Mgahawa aliotumia Rais John Magufuli kupata mlo wa mchana na msafara
wake juzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza, umekuwa kivutio kwa wateja
wengi wakinunua chakula na kutaka kukalia kiti na meza alivyotumia
kiongozi huyo.
Meneja wa mghahawa huo wa Victoria, Elizabeth
Maneno (pichani) alisema jana kwamba hali hiyo ilijitokeza mara baada ya
Rais kuondoka hapo.
“Hata leo tumepokea wateja wengi
kulinganisha na siku nyingine, baadhi yao wanaagiza chakula kwa sharti
la kutaka kukikalia kiti na meza aliyotumia Rais Magufuli,” alisema
Elizabeth.
Akizungumzia hali ilivyokuwa juzi kabla na wakati wa
ugeni huo meneja huyo alisema: “Ilikuwa ni hofu na woga uliochanganyika
na furaha kumwona Rais akiingia kwenye mgahawa wetu wa chai ya rangi ya
Sh200 na ya maziwa Sh300.
“Mshtuko wetu uligeuka furaha baada ya
kubaini kuwa oda ya sahani 28 za kubeba (takeaway), tulizoagizwa mapema
asubuhi bila kuelezwa zinakoenda zilikuwa za ujumbe wa Rais,” alisema na kuongeza:
“Kabla
Rais Magufuli hajaingia kwenye mgahawa wetu, alikuja mtu mmoja
tusiyemfahamu na kuagiza sahani 28 za chakula kwa gharama ya Sh5,000
kila moja,”
Alisema baada ya kumtaarifu mteja wake kuwa chakula
kiko tayari, alielekezwa kuandaa meza na viti kwa sababu wageni wake (wa
mteja), sasa wameamua kula palepale mgahawani.
“Ghafla
tulimwona Rais anaingia ndani ya mghahawa wetu; kwanza tulishikwa hofu,
woga na kihoro tusijue tufanye nini hadi tulipogutushwa na aliyetoa oda
kwa kutuagiza tugawe chakula alichoagiza,” alisema meneja huyo; “hapo
ndipo tulipobaini kumbe chakula kile kilikuwa cha ugeni wa Rais.”
Pamoja na chai
ya rangi na ya maziwa, mghahawa huo pia unauza vyakula vya aina
mbalimbali kwa bei kati ya Sh1,500 hadi Sh5,000 kwa vyakula vya kubeba,
huku soda ikiuzwa kwa Sh500 kwa chupa.
Credit Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment