SERIKALI imeshauriwa kuweka mfumo utakaowezesha wanafunzi kupata
vifaa vya kujisitiri wakiwa kwenye hedhi kuepusha kile kilichoelezwa
kuwa watoto wengi wa kike kushindwa kuhudhuria masomo wakati wote
kutokana na kukosa vifaa husika.
Miongoni mwa wabunge walioshauri juu ya hilo, wametaka pia shule zote
za serikali ziwezeshwe kuwa na huduma ya maji ambayo pia ni muhimu
zaidi kwa watoto wa kike wanapokuwa katika hali hiyo ya kibaiolojia.
Walitoa ushauri huo juzi bungeni wakati wakichangia Mwongozo wa
Mpango wa Maendeleo ya Taifa uliowasilishwa bungeni Jumatatu na
kujadiliwa mfululizo na wabunge wiki hii.
Mbunge wa Viti Maalumu, Zaynab Vullu ambaye alishauri mpango wa elimu
bure uendane na kumjengea mwalimu mazingira bora, alisema pia watoto
wanahitaji mazingira mazuri ya kujifunzia ikiwemo kuwapatia taulo
maalumu za kike.
“Tuangalie mazingira ya mtoto wa kike tangu chekechea. Maji ni
msingi. Tunahitaji uvunaji wa maji shuleni, mahitaji ya maji kwa mtoto
wa kike ni makubwa zaidi na pia wawekewe utaratibu wa kupewa mataulo ya
kike,” alisema.
Mbunge wa Njombe Mjini, Edward Mwalongo (CCM) alisema tatizo la
ukosefu wa vifaa vya watoto kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi ni kubwa
na linalohitaji kufanyiwa kazi.
Mbunge wa Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka (CCM) alisema, “mpango huu
uliowasilishwa ni mzuri kazi yetu ni kujazia ili waziri
atakapouwasilisha kipindi kijacho, uwe umekamilika.”
Chanzo Gazeti leo.
Thursday, 4 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment