Jengo la Mahakama Kuu.
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Shirika la Ndege (ATCL) David Mattaka, na
wenzake wawili, wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka ya
matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh
bilioni 86.5.
Mattaka anadaiwa kusababisha hasara hiyo kutokana na kusaini mkataba
wa kukodi ndege bila kufuata Sheria ya manunuzi ya umma pamoja na
ushauri wa kiufundi. Mbali na Mattaka washtakiwa wengine waliofikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni aliyekuwa Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) Ramadhani Mlinga pamoja
na Mkurugenzi wa Sheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashitaka
sita na Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Timony pamoja na mawakili
kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Peter Vitalis
na Stanley Luoga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Respicius Mwijage.
Wakili Timony alidai kuwa, Oktoba 9, 2007 katika ofisi za ATCL Dar es
Salaam, Mattaka akiwa Mkurugenzi wa shirika hilo, alitumia madaraka
yake vibaya kwa kusaini makubaliano ya kukodi ndege yenye namba A
320-214, kati ya ATCL na kampuni ya Wallis Trading Inc, bila kufuata
sheria ya manunuzi ya umma na taratibu za zabuni.
Aliendelea kudai kuwa, Oktoba 27, 2007, Mattaka alitumia madaraka
vibaya kwa kusaini makubaliano ya kukodi ndege hiyo bila kufuata ushauri
wa kiufundi. Katika mashitaka mengine, inadaiwa kati ya Oktoba 27, 2007
na Aprili 24, 2008, Mattaka alisaini makubaliano hayo bila kufuata
ushauri wa kiufundi jambo ambalo lilisababisha shirika hilo kupata
hasara ya dola za Kimarekani 772,402.08 ambazo zililipwa kwa kampuni ya
Aeromantenimiento kama gharama ya matengenezo ya ndege hiyo.
Aidha inadaiwa kati ya Oktoba 27 na Novemba 29, 2007, Mattaka
aliidhinisha makubaliano hayo bila kufuata ushauri wa kiufundi na
kusababisha hasara ya dola za kimarekani 35,984.82, ambazo zililipwa kwa
kampuni ya Lantal textiles kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali vya
ndege hiyo.
Wakili Timony aliendelea kudai, kati ya Oktoba 27, 2007 na Oktoba 26,
2011, kwa kutumia madaraka yake vibaya, Mattaka aliidhinisha
makubaliano hayo na kuisababishia serikali hasara ya dola za Kimarekani
42,459,316 ambazo ATCL iliilipa kampuni ya Wallis Trading Inc.
Katika mashtaka yanayowakabili, Mlinga na Soka, inadaiwa Machi 19,
2008, katika ofisi za PPRA, Ilala Dar es Salaam, kwa lengo la kufanya
udanganyifu, walighushi muhtasari wa kikao cha Machi 19, 2008, kwa lengo
la kuonesha siku hiyo, PPRA ilifanya kikao kujadili maombi ya kuruhusu
makubaliano ya ATCL kukodi ndege.
Baada ya kusomewa mashitaka, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu
mashtaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo
isipokuwa Mahakama Kuu. Wakili Timony alidai upelelezi wa kesi bado
unaendelea, pia hawana pingamizi la dhamana kwa Mlinga na Soka kwa kuwa
shitaka linalowakabili lina dhamana.
Hata hivyo alidai wanapinga dhamana ya Mattaka kwa kuwa mahakama hiyo
haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa mashtaka ya Uhujumu Uchumi pia
mashitaka yanayomkabili yanahusisha zaidi ya Sh bilioni 10, hivyo
alishauri awasilishe maombi ya dhamana katika Mahakama Kuu.
Mlinga na Soka waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya
kuwa na mdhamini mmoja alisaini hati ya Sh milioni 10, Mattaka
alirudishwa rumande. Hakimu Mwijage aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 29
mwaka huu itakapotajwa tena.
Chanzo HabariLeo.
Tuesday, 15 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment