Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
OFISA Mifugo wa Kata ya Kakunyu wilayani Misenyi mkoani Kagera, Eric
Kagoro amenusurika kutumbuliwa jipu kwenye mkutano wa hadhara baada ya
kuhusishwa na sakata la kuruhusu ng’ombe 291 kulisha kwenye Ranchi ya
Mifugo ya Misenyi.
Tukio hilo ni la jana wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza
na mamia ya wananchi waishio jirani na ranchi hiyo katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye makao makuu ya ranchi hiyo.
Waziri Mkuu alimuibua Kagoro katikati ya mkutano kwa kumtaja jina na
tuhuma zinazomhusu kuhusu mifugo iliyokamatwa. “Ofisa Mifugo wa kata
yupo hapa?,” alihoji Waziri Mkuu na kuendelea kumhoji, “Wewe ndiyo
Eric?”
Alipojibu Ndiyo, Majaliwa alimuuliza tena, “Nimekujuaje?” “Nimeambiwa
wale ng’ombe waliokamatwa ni wa rafiki yako na wewe ndiye ulitoa kibali
waje kulishwa kwenye ranchi hii. Siyo kazi yako kuruhusu mifugo ya nje
ije kulishwa hapa kwenye ranchi.
Kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote kuingiza mifugo kwenye ranchi
ili ipate malisho, “ alisema. “Leo nimekusamehe. Kazi yako ni
kuhakikisha mifugo ya kwenye kata hiiiko salama. Kazi yako ni kuwasaidia
wafugaji wa kata hii wafuge vizuri na uhakikishe mifugo yao inakuwa na
tija,” alisema Waziri Mkuu hukuakishangiliwa na wananchi.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa
watendaji wa kata na vijiji kutotumia nafasi zao kuleta migogoro baina
ya watu wa nje na wananchi wanaowaongoza. “Mwenyekiti wa kijiji huna
ruhusa ya kugawa kitalu cha ranchi au kuruhusu mtu yeyote akalime ndani
ya ranchi”, alisema.
Aliwataka pia maofisa uhamiaji wawe makini na vyeti vya kuandikisha
uraia wanavyovitoa kwa wananchi wanaoishi mipakani kwa kile alichosema,
imekuwa ni mianya ya kuleta migogoro ya ardhi. “Watu wa uhamiaji kuweni
makini na CN mnazotoa (CN=Certificate of Naturalisation). Wote wanaoomba
CN wanataka blocks (vitalu) tu.”
Alitoa agizo kuwa watafutwe watu wote walioingia nchini kwa mgongo wa
CN, wakamatwe na kurejeshwa makwao. “Kuna watu wamekuja hapa nchini
wakaomba CN lakini wakikaa wanaleta wenzao waje kununua ardhi kwa
kutumia mgongo wa CN zao.”
Alisema watu wametoka Wilaya ya Karagwe ambako pia kuna tatizo kama
la Misenyi na kuwataka wahusika wajiandae kuchujwa na kuchukuliwa ardhi
zao kama watakuwa hawajaziendeleza ili wapewe Watanzania wenye uhitaji
wa kulima na kufuga.
Chanzo Habarileo.
Monday, 14 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment