Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetoa taarifa ya maendeleo ya msako
unaofanywa dhidi ya majangili, waliomuua rubani wa ndege iliyokuwa
ikifanya doria katika Pori la Akiba mkoani Simiyu na kusema umefikia
hatua muhimu na hivi karibuni wahusika watakamatwa.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gaudence Milanzi alitoa taarifa hiyo jana
kwa waandishi wa habari mjini hapa, akisisitiza kwamba Serikali
itashinda vita dhidi ya ujangiri hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.
Pamoja na taarifa hiyo, Katibu Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya maswali
mbalimbali yaliyojitokeza baada ya tukio hilo, ikiwemo madai kwamba
kulikuwa na mizoga mingi ya tembo katika hifadhi hiyo na walichelewa
kutoa msaada.
“Msako umefikia hatua muhimu na kasi iliyooneshwa, hivi karibuni
wahusika wote watakamatwa,” alisema na kupongeza watumishi wanaohusika
na msako kwamba wamefanya kazi usiku na mchana bila kujali mazingira
magumu, ikiwemo mvua.
Akisisitiza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kwamba msako
ufanyike na wahusika wakamatwe mapema iwezekanavyo, alisema kazi hiyo
imefanywa na wizara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama.
Alisema yeye pia aliagizwa na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Jumanne
Maghembe afanye ziara kufuatilia maendeleo ya msako, jambo ambalo
alitekeleza na kuikamilisha juzi.
Aliendelea kusema, “ziara nimeikamilisha juzi jioni...nimefarijika
msako wa wahalifu unaendelea vizuri kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo
ya Ndani na vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa (Simiyu) na kitaifa.”
Akizungumzia muda ambao msaada ulipatikana baada ya ndege kuanguka,
alisema juhudi zilichukuliwa kuhakikisha msaada unapatikana kwa kutumia
doria nyingine kwenye eneo la tukio ndani ya saa mbili.
Alisema kutokana na eneo hilo la Pori la Akiba la Maswa na Ranchi ya
Wanyamapori ya Mwiba kuwa na mito, wengine waliokwenda kutoa msaada
iliwabidi waogelee.
Upande wa madaktari ambao alisema walitoka Arusha na wengine Nairobi, Kenya, Katibu Mkuu alisema walifika baada ya saa tano.
Kuhusu hatma ya mabaki ya ndege katika eneo hilo, mtendaji huyo wa
Wizara alisema yatachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika. Alisema
yamefunikwa na yako chini ya ulinzi, kuepusha ushahidi kuingiliwa.
Akifafanua idadi ya mizoga ambayo ndege hiyo ilishuhudia kabla ya
kuanguka, alisema ulikuwa moja tofauti na madai kwamba ilikuwapo mizoga
mingi. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, rubani aliyepoteza maisha, aliajiriwa
na Kampuni ya Mwiba Holdings ambao wamemilikishwa kitalu cha kupiga
picha za utalii.
Alisema kampuni hiyo, pia ina jukumu la kufanya ulinzi na kuhifadhi.
“Hilo ni jukumu la kawaida kwa kampuni zinazomilikishwa vitalu...mara
nyingi huwa wanafanya joint patrols (doria ya pamoja) pamoja na askari
wetu,” alifafanua.
Alisema mwili wa rubani huyo ulitarajiwa kusafirishwa jana usiku
kwenda kwao Uingereza. Serikali imetoa pole kupitia ubalozi wa nchi
hiyo.
Chanzo Gazeti leo.
Thursday, 4 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment