Askofu Msaidizi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa.
WAKATI Rais John Magufuli, Baraza la Mawaziri na viongozi wengine
wakiombewa ili kufanya kazi vizuri katika ibada ya Ijumaa Kuu
iliyofanyika jana, viongozi mbalimbali wamekumbushwa kutimiza wajibu wao
wa kuwatumikia wananchi kwa haki bila kushinikizwa.
Akihubiri katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maxmillian
Maria Kolbe, Mwenge jijini Dar es Salaam, Askofu Msaidizi, Jimbo Kuu la
Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, alisema ni vyema viongozi katika jamii
wakumbuke wamepewa dhamana ya kuangalia wengine na kuongoza kwa haki na
kuacha tabia ya ubinafsi na maamuzi ya kushinikizwa.
“Sisi tuliopewa dhamana tuamue kwa haki na kamwe tusiamue kwa
shinikizo, kwa sababu ni heri kufa shahidi kuliko kuangamiza damu za
watu wasio na hatia,” alisema Askofu Nzigilwa katika Ibada ya Ijumaa Kuu
iliyofanyika kitaifa kanisani hapo.
Aliwataka waumini kutumia Ibada ya Ijumaa Kuu kuwa kiele- lezo cha
upendo kwa wengine na kamwe usaliti usiwepo kwa kuwa ni jambo baya lin-
aloleta uharibifu. Alisema usaliti uliofanywa na Yuda Iskariote wa
kumbusu Yesu Kristo, ni jambo gumu linalotakiwa kuepukwa na wanadamu kwa
sababu ni sumu inayoua.
“Matendo ya unafiki na usaliti ni mabaya, kwa sababu mtu au watu
wanaofanya huyafanya dhidi ya wengine huku mkichekeana, lakini kwa ndani
unamuua, tafadhali tusiwe na sura mbili, kama ni ndiyo iwe ndiyo na sio
iwe sio,” alisema Askofu Nzigilwa.
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es
Salaam, Dk Valentino Mokiwa, amewataka Watanzania hasa waumini wa dini
ya Kikristo kuachana na dhambi na kuishi katika uadilifu unaompendeza
Mungu.
Akizungumza baada ya misa ya Ijumaa Kuu katika Kanisa Kuu la
Mtakatifu Albano, Askofu Mokiwa alisema, kuna kila haja ya watu
kubadilika na kuachana na maisha ya dhambi kwa kuwa hayampendezi Mungu.
Naye Padre Nicholaus Masamba wa katika Kanisa Kuu Katoliki la
Mtakatifu Joseph, aliwataka Watanzania kutekeleza wajibu wao katika
mambo mbalimbali ili kuhakikisha familia zinakua na maadili mazuri.
“Wazazi wanatakiwa kuhakikisha watoto wanalelewa katika malezi bora
ili kuendana na tafakari ya Yesu iliyosema yametia wakati anakata roho
baada ya kutimiza wajibu wake,” alisema.
Katika Kanisa la Kiinjili la Kiletheri Tanzania (KKKT) Usharika wa
Azania Front, Mchungaji wa kanisa hilo, Charles Mzinga, aliwataka
Wakristo kumtegemea Mungu katika kila jambo wanalopitia na kulifanya kwa
kuwa ndio nguzo muhimu katika maisha ya binadamu.
Alisema ibada hiyo inawakumbusha mateso na kifo cha Yesu hivyo kila mmoja anapaswa kumpokea na kumtegea katika maisha yake.
Magufuli aombewa
Katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kipawa Kigango cha Stakishari,
Mlezi na Mhadhiri wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea,
Padre Peter Msafiri, aliwataka Wakristo kuombea Serikali inayoongozwa na
Rais Magufuli.
Aliwataka pia kuwaombea mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wote wa
vitengo serikalini, ili Mungu awaongeze kwenye utendaji kazi wao.
Wakati katika Kigango cha Stakishari wakifanya sala maalumu ya
kumuombea Rais Magufuli na Serikali yake, Rais Magufuli pamoja na mke
wake, Janeth Magufuli, walishiriki ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la
Mtakatifu Petro, jijini Dar es Salaam.
Katika ibada hiyo, mbali na Rais Magufuli na mke wake, viongozi
wengine waliohudhuria ni pamoja na mke wa Waziri Mkuu, mawaziri na
wabunge.
Mkoani Morogoro, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro,
Telesphor Mkude juzi katika ibada ya Alhamisi Kuu, aliwaasa waumini
kuonesha dhamira ya kujishusha na kuhudumia wadogo.
Mkude alisema Yesu Kristu anataka unyenyekevu huo katika jumuiya,
katika familia na jamii nzima kwa ujumla ambapo alisema kuwa wanapaswa
kutoa sadaka ya kuhudumiana.
Uchaguzi Zanzibar
Nako huko Dodoma Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri
Tanzania Dayosisi ya Dodoma, Mchungaji Samwel Mshana ameshauri vyama
ambavyo havikushiriki uchaguzi wa Zanzibar kuingizwa katika serikali ya
Umoja wa Kitaifa, kwani nao wana nafasi kubwa ya kujenga uchumi amani na
ustawi wa Zanzibar.
Katika mahubiri yake pia aliwakumbusha waumini kuiona Pasaka hiyo
kama sehemu ya kujihoji kwenye matendo wanayoyafanya kama kuna mahusiano
yoyote na Mungu badala ya kuichukulia kuwa ni sikukuu kama zingine.
Naye Askofu mstaafu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora,
Francis Ntiruka alishauri serikali ya Unguja kuachana na siasa na badala
yake iwatumikie wananchi. Askofu huyo aidha amemtaka Rais wa Zanzibar
kujali na kuwatimizia mahitaji wananchi wote kama alivyoahidi bila
kujali kama kuna vyama ambavyo vilisusia uchaguzi huo.
Aidha amewataka Wakristo kuhakikisha wanaitumia Pasaka kwa kutenda
mema na kuonesha upendo kwa vitendo huku wakijiepusha matendo yasiyofaa
kama vile ulevi uasherati wizi ikiwemo na matumizi ya madawa ya kulevya.
Imeandikwa na Ikunda Erick, Regina Kumba, Theopista Nsanzugwanko na
Katuma Masamba Dar, Agnes Haule, Morogoro na Sifa Lubasi, Dodoma.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 26 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment