Rais Magufuli pamoja na wajumbe wa serikari zote mbili wakishuhudia uwekwaji saini wa mkataba kuhuusu ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika nyanja za uchumi, biashara, uwekezaji, ufundi, vijana na
michezo. Kwa upande wa Tanzania mkataba ulisainiwa na Waziri wa Mambo
ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
MFALME wa Saudi Arabia, Salman Bin Abdulaziz Al Saud amemhakikishia
Rais John Magufuli, kuwa nchi yake imeichagua Tanzania kuwa nchi ya
kipaumbele katika mpango wake wa kuimarisha zaidi mahusiano na Afrika
uliolenga kuendeleza na kukuza biashara, uwekezaji na kushiriki katika
miradi ya maendeleo.
Ujumbe wa Mfalme Salman uliwasilishwa kwa Rais Magufuli jana na
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel Al Jubeir Ikulu jijini Dar
es Salaam. Katika salamu hizo pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa
kuchaguliwa kuiongoza Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania, Mfalme
Salman Bin Abdulaziz Al Saud amesema Saudi Arabia imedhamiria kukuza
zaidi mahusiano kati yake na Tanzania ili kuwaletea manufaa makubwa
wananchi.
Kwa upande wake, Dk Magufuli amemshukuru Mfalme wa Saudi Arabia kwa
kumtumia ujumbe na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuiongoza Tanzania na
amemhakikishia kuwa Serikali yake itafurahi kuona Saudi Arabia
inashirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa
Reli ya Kati na barabara.
Maeneo mengine ambayo Rais Magufuli na Waziri Adel Al Jubeir
wameyazungumzia ni ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika
kuendeleza elimu, utalii, bandari na miundombinu.
Pamoja na kufanya mazungumzo hayo, Rais Magufuli pia alishuhudia
utiaji saini wa mkataba kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi
Arabia katika nyanja za uchumi, biashara, uwekezaji, ufundi, vijana na
michezo.
Kwa upande wa Tanzania, mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi
Augustine Mahiga, na kwa upande wa Saudi Arabia umesainiwa na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel Al Jubeir.
Chanzo HabariLeo.
Thursday, 24 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment