Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. |
KUANZISHWA kwa chama chochote cha siasa malengo yake ya kudumu na ya mwisho ni kushika dola na kuiongoza. Ili chama kiweze kuaminiwa na wananchi kushika dola lazima chenyewe kijiamini kupitia watu wake, yaani viongozi.
Lakini jambo hili kwa hoja zitakazoelezwa hapa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kama chama cha Upinzani kinachotafuta ridhaa ya wananchi kuweza kuongoza taifa kila mwaka wa uchaguzi hakionekani kujiamini chenyewe kama chenyewe. Mambo yafuatayo yanadhihirisha kutokuaminiana.
Lowassa kuwa mgombea Urais Kitendo cha chama hicho kumteua mtu ambaye amekuwa mwanachama wa chama hicho kwa takribani siku tano na kuwa mgombea wa urais si tu kwamba kilionesha ni kwa namna gani chama hicho kilikuwa hakina watu makini wa kupeperusha bendera ya chama hicho bali kinastahili kuingia kwenye rekodi za kidunia maana si jambo la kawaida uteuzi na msimamo wa chama kubadilishwa na mtu mmoja ndani ya siku chache.
Kwa hakika katika hili, Edward Lowassa aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwa kipindi kifupi sana anastahili kupewa hata tuzo ya kuwa mshawishi mkubwa wa mwaka wa Chadema (Chadema lobbyist of the year). Kama hilo halitoshi Lowassa ameendelea kutoa maagizo na amri ilhali yeye ni mwanachama wa kawaida tu. Hili linaleta hisia kwamba endapo akipewa chama anaweza kutangaza lolote atakalo ndani ya chama.
Suala hili la nafasi ya Lowassa baada ya uchaguzi, hasa endapo kingelishindwa uchaguzi lilijadiliwa sana wakati wa kampeni lakini Chadema haikuwasumbua maana hawakuwa na uhakika na mtu gani wamsimamishe. Kwa ufupi labda walikuwa na upungufu wa watu wenye uwezo wa kuwa rais. Umeya Dar es Salaam Sakata la umeya nalo limedhihirisha kwamba Chadema imejaa watu ambao hawaaminiani pamoja na kwamba ni viongozi.
Kama viongozi mlioaminiwa na wananchi hawaaminiani itakuwaje kwa wanachama wa kawaida? Na kama hawaaminiani kwenye nafasi hizi ndogo nchi wangeiweza? Hofu ni kwamba chama kingeweza kupata mawaziri ambao wangerubunika kirahisi kuuza siri hata za nchi! Wengi wanaonekana kusifia kitendo cha Chadema kutumia kalamu za kamera na kuwafungia kambini madiwani na kisha kuwapokonya simu zao kabla ya uchaguzi wa umeya wa Kinondoni na Ilala madiwani wake.
Ni mkakati mzuri kwa maana umewasaidia kushinda. Lakini, kama alivyonukuliwa na vyombo vya habari, Halima Mdee, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na viongozi wengine wa chama hicho, walifanya hivyo kwa hofu ya kusalitiana na hatimaye ushindi kwenda CCM. Jambo hili ni hatari kwa chama cha siasa kufikia hatua ya kutokuaminiana kiasi hicho ilihali mpinzani wako unamzidi wapiga kura zaidi ya kumi.
Kwa mfano, kwa Dar es Salaam nzima Chadema, kwa maana ya chama hicho na washirika wake wanaounda umoja wao maarufu kwa jina la Ukawa, ina madiwani takribani 84 na CCM 74. Hii pia inaonesha kwamba madiwani wa Ukawa wengi wao ni dhaifu na wapenda rushwa sana maana kama unafikia mkakati wa kumdhibiti kiasi hicho maana yake ni kwamba viongozi wa chama hawaaminiani hata kwa chembe ya haradani.
Je, Chadema itaendelea kutokuaminia hivi mpaka lini? Nyongeza ya hilo, Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob amekaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba CCM walitaka kumpa rushwa ya milioni 40 ili Ukawa ishindwe. Kitendo tu cha watu kuthubutu kukufuata ili wakuhonge walishakutathmini na kuona una uelekeo huo. Suala hili wala halikuwa sifa nzuri. Kwangu mimi naliona kama sifa mbaya kwa mwanasiasa kama Jacob.
Kamati za kudumu za Bunge Chadema kuanza kulalama juu ya uteuzi wa kamati kunaonesha kwamba kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kuziba udhaifu uliokuwepo huko nyuma, ina kazi ya ziada, maana walizoea mteremko wa kukosoa kosoa. Sasa utakosoa nini wakati ulikuwa ukipata umaarufu wa kisiasa kwa matukio ambayo yameshakuwa adimu katika kipindi hiki na bila shaka yataendelea kuwa adimu.
Inahisiwa ni sababu hizi zinazowafanya Chadema waanze kulia na kamati mbili tu za PAC na LAAC kana kwamba kuna watu waliumbwa wawe tu wenyeviti wa kamati hizo au kamati zingine hazina maana yoyote zaidi ya hizo mbili. Niulize kuna mtu alizaliwa au alichaguliwa ili awe mwenyekiti wa kamati fulani? Nijuavyo mimi sote tulizaliwa uchi na nguo tumezikuta duniani, hivyo hivyo, umechaguliwa kuwa mbunge.
Kama ndivyo, uwaziri au uenyekiti wa kamati ni majaliwa. Sambamba na sababu hizo, Chadema tena katika hili wameonesha tena tabia ya kutokuaminiana pamoja na kutengeneza madaraja kwamba kuna wabunge daraja la kwanza wanaostahili kamati fulani na wengine daraja la pili, la tatu na kuendelea labda mpaka wabunge wa daraja sifuri ndani ya Chadema ndio wa madaraja kama ya Ndalichako na GPA.
Hili ni suala la kushtua kwa chama kilichokua kinataka kushika dola, hivi inakuwaje mpaka mbunge fulani anaonekana hastahili na mwingine anastahili katika kamati fulani? Kwa hiyo wakati wa kampeni tuseme Chadema walitudanganya kwamba wana uwezo wa kutetea maslahi ya wananchi bungeni ilihali uwezo huo hawana au ni wa wabunge wawili watatu tu?
Kama kila mbunge ana uwezo na nafasi sawa ya kutetea maslahi ya jimbo lake na Watanzania kwa ujumla mbona mnawaona hawastahili kuwa wenyeviti wa kamati zilizopangwa na spika? Hoja dhaifu ya kitetezi inayotolewa eti suala la uzoefu na kamati kuwa muhimu. Je, Zitto Kabwe alipata wapi uzoefu? au Freeman Mbowe alizaliwa akiwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni? Je, alienda kufundishwa uzoefu mahali?
Kama alikwenda mahali kupata shule, kipi sasa hivi kinashindikana kuwapeleka wabunge wapya watakaochaguliwa kuongoza kamati hizo wakapigwe shule? Au ndio hawafundishiki? Sielewi. Inawezekana labda, nasema tena labda, kuna ajenda ya ziada juu ya uteuzi wa kamati lakini Chadema kama chama cha siasa makini ilipaswa kuwa na watu makini zaidi wakati wote na siyo kutegemea watu fulani fulani.
Mambo haya ndio yanayoleta umangimeza na ubwanyenye kwenye vyama, kwamba bila fulani kusema basi wengine hawasemi na fulani akisema basi ni alifa na omega, wote wanafuata kama kundi la nyumbu. Uongozi ndani ya Chadema Kunaendelea kujidhihirisha kuwa hakuna kuaminiana ndani ya chama hiki pamoja na chama kuwa na umri wa kijana mtu mzima (zaidi ya miaka 23).
Kumesikika kwenye vyombo vya habari kuwa Fredrick Sumaye pengine ndiye akapewa nafasi ya ukatibu mkuu. Hili nalo linapaswa kuingia kwenye historia ya siasa za dunia kwamba kuna chama nchini Tanzania kilimpa ukatibu mkuu mtu ambae si mwanachama. Wakati akihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) Sumaye hakuchukua kadi ya chama chochote ndani ya Ukawa. Sasa inakuwaje afikiriwe kupewa nafasi ya utendaji mkuu wa chama mtu ambaye haamini hata katika itikadi ya chama chenyewe?
Maana hana hata kadi. Tafsiri ya jaribio hili ni kwamba hakuna watu makini ndani ya Chadema ambao chama kama chama kimewaandaa ili wachukue nafasi za uongozi isipokuwa wanaviziavizia tu. Klabu ya mpira inayofanya usajili wa kuvizia lazima ifungwe tu maana hakuna namna nyingine. Kuendelea kutokuaminiana ndani ya Chadema kunaweza kuendelea kwa muda mrefu kama viongozi wakuu wa chama hawatotaka kuandaa watu wa kurithi madaraka yao kama ilivyo kwa CCM.
Kinachoonekana ni kwamba wanataka kutawala maisha yao yote. Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Anapatikana kupitia 0687281398.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment