Na Raymond Mushumbusi- MAELEZO
Serikali
kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya takribani Sh.
billioni 12 kutoka kwa wafanyabiashara ambao walikwepa kodi na kupewa
muda wa siku 14 na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli kulipa kodi hizo kwenye mamlaka hiyo.
Akitoa takwimu hizo jana mara baada ya kuapishwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata alisema,
kila Mtanzania ana jukumu la kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na sio
kukwepa na amehaidi kulisimamia vizuri suala la ukusanyaji wa mapato
katika sehemu mbalimbali ili kuongeza mapato ambayo yatasaidia
kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali.
“Tutajitahidi
kwa kila namna kuwaelimisha wananchi wetu ili wafahamu wajibu wao na
umuhimu katika kulipa kodi na sio kukwepa kulipa kodi na tunawaomba
wananchi kila waendapo kupata huduma yoyote ile iwe katika sekta binafsi
au Serikalini basi anatakiwa aombe stakabadhi za manunuzi au huduma ili
tuweze kudhibiti upotevu wa kodi” alisema Kidata.
Kamishna Kidata aliongeza kwamba
mamlaka hiyo ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kama kuna suala
lolote au tatizo kuhusu kodi kuna ofisi katika mikoa yote ikiwa ni hatua
ya kutatua shida zao na kama kuna mtumishi yoyote wa mamlaka hiyo
atashindwa kumuhudumia mwanachi inavyotakiwa basi taarifa zitolewa mara
moja kupitia namba zao zilizoko kwenye tovuti ya mamlaka hiyo, ambayo ni
www.tra.go.tz ili kuimarisha huduma zetu kwa wateja.
Aidha Kamishna Mkuu huyo alisema
kuwa watawachukulia hatua wale wote ambao hawatalipa au hawajalipa kodi
zao kwa kuwapeleka mahakamani kwa kukaidi kulipa kodi halali kwa mujibu
wa Sheria.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria na ina
mamlaka ya usimamizi wa makusanyo ya Mapato Tanzania na kwa kipindi cha
hivi karibuni kumekuwa na ukwepaji wa kodi uliotokana na sakata la
upotevu wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam hivyo kuikosesha
mapato Serikali lakini jitihada thabiti zimefanywa na mamlaka hiyo
kukusanya madeni kutoka kwa wakwepa kodi na kuwafikisha mahakamani ambao
wamekaidi kulipa.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment