Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Ramadhan Mwinyi
SERIKALI imesema itaendelea kuhakikisha wanafunzi wanaosoma nje
wanakuwa katika mazingira salama, na tayari watu watano waliohusika na
tukio la kushambuliwa kwa wanafunzi wanne wanaosoma India wanashikiliwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Ramadhan Mwinyi aliyasema hayo
jana Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi wa tukio lililotokea
Bangalore India.
“Tulipata taarifa kuwa wananchi wetu ambao ni wanafunzi wa Bangalore
India walishambuliwa baada ya raia wa Sudan kumgonga raia wa India kwa
gari na kisha kufariki dunia, ambapo kuanzia hapo palitokea mtafaruku wa
kushambulia watu wenye asili ya Afrika waliokuwepo maeneo hayo,”
alieleza Balozi Mwinyi.
Alisema baada ya tukio hilo wanafunzi hao wa Kitanzania wakitokea
chuo walisimama maeneo hayo ili kujionea ni nini kimetokea lakini wao
pia walichanganywa na kuanza kushambuliwa na raia hao wa India kwa kuwa
walikuwa hawatofautishi watu, bali walikuwa wakishambulia raia wote
wenye asili ya Kiafrika.
“Katika tukio hilo raia wetu wanne walishambuliwa vibaya na baadaye
walipelekwa hospitali na kupatiwa matibabu. Kufuatia hilo balozi wetu
nchini humo amefuatilia hili na ameandika barua ya kibalozi kutaka
Serikali ya India kueleza ni kitu gani kimetokea na kueleza jinsi gani
wanawalinda raia wetu,” alieleza.
Aidha, alisema jana Balozi wa Tanzania nchini humo amefanya ziara ya
kutembelea jimbo hilo na atazungumza na raia ili kuhakikisha usalama wao
unalindwa.
Pia alisema jana alimuita Balozi wa India nchini na kufanya naye
mazungumzo na alimhakikisha kwamba tayari hatua zimeshachukuliwa na
tamko limeshatolewa la kilichotokea Bangalore na wameahidi kwamba
watahakikisha wahusika wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Alisema katika hatua za awali tayari watu watano wameshakamatwa na
ulinzi wa wanafunzi umeimarishwa na kuahidi wataimarisha usalama zaidi
ili wananchi walio nje waishi kwa usalama na mabaya zaidi yasijitokeze.
Aidha, Balozi Mwinyi alisema kuna tukio lingine limetokea juzi jioni
la mwanafunzi Mtanzania Christian Benjamin Mutandisi aliyekuwa akisoma
Chuo cha Koshys ambaye alipata ajali ya pikipiki na kufariki dunia papo
hapo na kubainisha kwamba baada ya uchunguzi wamegundua kwamba ajali
hiyo haihusiani na tukio la Bangalore.
“Tumegundua kwamba mwanafunzi huyo hakuvaa kofia ngumu, tumepata
taarifa kwamba Jumuiya ya Watanzania inaendelea na taratibu za mazishi.
Hivyo tukio hili halihusiani kabisa na lile la Bangalore,” alisema.
Pia Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda
na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga alilitolea taarifa tukio hilo jana
bungeni mjini Dodoma kutokana na Mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 47
uliotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).
Zitto alisema pamoja na kauli hiyo, Serikali ya India iombe radhi kwa
Serikali ya Tanzania kwa kushindwa kuwalinda wanafunzi hao wanaosoma
nchini mwao kwa kufuata taratibu na sheria.
Chanzo Gazeti Leo.
Thursday, 4 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment