Sunday, 13 March 2016

Tagged Under:

JWTZ Wamuokoa Daktari Aliyesusiwa Maiti na Wananchi Wakimtuhumu Kusababisha Kifo cha Mgonjwa Wao

By: Unknown On: 21:35
  • Share The Gag

  • Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kambi ya Ikola wamelazimika kulinda nyumba ya mganga wa Zahanati ya Kapalamsenga iliyopo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi baada ya wanakijiji kupanga kutelekeza mwili wa mgonjwa wanayedai daktari huyo amesababisha kifo chake kwa kukataa kumtibu.

    Tukio hilo lilitokea juzi saa 10.00 alfajiri baada ya wanakijiji kupata taarifa kuwa mgonjwa wao huyo, Bibiana Karangi (49) ambaye mganga huyo alidaiwa kukataa kumtibu, amefariki.

    Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Hamad Mapengo alisema siku ya tukio saa saba usiku, mgonjwa huyo alifikishwa katika zahanati ya kijiji hicho na walipomuamsha mganga huyo nyumbani kwake umbali mita 20, alikataa akiwataka wampeleke Kituo cha Afya Karema.
    Inadaiwa kuwa mgonjwa huyo alipofikishwa Kituo cha Afya Karema aligundulika kuwa na upungufu wa damu, hivyo alitakiwa apelekwe Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, lakini wakati akiwa bado kituoni hapo alifariki dunia.

    Baada ya mgonjwa huyo kufariki, wanakijiji hao walipata taarifa ndipo waliamua kukusanyika kwa lengo la kwenda Karema kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka nyumbani kwa mganga wa zahanati hiyo ili wamsusie afanye maziko mwenyewe wakidai ndiye aliyesababisha kifo hicho kwa kutompatia huduma mapema.

    Kutokana na mpango huo, viongozi wa kata hiyo walipata taarifa hizo na kuomba msaada kwa wanajeshi wa Ikola ambao walifika na kuizingira nyumba ya mganga huyo, hivyo kuwalazimu wananchi hao kuanza kutawanyika.

    Mwenyekiti huyo alisema kutokana na mazingira hayo ilimlazimu yeye na kaimu mganga mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Naibu Mkongwa kwenda kumuondoa mganga huyo na kumpeleka mjini Mpanda kwa kuhofia usalama wake na familia yake.

    Baada ya kuondolewa kijijini hapo ndipo askari wa JWTZ walipoondoka nyumbani kwa mganga huyo.

    Ofisa Tarafa wa Karema, Zawadi Mirambo alifika kijijini hapo na kufanya kikao na wananchi, lakini maoni ya wanakijiji hao yalitofautiana na wauguzi ambao walidai mgonjwa huyo alikuwa na maradhi, hivyo ushauri wa kwenda kituo cha jirani ulikuwa sahihi.

    Hata hivyo, wanakijiji hao walidai imekuwa ni kawaida kwa mganga huyo kukataa kutoa huduma kwa wagonjwa usiku hata kwa wajawazito.
    ==

      Credit;Mpekuzi Blog 

    0 comments:

    Post a Comment