Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango.
WAKATI Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ikitangaza
kuinyima Tanzania msaada wa Dola za Marekani 473 (zaidi ya Sh trilioni
1), Serikali imesema ilishajiandaa kuhusu hatua hizo na fedha hizo
haikuzijumuisha katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2016/17.
MCC imezuia fedha hizo za maendeleo kutokana na hatua ya Tanzania
kuitisha uchaguzi wa marudio ya Zanzibar pamoja na kutumika kwa Sheria
ya Makosa ya Mitandao. Chini ya Mpango wa Uwekezaji wa MCC–2, fedha hizo
zilikuwa ziende katika kuboresha huduma za umeme, ikiwamo kusambaza
umeme katika vijiji vingi zaidi nchini.
Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka
asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo ilitokana na
msaada wa MCC-1. Fedha hizo zilikuwa ni awamu ya pili ya msaada kutoka
MCC na tayari katika awamu ya kwanza, Tanzania ilipokea Dola za Marekani
milioni 698 ambazo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara za
Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili
ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme
katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara, zilitumika kutandaza njia
ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na
Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga barabara zote kuu za Kisiwa
cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.
Kauli ya Waziri wa Fedha Akizungumzia na gazeti hili jana, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alisema tangu Desemba mwaka jana
walishasoma alama za nyakati na hivyo kuamua kutozijumuisha fedha za
MCC-2 katika maandalizi ya Bajeti ya Serikali yanayoendelea kwa mwaka
ujao wa fedha.
“Tulisoma kwenye mitandao matamshi ya viongozi wa Mfuko huo ndio
maana tukaamua kutozijumuisha fedha za MCC kwenye bajeti ya mwaka ujao
wa fedha, hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya kusitishwa kwa
msaada huo,” alisema Dk Mpango.
Hata hivyo, alisema Serikali itatoa tamko rasmi baada ya kupata barua
kutoka MCC ikiwaeleza wamesimamisha msaada huo hadi lini na nini
Tanzania inatakiwa kufanya ili kupata msaada huo. “Sisi tukipata hiyo
barua tutaitafakari na tutawajibu,” aliongeza waziri. Alisema Serikali
bado inaamini uhusiano wa Tanzania na Marekani ni mzuri na wa muda mrefu
hivyo huko mbele kutakuwepo na maelewano na fedha hizo zitatolewa.
“Sisi sio nchi ya kwanza kusimamishiwa msaada huo, Malawi waliwahi
kunyimwa lakini baadaye walipewa, na mimi bado naamini tutaelewana huko
mbele ya safari,” alibainisha. Dk Mpango pia alitoa mwito kwa Watanzania
kuiunga mkono Serikali inapokusanya maduhuli kutoka vyanzo visivyo vya
kodi na wahakikishe wanalipa kodi inayostahili ili nchi iondokane na
utegemezi wa wahisani.
“Hili liwe fundisho kwetu kwamba nchi itapiga maendeleo kwa kutegemea
vyanzo vya ndani, hatuwezi kuwa tegemezi miaka yote ni lazima ifike
mahali tusimame kwa miguu yetu na tutafanikiwa tu iwapo tutalipa kodi
stahiki,” alisema Dk Mpango.
Uamuzi wa MCC Desemba 2015, Bodi ya Wakurugenzi ya MCC iliahirisha
upigaji kura ya kuichagua tena Tanzania kufuzu vigezo vya kupata mkataba
wa mpya wa MCC kutokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar na
kusisitizia haja ya kukamilishwa haraka, kwa haki na kwa amani kwa
mchakato wa uchaguzi.
Aidha, Bodi ilihitaji kupata uthibitisho kutoka kwa Serikali ya
Tanzania kwamba Sheria ya Makosa ya Mitandao isingetumika kukwaza uhuru
wa kujieleza na kujumuika, hususan kuhusu matumizi ya sheria hiyo
kuwakamata watu kadhaa wakati wa uchaguzi. Wasiwasi huu ulirejelewa mara
kadhaa, ikiwa ni pamoja na katika tamko lililotolewa na Balozi Mark
Childress.
Mojawapo kati ya vigezo vya msingi kabisa ambavyo MCC hutumia kuingia
ubia na nchi yoyote, ni dhamira ya dhati ya nchi hiyo kuimarisha
demokrasia na kuendesha chaguzi zilizo huru na za haki.
Chaguzi visiwani Zanzibar na matumizi ya Sheria ya Mtandao yanakwenda
kinyume kabisa na dhamira hii, imedai Marekani. “Kwa sababu hiyo,
wakati ambapo Marekani na Tanzania wanaendelea kuchangia vipaumbele
vingi, Bodi ya Wakurugenzi ya MCC imeona kwamba Serikali ya Tanzania
imekuwa ikichukua hatua zisizoshabihiana na vigezo vya kupata sifa ya
kuingia ubia na MCC. Hivyo basi, Bodi ilipiga kura kusitisha ubia wake
na Serikali ya Tanzania.
Kwa hali hiyo, MCC inasimamisha shughuli zote zinazohusiana na
maandalizi ya mkataba wa pili na Tanzania,” ilieleza. Balozi wa Marekani
anena Katika tamko lake, Balozi wa Marekani nchini Mark Childress
alisema, “Ninaunga mkono kikamilifu uamuzi huo wa Bodi wa kusitisha
maandalizi ya mkataba wa pili. Marekani na Tanzania tumekuwa na uhusiano
wa muda mrefu na wa kina katika sekta nyingi.
“Tukiwa mbia mkubwa zaidi wa maendeleo kwa Tanzania, Marekani
itaendelea kufanya kazi pamoja na Tanzania katika kuboresha afya na
elimu, kukuza uchumi na kuimarisha usalama,” alisema Balozi Childress.
Maoni ya wachumi Mkurugenzi wa Asasi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini
(REPOA), Profesa Samuel Wangwe alisema athari ya msaada wa MCC ni ndogo
kwa uchumi wa nchi kwa kuwa nusu ya fedha hizo zingerudi Marekani
kutokana na mfumo wa masharti hayo.
Alisema dawa ya kujitegemea ni kama ile aliyoitoa Rais John Magufuli
kutumia rasilimali za ndani kuendeshea shughuli za maendeleo badala ya
kutegemea misaada kutoka nje. Profesa Wangwe alihoji kama suala ni
kuminya demokrasia, vitendo ambavyo Marekani imefanya Irak na Libya ndio
kielelezo cha demokrasia?
Alisema kuna haja kubwa ya kuwa na chombo cha umoja wa kimataifa
kifafanue demokrasia gani inakubalika ulimwengune, lakini sio kwa maana
inayotaka Marekani. Naye Mtaalamu wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk Haji Semboja alisema Marekani haina rafiki katika nchi
maskini na haina utamaduni wa kuzisaidia nchi maskini isipokuwa
inasaidia pale inapokuwa na ajenda zake na pale inapotokea wanabadili
ajenda zao lazima watoe sababu ya kusitisha msaada.
“Misaada ya kimarekani ni ya kipuuzi na hata watu wenye akili
hawawezi kuupigia bajeti kwa sababu wakati wowote taifa hilo linaweza
kutoa sababu za kipuuzi kukunyima msaada ambao imekuahidi na hiki ndicho
kilichotokea kwani suala la Zanzibar halihusiani na msaada huo,”
alisema Dk Semboja. Alisema kisingizio cha Zanzibar na sheria ya
mitandao kilichotumiwa na Marekani havina maana na hiyo inatokana na
taifa hilo kutokuwa na historia ya kuzisaidia nchi maskini kwa sababu.
Alisema msaada wa MCC ulitokana na urafiki uliokuwepo kati Rais
George Bush na Rais Kikwete na sio kati ya Serikali ya Tanzania na
Marekani. “Serikali haikupaswa kuweka fedha za msaada wa Marekani kwenye
bajeti, wenzetu wa Kenya walishafanya hivyo kwa sababu ya ubabaishaji
wa Marekani, lakini sisi kwa kuwa ni masikini wa akili tunaweka bajeti
kwa kutegemea mfuko wa mtu mwingine na madhara yake ndo haya,” alisema
Dk Semboja.
Naye Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk
Ulingeta Mbamba alisema ni kweli kufutwa kwa msaada huo kutakuwa na
athari kwa uchumi ila akaeleza kuwa kama nchi ni lazima ijenge misingi
ya kujitegemea. “Sijalisoma hilo tamko lao, ila najua hizo fedha ilikuwa
ziende kwenye umeme, hili liwe funzo kwetu kwamba msaada sio suluhu ya
maendeleo ya nchi yetu, kujitegemea ni kuzuri zaidi,” alisema Profesa
Mbamba.
Kigeugeu cha MCC Septemba 26, 2015, Rais mstaafu Jakaya Kikwete
alihakikishiwa na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana Hyde katika mkutano
uliofanyika katika Hoteli ya JW Marriot Essex House, New York, na
kuhudhuriwa na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Kamran Khan, Makamu
wa Rais wa Operesheni za MCC.
“Hongera Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote
ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC - 2, ikiwa ni pamoja na
uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati
kupambana na rushwa,” alisema Hyde wakati huo akimueleza Rais Kikwete.
Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry
imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika masharti ya
kupata fedha za MMC kuwa ni kweli Tanzania inakabiliana ipasavyo na
rushwa na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na janga hilo la rushwa.
Chanzo HabariLeo.
Tuesday, 29 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment