WATU sita wamefariki baada ya msafara wa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
TAMISEMI, Suleiman Jaffo na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na
Serikali za Mitaa kupata ajali wilayani Bagamoyo katika mkoa wa Pwani
jana.
Ajali hiyo ambayo ilihusisha magari manne ambayo ni gari dogo aina ya
Toyota Blitz lenye namba za usajili T758 DES, lori la mchanga aina ya
Scania namba za usajili T738 DCW, Landrover Defender namba za usajili
STL 1620 na SM 10414 Nissan Patrol, ilitokea jana saa 5 asubuhi katika
eneo la Kerege.
Msafara wa Jaffo pamoja na Kamati hiyo ulikuwa ukitokea katika kata
ya Mapinga, kukagua mradi wa maji unaohudumia vijiji vitatu vya
Changoela, Mtambani na Mapinga ambako walienda kukagua miradi ya
Tamisemi pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani humo.
Akithibitisha vifo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Dk Amir
Batenga alisema ajali hiyo imesababisha vifo vya watu sita na majeruhi
10 ambao kati yao wanane walipelekwa Hopitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Alisema waliopelekwa Muhimbili hali zilikuwa mbaya kutokana na kupata
majeraha makubwa.
“Hawa wanane wamepelekwa Muhimbili, lakini mmoja alitibiwa na
kuruhusiwa na mwingine alitibiwa na kuchukuliwa na polisi,” alisema Dk
Batenga.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Mkuu wa Idara ya
Mipango na Uchumi wa Wilaya, Hilda Msele (59), Makame Ally (40) dereva
wa Tasaf, dereva wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wa Wilaya, Khalid
Hassan (40), Mwanasheria wa Wilaya, Tunsiime Duncan na Mchumi wa Wilaya
Ludovick Pallangyo.
Waliojeruhiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bagamoyo, Ibrahim
Matovu, Mhandisi wa Maji wa Wilaya Juliana Msaghaa, Mratibu wa Tasaf
Wilaya, Dorothy Njetile na Mweka Hazina wa Wilaya, George Mashauri.
Wengine ni Mshauri wa Tasaf, Amadeus Mbuta, Mkuu wa Idara ya
Maendeleo ya Jamii wa Wilaya Julius Mwanganda, Tauliza Halidi na Amari
Mohammed ambao ni wananchi na Grace Mbilinyi aliyetibiwa na kuruhusiwa.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa Mhandisi
Msaghaa alifariki akiwa njiani kupelekwa Muhimbili kutokana na kuvuja
damu kwa wingi kwani aliumia maeneo ya kichwani. Akizungumzia ajali
hiyo, Jaffo alisema Tamisemi imesikitishwa na ajali hiyo kwani imepoteza
watu wake ambao ilikuwa ikiwategemea katika utendaji wa majukumu yao.
“Tumepoteza wafanyakazi wetu ambao tulikuwa tukiwategemea kutokana na
ajali hii…huku tulikuja kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya
maendeleo,” alisema Jaffo.
Hata hivyo, aliwataka madereva kuheshimu na kufuata sheria za
barabarani kwani ajali hiyo ilisababishwa na madereva wasiofuata sheria
jambo lililosababisha kuvamia msafara huo.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Lubeje alisema kutokana
na ajali hiyo, kamati yake imelazimika kusitisha ukaguzi wa miradi hiyo
ili kutoa nafasi ya kufanya maombolezo ya kuwapoteza watu hao.
Lubeleje ambaye ni Mbunge wa Mpwapwa (CCM), alisema ziara za ukaguzi
huo zilikuwa zifanyike katika vijiji vya Mapinga, Chasimba na Buma,
lakini imeahirishwa kutokana na ajali hiyo.
Chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari dogo aina ya Toyota Blitz
ambaye alikuwa akitokea Bagamoyo kwenda Dar es Salaam kulipita lori la
mchanga katika mlima bila tahadhari na kusimama ghafla baada ya kuona
msafara kabla ya lori hilo kumgonga kwa nyuma na gari hiyo kugeukia
lilipotoka.
Baada ya kuligonga gari hilo kwa nyuma dereva wa lori alishindwa
kulimudu gari hilo na kuligonga gari lingine aina ya Defender mali ya
Tasaf na baadaye gari la DED aina ya Nissan Patrol ambalo aligongana
nalo uso kwa uso.
Chanzo HabariLeo.
Monday, 21 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment