Askari nane wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kigona wakituhumiwa kwa mauaji ya Erick Nilamewa (16) waliyemtuhumu kuwaibia simu moja aina ya Techno na Sh. 6,000.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni Mtaa wa Mabatini Mwanga Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Wanajeshi
hao wakiwa nane, walionekana wakimpiga Nilamewa kwa mateke, fimbo na
kumchoma na pasi tumboni, kifuani na mgongoni, baada ya kumkamata
wakimtuhumu kwa wizi huo.
Mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni.
Aidha,
Ahamad Mussa, mkazi wa Mabatini eneo la Mwanga Manispaa ya
Kigoma/Ujiji, amelazwa wodi namba 7 katika hospitali ya Mkoa Maweni kwa
matibabu, kutokana na purukushani hiyo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kigoma Ferdinard Mtui, alithibitisha kukamatwa kwa
askari hao nane wa JWTZ kwa tuhuma za mauaji ya kijana huyo na
kumjeruhi Mussa (16).
Mtui alisema “Ni
kweli tunawashikilia wanajeshi nane na tunaendelea na upelelezi, na
baada ya uchunguzi tutawapeleka mahakamani ili sheria iweze kuchukua
mkondo wake.”
Akizungumza
kutoka kitandani alikolazwa, Mussa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha
kwanza katika Shule ya Sekondari Kitwe, alitumiwa ujumbe wa simu na
wanajeshi hao akiwa shuleni ambao walisema kwamba wanamhitaji.
“Baada
ya kutumiwa ujumbe huo mimi nilimbipu, akanipigia na kujitambulisha
kuwa yeye ni afande Aberi, akasema njoo mara moja nakuhitaji," alisema Mussa.
"Kwa
sababu tunakaa mtaa mmoja, pia huwa naingiaga kwenye makazi yao
wanaponituma vitu mbalimbali kama sigara, sikuwa na wasiwasi wowote
kuhusu wito huo.”
Alisema
alipofika alibisha hodi na walimwitikia na kumwambia akae uani ndipo
baada ya muda alitoka Aberi akiwa amevaa kaptura ambaye alianza kuita
wenzake ambao walianza kumsulubu.
“Nilimsikia
akiwaita wenzake wakina afande Mayowa, Ally na wengine nimesahau majina
yao lakini jumla walikuwa wanajeshi nane ambao walikuwa wakinipiga.
"Waliniambia
ninyooshe miguu yangu juu ya ukuta na niliponyoosha walinipiga na ubao
na fimbo ya mianzi kichwani… damu zilianza kutoka.
"Wakachukua
maji wakasafisha, wakapiga tena kichwa nikaanguka chini kisha
wakanipiga mateke na kunichapa na nyaya za umeme huku wakiuliza ilipo
simu na Sh 6,000 nilizoiba,” alisema Mussa.
Alisema
wakati hali ikizidi kuwa mbaya, "walichukua chupa ya pombe na
kunimiminia" kabla ya kujitokeza mwanamke mmoja wa nyumba ya jirani
anayefahamika kwa jina la mama Hoza ambaye aliwaambia wamwache "mtoto wa
watu maana watamuua bure.
“Mimi sijaiba simu wala siku ya leo (jana) sijafika kambini hapo.
"Sijaiba
wao wakaendelea kunipiga na kunimwagia maji na kunigalagaza kwenye
mchanga wakati huo damu zinaendelea kuvuja kichwani, ndipo mimi
nikawambia naomba niende nyumbani nikamwambie mama yangu na tulienda na
mwanajeshi mmoja na tulipofika nyumbani tulimkuta mama yangu.
"Mwanajeshi
huyo akasimama nje mimi nikaingia ndani nikapita uani na kukimbia na
ndiyo ikawa pona yangu la sivyo na mimi ningefariki dunia.”
Alisema
baada ya yeye kukimbilia ndipo walipomkamata Erick mtaani na kumpeleka
kwenye makazi yao ambako walimpiga na kumtesa hadi walipoona hali yake
kuwa mbaya, walikwenda polisi kuchukua fomu namba 3 (PF3)kwa ajili ya
kumpeleka hospitali ya Maweni kwa matibabu, lakini alifariki dunia.
Mama
mzazi wa majeruhi huyo, Mwaisala Ahamad (36) alisema wanajeshi
walimuagiza mtoto mmoja kwenda nyumbani kwake kwamba wanamuitaji mtoto
wake na aliwaambia kuwa ameende shuleni.
“Waliniomba namba ya simu ya mtoto wangu nikawapatia kwasabababu wanajeshi hawa walikuwa na mazoea na mwanangu," alisema Mwaisala.
"Nilipowapa nilienda kwenye shughuli zangu kama kawaida sikuwa na wasiwasi wowote, hawa tunawajua.
"Wengine
wana nyota moja (luteni nusu) na wengine mbili (luteni) na wengine tatu
(kepteni) na kutokana na vyeo walivyokuwa navyo sikutarajia mtoto wangu
yamkute yaliyomkuta.”
Aliongeza
kuwa kama askari hao walihisi kuwa mtoto wake ndiye aliyeiba simu yao
walipaswa kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi.
Kwa
upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mshumbusi Edmond
alithibitisha kumpokea marehemu Nilamewa akiwa na majerahe kifuani,
tumboni na mgongo lakini akafariki muda mfupi baada ya kufikishwa
hospitalini hapo.
Mwili wake uko chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni, alisema.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment