Sunday, 27 March 2016

Tagged Under:

Wenye tumbili wao walia na serikali

By: Unknown On: 22:30
  • Share The Gag

  • Tumbili.

    CHAMA cha Wasafirishaji wa Nyara Tanzania (TWEA) Kanda ya Kaskazini kimeiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuwaachia wanachama wao waliokamatwa mwishoni mwa wiki kwa tuhuma za kusafirisha tumbili hai 62 bila vibali huku wakieleza kuwa wapo tumbili wengine katika mabanda yao.

    Miongoni mwa waliokamatwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Arusha Bird Traders na raia wawili wa Uholanzi waliokamatwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wakituhumiwa kusafirisha tumbili hao.
    Akizungumza na waandishi wa habari jana hapa, Mwenyekiti wa Twea Kanda ya Kaskazini, Othman Bhoki alisema kukamatwa kwa raia hao wawili KIA ambao ni Arten Vardanian (52) na Edward Vardanian (46) pamoja na Idd Misanya ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni iliyotumika kukamata tumbili hao ya Arusha Bird Traders ni kuwarudisha nyuma wafanyabiashara ambao wana vibali halali vya kuvuna tumbili hao.

    Alisema wasafirishaji wa tumbili hao ambao ni Kampuni ya Arusha Bird Traders wana vibali halali vya kufanya biashara hiyo kwa maelekezo ya tangazo la Wizara ya Maliasili na Utalii.
    Alisema suala hilo ni vyema likachunguzwa kwa kina kwani kampuni hiyo imewasilisha kibali halali cha kusafirisha wanyama hao chenye namba 29655 (Cites) kilichotolewa Februari 24, mwaka huu ambacho kinamalizika muda wake Agosti 23, mwaka huu.

    Alisema kibali hicho kimeruhusu tumbili 62 kusafirishwa kwenda nchini Armenia na kukamatwa kwao kunaleta mkanganyiko kwani kwa mujibu wa kibali cha kukamata wanyama hao, kinaonesha kuruhusu daraja namba 13 la kuruhusu gawiwo la tumbili kuuzwa nje ya nchi.
    Alisema aina ya tumbili waliozuiwa wapo katika mgawo wa Taifa iliyoruhusu wauzwe tumbili 5,000 kwa mwaka na wafanyabiashara na gawiwo hilo kwa daraja tajwa lina tumbili aina mbili; Velvet Monkey na Blue Monkey (400).

    Alisema katika mazingira hayo wanashindwa kuelewa ni vigezo gani alivyotumia Waziri wa Maliasiali na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kuzuia wanyama hao kwenda nje ya nchi kwani daraja lililokatazwa kufanyiwa biashara ni la 14 ambalo linahusu wanyama wakubwa hasa wale wenye pembe na kwato.

    Alisema kinachoshangaza zaidi wakati tumbili hao wakizuiwa kusafirishwa huku wakurugenzi wakishikiliwa na Polisi, wanachama hao wa TWEA Kanda ya Kaskazini bado wana tumbili katika mabanda yao wanaosubiri kusafirishwa nje ya nchi katika masoko mbalimbali barani Ulaya.
    “Tunalaani kuitwa watoroshaji wa wanyama hawa wakati tuna vibali vinavyoturuhusu kusafirisha wanyama hawa tunaomba uchunguzi wa kina juu ya suala hili ili tujue hatma ya raia hao wanaoshikiliwa na polisi maana hapa kuna mkanganyiko na hatujui Waziri Maghembe amezuia kwa kibali gani ni hiki tulichonacho au la,” alisema.

    Naye Katibu wa Twea, Said Gumbo alisema kwa hatua hiyo ya Wizara kuzuia wanyama hao, wafanyabiashara hao wamewekwa katika mazingira magumu kwani wanaofanya biashara hiyo ni raia wa Tanzania wanaotafuta riziki zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.
    Aliiomba Serikali kufanya uchunguzi wa haraka wa tukio hilo na kuwaachia wanachama hao wanaoshikiliwa. Mwishoni mwa wiki, vyombo vya ulinzi na usalama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) viliwanasa wafanyabiashara wawili ndugu raia wa Uholanzi wakijaribu kusafirisha tumbili kwenda nchini Armenia.

    Wanyama hao wakiwa kwenye makasha sita tofauti ya kuhifadhia walikuwa wasafirishwe kwa ndege maalumu ya mizigo yenye namba EW/364G iliyosajiliwa Belarus kupitia Kampuni ya Arusha Freight Limited ya hapa.
    Mbali ya raia hao wa Uholanzi pia wanamshikilia Mtanzania, Misanya ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni iliyotumika kukamata tumbili hao ya Arusha Bird Traders anayedaiwa kuwauzia wanyama hao.
    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Wilbroad Mutafungwa alithibitisha kukamatwa kwa raia hao na wamehifadhiwa Kituo cha Polisi KIA huku uchunguzi zaidi wa tukio hilo ukiendelea.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment