Sunday, 27 March 2016

Tagged Under:

Askofu aonya maadui ndani ya Kanisa

By: Unknown On: 22:23
  • Share The Gag

  • ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa

    ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa ameonya juu ya kuwepo hatari ya kusambaratika kwa makanisa nchini kutokana na kuibuka kwa maadui ndani ya makanisa yenyewe.

    Alisema katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka vikwazo vinavyohatarisha mhimili wa kanisa nchini ikiwemo mashindano baina ya madhehebu, vita baina ya maaskofu, ulaghai, wizi, fitna na matendo maovu.
    Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amepiga marufuku makanisa kutumia polisi kwenye migogoro yao na kuwa watakaotoa taarifa ya kuomba polisi ili kuingilia masuala ya kanisa watawekwa mahabusu.

    Askofu Dk Mokiwa aliyasema hayo alipokuwa akitoa mafundisho katika Ibada Kuu ya Sikukuu ya Pasaka ambayo kitaifa ilisaliwa katika Kanisa la Anglikana la St Albano, Upanga jijini Dar es Salaam jana.
    Akizungumzia kuhusu mashindano baina ya makanisa yenyewe, Askofu Mokiwa alisema tofauti na miaka ya nyuma ambako Wakristo bila kujali tofauti yao ya kimadhehebu walikuwa wakiishi kwa umoja, upendo na maelewano, hali ni tofauti sasa kwani kumeibuka mashindano baina ya madhehebu.
    “Hivi sasa Kanisa hili linataka kujionesha kuwa ni bora kuliko lingine, linataka kuonekana maaskofu wake wana sauti ya kusikilizwa kuliko wengine, linataka kuonesha lina shule na vitega uchumi vingi kuliko lingine, linataka kuonesha lina fedha nyingi kuliko lingine, mambo ambayo hayana msingi katika Ukristo,” alisema Askofu Mokiwa.

    Kuhusu vita baina ya maaskofu, Dk Mokiwa alisema kumeibuka jambo la hatari kwa maaskofu wa madhehebu tofauti kuanza kutukanana, kushutumiana, kufanyiana hujuma na hata kutaka kuangushana, hatua ambayo inatia shaka mustakabali wa uhai wa Kanisa. “Anasimama askofu wa dhehebu moja anamtukana askofu mwenzake hadharani bila aibu.
    Askofu anadiriki kuvuka mipaka yake anazungumzia madhehebu yasiyomhusu kama vile yeye ni kiongozi wa madhehebu yote nchini jambo ambalo ni la hatari kwa Kanisa,” alisema Dk Mokiwa.
    Alisema kama hiyo haitoshi sasa kumeingia ulaghai, wizi, fitna, majivuni na matendo mengine maovu ndani ya Kanisa, hatua ambayo alisema inakwenda kinyume cha mafundisho ya Mungu kuhusu Kanisa na alionya kuwa ni lazima mtindo huo ukemewe ili ukome mara moja kwa nia ya kulinusuru Kanisa.

    “Hatuwezi leo hii kuzungumzia maadui wa nje wakati wapo maadui wa ndani ya Kanisa lenyewe ambao ni hatari zaidi na wanahatarisha uhai na ukuaji wa kiroho. Naomba kuyapongeza makanisa ambayo yameendelea kuonesha utulivu na kufuata misingi ya Kanisa, lakini kwa wale wanaokiuka misingi ya Ukiristo ni lazima tuwaeleze,” alisema.
    Kwa upande wake, akitoa salamu za Sikukuu ya Pasaka katika Ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Makonda alieleza kushangazwa na hatua ya makanisa kuanza mtindo wa kutumia vyombo vya dola ili kushughulikia mambo yao ya ndani na kwamba hatakubali kuona mtindo huo ukiendelea kutokea.

    “Ni jambo la aibu sana kuona sasa badala ya sisi serikali kuja kanisani kuomba msaada wa kuleta amani na utulivu ndani ya jamii, eti makanisa ndiyo yanakuja serikalini kuomba ulinzi wa polisi ili waweze kutimiza lengo fulani.
    Imefikia hatua watu wanataka kumsimika Askofu halafu eti wanaomba ulinzi wa polisi. “Labda niseme tu kwamba hilo mimi sitalikubali. Ni lazima makanisa yawe mfano wa kushughulikia masuala yao kwa misingi ya kiroho.

    Kuanzia sasa mtu atakayekuja kwangu kuomba ulinzi wa polisi katika masuala ya Kanisa nitamweka ndani yeye kwanza kabla ya kuwashughulikia wengine,” alisema Makonda.
    Alisema ni lazima viongozi na Wakristo warudi katika misingi ya kidini inayosimamia namna ya kumaliza matatizo yaliyopo ndani ya makanisa yao ili kuondoa aibu ambayo imeanza kusababishwa na baadhi ya Wakristo na kuchafua sifa nzima ya makanisa nchini.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment