Rais Dk John Magufuli.
UJUMBE wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) umeridhishwa na juhudi
zinazofanywa na Serikali ya Rais John Magufuli katika kuongeza juhudi za
kupambana na rushwa. Hali hiyo itabadili mtazamo wa awali kwamba
utawala bora ulishapotea nchini, kama ilivyoonekana katika tafiti nyingi
zilizofanyika.
Aidha, ujumbe huo unaunga mkono malengo ya uchumi yaliyomo katika
mwongozo wa Bajeti ya mwaka 2016/2017 uliochapishwa, ambayo yamezingatia
uhalisia katika ukadiriaji wa mapato.
Hayo yalielezwa katika taarifa ya shirika hilo, iliyotolewa kwa
vyombo vya habari jana Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa ziara ya
ujumbe huo ulioongozwa na Mkurugenzi Msaidizi na Mkuu wa IMF nchini,
Herve Joly. Ujumbe huo pia ulifanya tathmini ya nne ya Mpango wa Ushauri
wa Sera za Uchumi (PSI), ulioidhinishwa na Bodi Tendaji ya IMF mwaka
huu.
Ilieleza taarifa hiyo kuwa “ujumbe umeridhishwa na juhudi
zinazofanywa na serikali katika kuongeza juhudi zaidi za kupambana na
rushwa, hali ambayo itabadili mtizamo wa awali kwamba utawala bora
ulikwishapotea nchini kama ilivyoonekana kwenye tafiti nyingi
zilizofanyika.”
Tangu aingie madarakani Novemba mwaka jana, Rais John Magufuli na
serikali yake imejipambanua kwa kupambana na rushwa na ufisadi kwa
kuwachukulia hatua wakwepa kodi na watendaji wa serikali ambao ni wala
rushwa, kuwapeleka mahakamani na kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwongozo wa bajeti ya Tanzania kwa mwaka
2016/17 umezingatia kupunguza kwa kiasi kikubwa nakisi ya bajeti na
matumizi ya kawaida ili kutoa fursa ya kuongeza matumizi ya maendeleo.
“Changamoto kubwa katika kukamilisha bajeti ni kuhakikisha kuwa matumizi
yanaendana na mapato halisi. Majadiliano yataendelea katika wiki chache
zijazo ili kufikia muafaka juu ya mfumo mzima wa sera za uchumi ambazo
zitapelekwa kukamilisha mapitio ya nne ya mpango wa PSI,” ilieleza
taarifa hiyo.
Mapitio hayo ya mpango wa PSI na majadiliano chini ya kanuni ya nne
ya mkataba ulioanzisha IMF, yanatarajiwa kujadiliwa na Bodi Tendaji ya
IMF mwaka huu. Majadiliano chini ya mpango wa PSI pia yamelenga kwenye
utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 na mipango ya bajeti ya mwaka
2016/2017.
Katika taarifa hiyo, Joly alisema mwenendo wa uchumi umeendelea
kuimarika kwani makadirio yanaonesha kuwa Pato la Taifa kwa mwaka jana
lilikua kwa asilimia saba, huku shughuli zilizokua kwa kasi ni ujenzi,
mawasiliano, huduma za kifedha na uchukuzi. “Mfumuko wa bei umeendelea
kubakia kwenye kiwango cha tarakimu moja muda wote wa mwaka 2015 na
kufikia wastani wa asilimia 5.6, japokuwa thamani ya Shilingi ilishuka
kwa kiasi kikubwa katika nusu ya mwaka,” alisema Joly.
Alisema majadiliano na serikali chini ya kanuni ya nne ya mkataba wa
IMF yalijikita kwenye namna ya kuendeleza ukuaji wa uchumi kwa kiwango
cha juu unaozingatia utekelezaji wa vipaumbele vya serikali bila
kusababisha athari za kiuchumi. Hata hivyo, mabadiliko makubwa ya
kimfumo yanahitajika ili kuboresha mfumo mzima wa kiuchumi na kuongeza
tija katika uzalishaji na uwekezaji.
“Kumekuwa na mtazamo sawa wa maoni kwenye maeneo ya vipaumbele vya
maboresho ya kiuchumi na jinsi serikali itakavyochangia katika kuwezesha
uchumi endelevu na unaoongozwa na sekta binafsi,” aliongeza Joly.
Alisema uboreshaji wa sekta ya kilimo inayoajiri idadi kubwa ya watu
utasaidia kuongeza kipato cha watu wa vijijini na hiyo kuchangia
kupunguza umasikini.
Aidha, utatoa fursa ya ajira kwa sekta nyingine za uchumi na kukuza
viwanda mbalimbali ikiwemo vya kusindika vyakula. Kipaumbele kingine ni
kuboresha mazingira ya kufanya biashara, ikiwa ni pamoja na upatikanaji
wa nishati na miundombinu bora ya usafirishaji na upatikanaji wa ardhi
na mitaji.
Aidha, kuendelea kuimarisha hali ya kifedha ya Shirika la Umeme
(Tanesco) na kulipa malimbikizo ya madeni ya huduma za gesi na umeme ni
muhimu katika kuwawezesha wawekezaji binafsi kuendelea kuwekeza kwenye
sekta ya nishati. “Tanzania inaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa na
kukamilika kwa soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo
litasaidia kuvutia mitaji na kukuza ushinda na kuongeza ufanisi,”
alisema.
Wakati huo huo, mapato ya serikali kwa mwezi huu yamefikia Sh
trilioni 1.4, kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Mpango
alieleza mchanganuo wa fedha hizo kuwa ni mapato ya kodi (Mamlaka ya
Mapato Tanzania -TRA) ni Sh 1,283,274,000,000, mapato yasiyo ya kodi Sh
77,504,000,000 na mapato yatokanayo na vyanzo vya Halmashauri Sh
43,490,000,000, kufanya jumla ya Sh 1,404,268,000,000.
“Tunatarajia pia kupata mikopo na misaada ya mifuko ya ‘Basket’ na
miradi ya maendeleo kutoka kwa washirika wa maendeleo shilingi
71,200,000,000,” alieleza Dk Mpango. Akieleza mchanganuo wa matumizi, Dk
Mpango alisema yametumika katika kulipa mishahara ya watumishi wa
Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, watumishi wa Taasisi na Wakala za
Serikali pamoja na malimbikizo ya Sh 518,822,320 kwa Taasisi na Wakala
24 na hasa sehemu kubwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo jumla ya
mishahara ni Sh 582,043,000,000.
Alitaja matumizi mengine ni kulipia posho ya chakula kwa ajili ya
vyombo vya ulinzi na usalama, ruzuku ya vyama vya siasa, posho ya
madaktari wanafunzi 1,608, Wizara ya Afya ununuzi wa dawa na vifaa tiba,
mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa semista ya tatu, kutekeleza
mpango wa Elimu bure na mapato ya ndani kwa Halmashauri kwa ajili ya
miradi na uendeshaji wa ofisi.
Mengine ni madeni ya watumishi wasio walimu katika Halmashauri,
miradi ya umeme, Wakala wa Umeme Vijijini, Mradi wa Umeme Kinyerezi I,
Mradi wa Kufua Umeme Makambako – Songea, malimbikizo ya madeni ya
makandarasi wa barabara, miradi ya maji, Mfuko wa Reli, fidia kwa
wananchi kupisha mradi wa Kurasini Trade and Logistic Hub, Mradi wa
Ununuzi wa Dawa na Vifaa Tiba (ORIO) na Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya
Jimbo.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 23 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment