Mawaziri wastaafu Basil Mramba (kushoto) na Daniel Yona wakiwa na zana za kufanyia usafi
katika Kituo cha Afya Sinza, Dar es Salaam jana ikiwa ni sehemu ya
kutumikia kifungo cha nje kwa kufanya kazi za kijamii.
MAWAZIRI wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona wameanza mchakato wa
kutumikia jamii kama sehemu ya kifungo chao cha nje baada ya jana
kukabidhiwa vifaa vya kufanyia usafi na kuoneshwa maeneo yatakayohusika
na usafi huo katika Hospitali ya Sinza, Dar es Salaam ikiwa ni
utekelezaji wa kifungo hicho.
Walibadilishiwa adhabu ya kifungo cha jela na kupewa adhabu ya
kutumikia kifungo cha nje mwishoni mwa wiki iliyopita na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukamilika mchakato wa kufikia hatua hiyo.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alisema Sheria ya
Huduma kwa Jamii Namba 6 Kifungu Namba 3(1) ya mwaka 2002, inasema mtu
yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni miaka mitatu
kushuka chini, Mahakama inaweza kumpa adhabu ya kutumikia jamii.
Mramba na Yona waliwasili katika eneo la hospitali saa 9:45 asubuhi
wakiwa wanatumia gari Toyota Fortuner lenye namba za usajili T222 DCL
huku Yona akiwa kiti cha mbele na Mramba akiwa kiti cha nyuma kushoto.
Baada ya kuwasili hapo, tayari kwa kuanza kutumikia adhabu yao ya
kifungo cha nje cha huduma kwa jamii, watu walianza kufurika katika eneo
hilo wakiwemo wagonjwa hospitalini hapo na wengine kutoka nje ambao
walikuwa wakiingia hapo licha ya walinzi kuwazuia bila mafanikio.
Hali hiyo ilipozidi ndipo polisi walipofika wakiwa katika gari lenye
namba za usajili PT 3946 na kuwatawanya watu hao na hali kutulia huku
mawaziri hao wa zamani wa Fedha na Nishati na Madini, wakienda kuripoti
katika ofisi za utawala tayari kwa kuanza kutumikia adhabu yao hiyo.
Yona akiwa mchangamfu kuliko mfungwa mwenzake Mramba walikabidhiwa
vifaa mbalimbali vya usafi zikiwemo fyekeo, fagio, majembe, buti, makoti
maalumu watakayokuwa wakivaa wakati wa usafi huo, vifaa vya kujikingia
vumbi na glovu. Walikabidhiwa na Ofisa Mazingira wa Hospitali ya
Palestina-Sinza, Miriam Mongi.
Baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, walitembezwa katika maeneo kadhaa
ambayo watatakiwa kufika kila siku na kufanya usafi kwa muda wa saa nne
kila siku hadi Novemba 5, mwaka huu ambapo adhabu yao hiyo itakoma. Yona
alivaa koti na kushika fyekeo na kujaribu kufyeka huku wanahabari
wakipiga picha na Mramba alivunja ukimya uliokuwa umemtawala na kutamka
kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Ofisa Huduma za Jamii wa Hospitali ya Palestina – Sinza, Deogratius
Shirima alisema wafungwa hao kabla ya kufika hapo walianzia Mahakama ya
Kinondoni ambako walipewa maelekezo ya namna ya kutumikia kifungo chao.
“Kabla ya kuja hapa Yona na Mramba walianzia Mahakama ya Kinondoni
ambako walipewa maelekezo ya namna kifungo chao kinavyotakiwa
kutekelezwa, walielezwa nini cha kufanya na nini wakifanya watarejeshwa
ndani na baadaye wakaja hapa kuoneshwa na kukabidhiwa vifaa vya kazi,”
alisema Shirima.
Baada ya kumaliza taratibu zote za makabidhiano ya vifaa na kuoneshwa
maeneo ya kutumikia adhabu yao hiyo, wafungwa hao waliondoka
hospitalini hapo kwa kutumia gari lao likiongozwa na gari la Polisi saa
5:19 asubuhi.
Leo Mramba na Yona wanataraji kuanza rasmi kutumikia adhabu yao hiyo
kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana kila siku, isipokuwa
Jumamosi na Jumapili. Aidha, Shirima alisema hukumu hiyo imewavuta watu
wengi kwa kuwa tu Yona na Mramba walikuwa ni viongozi na ni watu wenye
majina makubwa katika jamii, lakini adhabu kama hiyo inatumikiwa na
wananchi wa kawaida zaidi ya 1,000 jijini Dar es Salaam kila siku.
Julai 6, 2015, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu kwenda
jela miaka mitatu na kulipa faini ya Sh milioni tano, Mramba na Yona
huku ikimuachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray
Mgonja baada ya kumuona hakuwa na hatia.
Viongozi hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya
madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 kutokana na
kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni iliyopata zabuni ya ukaguzi wa madini
ya dhahabu nchini ya M/S Alex Stewart.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa na Hakimu Mkazi Mahakama ya Kisutu, Dar
es Salaam, Sam Rumanyika ilimtia hatiani Mramba katika mashitaka 11 na
Yona mashitaka matano.
Chanzo HabariLeo.
Monday, 8 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment