Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)
waliofutiwa mikataba ya kazi, wamegoma kupokea barua za kuachishwa kazi
wakidai kwamba hawajui kilichoandikwa kuhusu hatima ya madai yao.
Wafanyakazi
hao walikutana jana Dar es Salaam na kiongozi wao, Seif Kibangu alisema
wamekubaliana kutochukua barua hizo hadi pale watakapopata ushauri
kutoka kwa wanasheria.
“Licha ya mishahara ya miezi mitatu tuna
madai yetu mengine ikiwamo makato ya mafao yetu yaliyotakiwa kupelekwa
kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, pia tumekuwa tukikatwa bima ya afya
asilimia tatu ya mishahara yetu hatujui hatma yake.
"Sasa leo wanataka
tuchukue barua hizo tena kwa kusaini kabla ya kujua kilichoandikwa
hapana tuendelee kuvumilia haki yetu tutaipata,” alisema Kibangu.
Aliwakosoa waliochukua barua hizo akisema waliajiriwa kwa makundi, ingawa pia wapo waliopewa kazi hiyo kwa vimemo.
“Hili
ni jasho letu, hatuibi cha mtu kwa hiyo tunastahili kupata haki zetu
zote, mishahara tunayodai kwa miezi mitatu, acha hayo madai mengine...
Tunadaiwa huko tunapoishi kwa kweli tunaomba wahusika waingilie kati
jambo hili linatuumiza na kuyumbisha maisha yetu,” alisema.
Akizungumza
kwa niaba ya madereva wenzake, George Mmari alidai kuna gharama nyingi
walizoingia ambazo Nida inapaswa kuzilipa ikiwamo malipo ya kuegesha na
kuosha magari waliyokuwa wakiendesha.
Akizungumzia madai hayo,
Ofisa Habari Mwandamizi wa Nida, Rose Mdami alieleza kushangazwa na
hatua ya wafanyakazi hao kugoma kuchukua barua zao badala ya kuzipokea
ili wajue kilichoandikwa ili kama wana madai waandike barua na
kuyaorodhesha.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment