kiungo Godfrey Mwashiuya wanakosa safari hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa pasi ya kusafiria.
    Wachezaji waliokuwa majeruhi, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Amissi Tambwe wote watasafiri na timu na mkuu wa msafara ni Ayoub Nyenzi, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Kikosi kinachokwenda Mauritus ni Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’. Mabeki ni Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Vincent Bossou na Pato Ngonyani.
    Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Issoufou Boubacar na Deus Kaseke. Washambuliaji ni Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment