Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
SERIKALI imetoa tamko kuwa kwa sasa haina mpango wa kuteketeza meno
ya tembo yaliyohifadhiwa ambayo yametokana na vitendo vya ujangili na
vifo asilia vya tembo.
Tamko hilo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Profesa Jumanne Maghembe alipokuwa anazungumza na Balozi wa Marekani
nchini, Mark Childress.
Balozi huyo alimtembelea waziri Maghembe ofisini kwake kujadili maendeleo ya Sekta ya Maliasili nchini.
Akiwa hapo, alipendekeza Tanzania ichome sehemu meno ya tembo
yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe mzito duniani juu ya dhamira ya
Serikali kukomesha biashara hiyo haramu.
Hata hivyo, katika majibu yake, Profesa Maghembe alisema; “Naomba
niweke wazi kuwa kwa sasa hatupo tayari kuteketeza meno haya. Tunaweza
kuyatumia kwenye tafiti za kisayansi au vielelezo kwa ajili ya kesi za
ujangili ambazo zipo mahakamani na nyingine ambazo bado zinafanyiwa
uchunguzi.”
Hatua hiyo imekuja huku nchi jirani za Kenya na Malawi zimeteketeza
meno yake ya tembo yaliyohifadhiwa ikielezwa kufanya hivyo ni njia
mojawapo ya kuishawishi dunia juu ya umuhimu wa kukomesha biashara
haramu ya meno ya tembo. Nchi nyingine zilizofanya hivyo ni Chad,
Ubelgiji, Ufaransa, China, India, Marekani na Ureno.
Kwa upande wa nchi ambazo zina msimamo sawa na Tanzania katika
kuendelea kuhifadhi meno ya tembo ni pamoja na Afrika ya Kusini,
Botswana na Zimbabwe.
Akizungumzia kuendeleza sekta ya Maliasili nchini, Profesa Maghembe
amemuomba Balozi Childress kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
kukuza sekta hiyo kwa kuleta wawekezaji kutoka Marekani, lakini pia
kusaidia katika mapambano dhidi ya ujangili.
Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji
mkubwa ikiwemo hoteli za kitalii, fukwe za kisasa na kuendeleza vivutio
mbalimbali vilivyomo hapa nchini.
Pia alimshukuru balozi huyo kwa misaada mbalimbali kutoka Serikali ya
Marekani ya kuendeleza sekta ya Maliasili nchini ukiwemo wa hivi
karibuni wa mbwa maalumu wa kusaidia utambuzi wa rasilimali za maliasili
zinazoweza kutoroshwa nje ya nchi kupitia bandari na viwanja vya ndege.
Chanzo habariLeo.
Saturday, 26 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment