Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samiah Hassan Suluhu.
KAZI ya kusimamia Sh milioni 50 zilizopangwa kutolewa kwa kila kijiji
kwa ajili ya kukabili umasikini wamepewa wakuu wa mikoa. Makamu wa
Rais, Samia Hassan Suluhu alisema jana kwamba Serikali imejiandaa
kutimiza ahadi ya kutoa fedha hizo na utekelezaji wake, utaanza katika
bejeti ijayo ya mwaka 2016/2017.
Akizungumza baada ya wakuu hao wa mikoa kutia saini kiapo cha utii,
Ikulu Dar es Salaam , Samia alisema fedha hizo lengo lake ni kupunguza
umasikini kuanzia ngazi ya chini. “Najua kuna taasisi mbalimbali
zimekuwa zikiwafikia na kuwasaidia wananchi katika hili ukiwemo Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na
Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) lakini bado kuna kazi kubwa ya
kuwafikia wananchi masikini,” alisema Mama Suluhu.
Alisema fedha hizo zimeanza kuingizwa kwenye bajeti hiyo na
zinategemewa kusambazwa katika vijiji vyote mwanzoni mwa utekelezaji wa
bajeti hiyo. “Napenda niwafikishie maagizo ya Rais John Magufuli kwenu
kuwa fedha hizi zinakuja kwenu zisimamieni ili zifanye kazi
iliyokusudiwa,” alisisitiza.
Awali kabla ya viongozi hao kutia saini hati hiyo ya kiapo cha utii,
Kamishna Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili, Jaji Salome Kaganda, alisema
hati hiyo ya kiapo cha maadili ni lazima kila kiongozi aisaini kwa
mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aliwataka wakuu hao wa mikoa ambao hawakubaliani na kiapo hicho cha
utii kuhakikisha kuwa hawasaini hati hiyo na hivyo sekretarieti hiyo
itawasilisha majina yao kwa Rais Magufuli ikiwa ni ishara kwamba
wameukataa uteuzi wake.
Hata hivyo, wakuu hao wa mikoa kwa pamoja walisoma kwa sauti kiapo
hicho ambacho kinawataka kuheshimu wadhifa wao, kuepuka rushwa,
kutokutoa siri za ndani katika kazi zao, kuwahudumia wananchi, kupambana
na ubadhirifu na ufisadi lakini pia kusimamia maendeleo pamoja na
usalama wa mikoa yao.
Chanzo HabariLeo.
Tuesday, 15 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment