KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Dk Primus Nkwera, amejiuzulu nafasi hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali. Uamuzi wa kujiuzulu kwa Dk Nkwera, ulitangazwa juzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo, Steven Mlote wakati akizungumza na wafanyakazi wa baraza hilo kwenye kikao cha dharura.
Mlote alisema, Dk Nkwera amefikia uamuzi wa kujiuzulu, ili kulinda hadhi ya baraza hilo, baada ya gazeti moja la kila wiki kuchapisha habari zikimtuhumu kwa mambo mbalimbali, ikiwemo madai ya kughushi vyeti.
Alisema kwa mujibu wa Dk Nkwera nafasi kubwa kama hiyo katika taasisi ya elimu, haipaswi kushikwa na mtu mwenye tuhuma ya aina yoyote, hivyo baada ya kutafakari ameona ajiweke pembeni na uongozi wa baraza hilo, ili uchunguzi ufanyike akiwa pembeni.
“Tumetumia muda mrefu kutafakari hoja za Dk Nkwera na tumekubali kujiuzulu kwake kwa shingo upande,” alisema Mlote akiwaambia wafanyakazi waliokuwa katika kikao hicho. Mlote alisema kazi iliyofanywa na Dk Nkwera akiwa kiongozi wa baraza hilo inafahamika kwa kila mmoja na uamuzi wake huo ni majonzi kwa baraza hilo.
“Najua mmepata mshituko mkubwa, lakini Dk Nkwera hajafa. Yuko hai, na huyu bado ni mtumishi wa Serikali. Alichofanya ni kuamua kuachana na ukatibu mtendaji. Tutaendelea kumtumia itakapobidi kwa ushauri.
“Wakati mwingine ni lazima mkubaliane na hali hii, lakini endeleeni kuchapa kazi kwa ufanisi kama kawaida, kana kwamba bado mko na Dk Nkwera,” alisema Mlote. Kutokana na kujiuzulu kwa Dk Nkwera, Mlote alieleza kuwa Bodi imemteua Mkurugenzi wa Mitaala wa baraza hilo, Dk Adolf Rutayunga kukaimu nafasi hiyo wakati taratibu nyingine zikiendelea.
Akizungumza katika kikao hicho, Dk Rutayunga alisema kuwa viatu ambavyo ameiacha Dk Nkwera ni vikubwa kwake lakini atajitahidi kuhakikisha anaendeleza yale yote ambayo ameyaacha.
“Jambo hili ni kubwa, uamuzi huu wa kujiuzulu kwa Dk Nkwera ni mzito, lakini hatuna cha kufanya. Tutashikamana kuhakikisha kwamba kazi za Baraza zinasonga mbele kwa weledi uleule” alisema.
Mlote alipotafutwa na mwandishi wetu alikiri Dk Nkwera kujiuzulu bila kueleza kwa undani sababu za kujiuzulu kwake. “Ni kweli amejiuzulu nafasi yake, lakini siwezi kukupa maelezo yote kwa sababu niko barabarani naendesha gari,” alisema Mlote.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment