WATENDAJI wa Mahakama wametakiwa kuonesha tofauti ya hukumu zao na zenye utata kama iliyotolewa na Pilato kwa Yesu Kristo.
Paroko wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Bikira Maria Mpalizwa
Mbinguni, Jimbo la Tunduru Masasi, Dominick Mkapa, alisema hayo juzi
mjini hapa, wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika kanisa
hilo.
Kwa mujibu wa Paroko huyo, hukumu ya kifo iliyotolewa na Pilato
wakati huo, ilijaa utata na uongo, mazingira yaliyosababisha Yesu
Kristo, auawe kwa makosa ambayo hakutenda.
Alisema kushindwa kwa Pilato kusimama katika haki, woga pamoja na
shinikizo kutoka kwa Wayahudi, ni baadhi ya sababu zilizofanya Yesu
Kristo ahukumiwe, asulubiwe msalabani na hatimaye kifo na kuongeza kuwa
sababu kama hizo hutumika hata sasa katika baadhi ya hukumu.
Paroko Mkapa alisema hata makosa aliyoshitakiwa Yesu, hayakuwa na
ukweli wowote na alionesha wazi kusikitishwa na uamuzi wa Pilato wa
kutoa hukumu kubwa kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa Wayahudi.
“Nitoe mwito katika Ibada hii ya Ijumaa Kuu kwa mahakama nchini,
zitoe adhabu katika misingi ya haki na usawa na bila shinikizo kutoka
kwa mtu yeyote, ili kuepuka kutoa hukumu zenye utata na uonevu kama
aliyopewa Bwana Yesu Kristo. “Hukumu iliyotolewa na Pilato wakati wa
utawala wa Warumi chini ya Mfalme Kaiseri…haina tofauti na baadhi ya
hukumu zinazotolewa hivi sasa katika baadhi ya mahakama nchini, hivyo ni
vyema wanaokutwa na makosa wakatendewa haki,” alisema Mkapa.
Paroko Mkapa alisema mateso ya Yesu Kristo na kifo chake ni fundisho
kwa Watanzania ambapo wanapaswa kuishi kwa amani na upendo kama
inavyompendeza Mungu. Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Rais mstaafu wa
Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye yuko mjini Masasi kwa mapumziko ya
Sikukuu ya Pasaka.
Saturday, 26 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment