Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa siku 60
kuanzia leo kwa wanufaika wote wa mikopo wanaodaiwa na bodi hiyo
wajitokeze ili kuanza kulipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua za
kisheria.
Aidha, katika muda huo uliotolewa, waajiri pia wanatakiwa kuhakikisha
wanatekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa
wao waliohitimu katika vyuo vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Jerry Sabi, alitoa taarifa hiyo
jana kwa vyombo vya habari na kuwataka waajiri kuwasilisha taarifa
zinazojumuisha majina kamili ya waajiriwa, vyuo na mwaka waliohitimu.
“Hivyo basi, taarifa hii inalenga kuwakumbusha waajiri ambao bado
hawatimizi wajibu wao kisheria (kifungu cha 20) wa kuwasilisha majina ya
waajiriwa wao wote ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu kwa HESLB ndani ya
siku 28 tangu waajiriwe,” alisema Sabi.
Alifafanua kwamba, adhabu ya kutotekeleza wajibu huo kwa mwajiri ni
faini ya Sh milioni saba au kifungo au vyote kwa pamoja. Sheria
iliyoanzisha HESLB (Sura 178) (kama ilivyorekebishwa) inatoa wajibu kwa
mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu na pia wajibu kwa mwajiri.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, baada ya Bodi kupokea orodha kutoka kwa
mwajiri, itafanya uchambuzi kubaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu
na kumwelekeza mwajiri kuingiza makato ya marejesho kwenye mshahara wa
mnufaika na kuwasilisha makato hayo kwa HESLB.
Adhabu ya kutowasilisha makato kwa bodi ni faini ya asilimia 10 ya
makato yote ambayo hayajawasilishwa na faini hii inapaswa kulipwa na
mwajiri. Taarifa hiyo ya kaimu mkurugenzi, imefafanua kwamba, pamoja na
wajibu wa mwajiri, wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu tangu mwaka
1994, wana wajibu wa kisheria (Kifungu cha 19 cha sheria ya HESLB),
pamoja na mambo mengine, kutaarifu bodi kwa maandishi mahali alipo na
kuandaa utaratibu wa kulipa deni lake la mkopo wa elimu ya juu.
Iwapo mnufaika wa mkopo atashindwa kutoa taarifa hizo, adhabu yake ni
kushitakiwa mahakamani. “Aidha, HESLB inapenda kuwakumbusha wazazi,
walezi na wadhamini wa wanafunzi walionufaika na mikopo kuwa wana wajibu
wa kisheria (chini ya kifungu cha 22 cha sheria ya HESLB) wa
kuhakikisha kuwa taarifa muhimu za mnufaika waliyemdhamini zinaifikia
HELSB.”
Taarifa husika ni pamoja na mahali alipo mnufaika, majina aliyotumia
wakati akipata mkopo, mwajiri wake na kuhakikisha mnufaika aliyemdhamini
anarejesha mkopo wake kwa bodi. Kaimu Mkurugenzi, katika taarifa yake,
alisema lengo la bodi ni kuhahakisha madeni yote yanakusanywa kuongeza
uwezo wa kukopesha Watanzania wengi zaidi.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 13 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment