Raisi wa Zanzibar, Dr. Ali Mohamed Shein akionesha cheti cha ushindi alichokabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),
Jecha Salim Jecha baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio
katika hafla ya kutangaza matokeo iliyofanyika katika ukumbi wa bwawani mjini humo jana.
MGOMBEA Urais wa CCM visiwani Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein
ametangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa mshindi kwa kupata
kura 299,982 sawa na asilimia 91.4. Kwa ushindi huo, Dk Shein ataiongoza
tena Zanzibar kwa muda wa miaka mitano akiwa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha ambaye amekuwa mafichoni tangu
atangaze kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, jana alijitokeza
hadharani kutangaza matokeo ya jumla ya uchaguzi uliofanyika juzi katika
visiwa vya Unguja na Pemba. Tofauti na utaratibu uliozoeleka kuwa ZEC
hutangaza kura walizopata wagombea urais kutoka kila jimbo na baadaye
kutangaza mshindi wa jumla, hali ilikuwa tofauti jana maana matokeo ya
jumla yalitangazwa kabla ya kutangaza matokeo ya kila jimbo.
Hata hivyo, wakati anatangaza matokeo hayo ya jumla, Jecha hakueleza
sababu ya kuanza kutangaza matokeo ya jumla kabla ya kutangaza matokeo
ya awali kutoka katika kila jimbo la uchaguzi. Majimbo ya uchaguzi ya
ZEC ni 54.
Matokeo ya Uchaguzi Katika matokeo aliyoyatangaza jana Jecha
yanaonesha kuwa mgombea wa ACT Wazalendo Khamid Idd Lila alipata kura
1,225 (0.4%), Juma Ali Khatib (ADA Tadea) kura 1,562 (0.5), Hamad Rashid
Mohamed (ADC) kura 9,734 (3.0%), Said Soud Said (AFP) kura 1,303
(0.4%), Ali Khatib Ali (CCK) kura 1,980(0.6%) na Mohammed Masoud Rashid
(Chaumma) kura 493 (0.2%).
Seif Sharif Hamad (CUF) kura 6,076 (1.9%), Tabu Mussa Juma wa
Demokrasia Makini alipata kura 210 (0.1%), Abdallah Komba Khamis wa DP
kura 512 (0.2%), Kassim Bakari Ali (Jahazi Asilia) alipata kura 1,470
(0.4), Seif Ali Idd (NRA) 266 sawa na asilimia 0.1, Issa Mohamed Zonga
(SAU) kura 2,018 (0.6% na Hafidh Hassan Suleiman (TLP) alipata kura
1,496 sawa na asilimia 0.5.
Idadi ya wapiga kura kwa mujibu wa Jecha ni 503,580 na watu waliopiga
kura juzi ni 341,865 ambayo ni sawa na asilimia 67.9 ya watu wote
waliojiandikisha. Kura zilizoharibika zilikuwa ni 13,538 sawa na
asilimia 4.0.
Hata hivyo, vyama kama CUF, ACT Wazalendo, Chaumma, Jahazi Asilia na
NRA ambavyo vilisimamisha wagombea urais katika uchaguzi wa 2015
vilishatangaza kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio uliofanyika juzi.
Jecha: Vyama vyote vimeshiriki Akizungumza jana kabla ya kumtangaza
mshindi wa kiti cha urais, Jecha alisema mara tu baada ya ZEC kupitisha
uamuzi wa kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Machi 20, 2016, Tume
ilifanya mawasiliano na vyama vyenye wagombea kwa lengo la kuwapa
taarifa juu ya matayarisho ya uchaguzi huo ili waanze taratibu za
uchaguzi.
Alisema kutokana na taarifa hiyo baadhi ya vyama vilitoa taarifa
kupitia vyombo vya habari kuwa havitashiriki katika uchaguzi na kuwataka
wagombea wao kuandika barua za kutoshiriki katika upigaji kura huo.
Alisema wagombea wa vyama hivyo waliandika barua kwa ofisi za wilaya na
makao makuu ya tume, hata hivyo hakuna mgombea hata mmoja aliyewasilisha
barua tume aliyefuata utaratibu wa kujitoa katika uchaguzi kama
ilivyofafanua katika Kanuni za Uchaguzi wa mwaka 2015.
Alifafanua taratibu hizo kuwa mgombea urais angejiondoa kwa kutoa
taarifa ya maandishi aliyotia saini mwenyewe atakayowasilisha kwa
mwenyekiti wa tume si zaidi ya saa 10 za jioni ya siku ya uteuzi ambayo
alifafanua kuwa kwa uteuzi wa wagombea wa uchaguzi wa juzi ulifanyika
Septemba 6, 2015. Alisema utaratibu huo unawahusu wagombea uwakilishi
ambao walitakiwa kuwasilisha barua kwa msimamizi wa uchaguzi katika muda
huo kabla ya saa 10.
Alisema wagombea waliokuwa na nia ya kujiondoa waliwasilisha barua
zao kwa kuchelewa na hawakuambatanisha barua hizo na tamko la kisheria
lililotiwa saini mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kwa wagombea urais na ya
Hakimu Mkazi kwa wagombea uwakilishi na Diwani. “Kwa kuwa utaratibu wa
kikanuni haukufuatwa, tume ilibaki na uamuzi kuwa pamoja na barua hizo,
wagombea wote walioteuliwa na tume ni halali kwa uchaguzi mkuu wa
marejeo na tuliwapatia haki zote wanazostahiki kupatiwa wagombea wa
uchaguzi,” alisema Jecha.
Dk Shein aahidi kutenda haki Mara baada ya kutangazwa mshindi na
kupokea cheti cha ushindi, Dk Shein aliahidi kutenda haki kwa kila
Mzanzibari na kwamba hatamdhulumu mtu yeyote haki yake, badala yake
alisema atahakikisha Zanzibar inapaa kimaendeleo kwa kusogeza ukuaji wa
uchumi uwe kati ya asilimia 8 hadi 10 katika miaka mitano ijayo.
“Nafahamu changamoto ya kazi hii, niko tayari kutumika tena kwa
uaminifu na nia yangu kwa watu wa Zanzibar ni kuwaletea maendeleo,
naahidi kuwa mambo mazuri yanakuja kwa watu wote bila kujali itikadi zao
za kisiasa,” alisema Dk Shein. Kuhusu mgogoro wa kisiasa uliopo
visiwani hapa, Dk Shein aliahidi kuushughulikia na kwamba peke yake
hawezi isipokuwa akaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi wote “Wote
naomba tushirikiane kutatua changamoto za kisiasa zilizoko hapa kwetu
kwani ni jukumu letu sote kuilinda na kuitetea Zanzibar yetu,” alisema.
Alivipongeza vyombo vya ulinzi kwa kuweka ulinzi uliowezesha watu
wapige kura kwa amani na utulivu. Aliahidi kuendeleza amani hiyo na
kueleza bayana kuwa hatakuwa na mjadala na mtu yeyote ambaye yupo kwa
ajili ya kuvuruga amani ya nchi. Pia aliwaasa wananchi wa Zanzibar
kupendana na kushirikiana katika shughuli zao za kijamii wakati Serikali
inajipanga kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi kwa kutumia uwezo
uliopo wa Serikali.
CCM yazoa majimbo yote Pemba, Unguja Aidha, CCM imeibuka na ushindi
mnono wa kishindo wa majimbo yote 18 ya uchaguzi katika kisiwa cha Pemba
kwa nafasi ya Uwakilishi na Udiwani ambayo katika uchaguzi uliopita
yalikuwa yameshikiliwa na CUF. Kwa mujibu wa Ofisa Mdhamini wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar Pemba, Ali Mohamed Dadi, matokeo ya uchaguzi ya
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yanaonesha CCM imeyachukua majimbo yote
ya Pemba na kuviacha vyama vingine vikishindwa kuambuliwa hata jimbo
moja.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
amethibitisha kuwa CCM imeshinda majimbo yote 36 ya uwakilishi katika
kisiwa cha Unguja. Pemba wafurahia ushindi wa Shein Wananchi wa kisiwa
cha Pemba katika mitaa mbalimbali walifurahia ushindi wa mgombea wa CCM
katika nafasi ya urais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein baada ya
kutangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Katika Mtaa wa Chake Chake pamoja na Wawi Pemba jimbo ambalo mgombea
wa nafasi ya urais kwa tiketi ya ADC, Hamad Rashid Mohamed alipiga kura,
walionekana wakishangilia ushindi huo ambao umekuja baada ya kufanyika
kwa uchaguzi wa marudio. “Huu ni ushindi wetu wa CCM lazima tushangilie
kwa nguvu zote kwa sababu umetokana na jasho la kujituma na kufanya kazi
kwa bidii kuhamasisha wapiga kura ambapo kazi hiyo tuliifanya katika
kipindi kigumu,” alisema mkazi wa eneo hilo, Juma Haji.
Mafunda Said ambaye ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la
Wawi, alisema ni ushindi ambao wanachama wa chama hicho wanapaswa
kushangilia kwa nguvu zote kwa sababu umekuja katika kipindi kigumu
zaidi baada ya kuibuka kwa siasa za chuki na uhasama Pemba ikiwemo
kuchomeana moto nyumba.
“Huu ni ushindi wetu ambao tunalazimika kuushangilia kwa nguvu zote
kwa sababu sisi CCM tulikuwa katika wakati mgumu ikiwemo wapinzani
kututisha pamoja na kuchomewa nyumba zetu moto ili tusiweze kwenda
kupiga kura,” alisema Said. Mkazi wa Mtaa wa Tibitinzi ambaye
alijitambulisha kwamba ni mfuasi wa CUF aliwataka wananchi wadumishe
amani na utulivu kwa sababu baada ya uchaguzi maisha yanaendelea kama
kawaida.
“Mimi ni mfuasi wa CUF kwangu kubwa naomba amani na utulivu hata watu
wanaofurahia ushindi huo wazingatie suala hilo ili isiwe kero kwa
wengine na kuanza kusababisha fujo na vurugu,” alisema. Hata hivyo,
mwandishi wa gazeti hili alipotembelea wilaya ya Wete ambayo ni ngome ya
CUF, wananchi wengi walikuwa wamejikusanya vikundi kwa vikundi
wakitafakari uchaguzi pamoja na matokeo yake.
Katika uchaguzi wa marudio wafuasi wengi wa CUF walisusia uchaguzi
huo kutokana na maelekezo yaliyotolewa na mgombea wa nafasi ya urais wa
Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, Maalim Seif
Sharif Hamad kwa madai kwamba uchaguzi uliofutwa ulikuwa halali.
Rais Magufuli ampongeza Shein Rais John Magufuli amemtumia salamu za
pongezi Rais Mteule wa Zanzibar, Dk Shein kutokana na ushindi wake huo,
akisema umedhihirisha imani na matumaini makubwa waliyonayo Wazanzibari
kwake na kwa CCM. Aidha, Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Zanzibar
kwa kushiriki katika uchaguzi huo kwa amani na utulivu, na hatimaye
kumpata mshindi wa kiti cha Urais ambaye atawaongoza kwa kipindi cha
miaka mitano.
“Naomba nikupongeze kwa dhati Mheshimiwa Rais Mteule, Dk Ali Mohamed
Shein kwa ushindi ulioupata, ushindi ambao umeonesha kuwa wananchi wa
Zanzibar bado wanahitaji uwaongoze kwa kipindi kingine cha miaka
mitano,” alisema Rais Magufuli. Dk Magufuli pia ameahidi kuwa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi bega kwa bega
na SMZ na amewataka Wazanzibari wote kujielekeza katika maendeleo kwa
kuwa uchaguzi umekwisha.
“Ndugu zangu wa Zanzibar uchaguzi umekwisha, kilichobaki sasa ni
kushirikiana na serikali yenu kuijenga Zanzibar na ninaamini mnao wakati
mzuri wa kuijenga Zanzibar yenye maendeleo chini ya uongozi wa Dk Ali
Mohamed Shein,” alisisitiza Dk Magufuli. Serikali ya Umoja wa Kitaifa
yazikwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iko njia panda kutokana na
matokeo yaliyotangazwa jana na ZEC kuonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) peke yake ndicho chenye haki ya kuunda Serikali.
Ni CCM pekee ambayo mgombea wake wa urais amepata zaidi ya asilimia
10 ya kura na ndiyo imezoa wawakilishi karibu wote na hivyo kubaki chama
pekee chenye sifa ya kuingia kwenye serikali ya umoja wa kitaifa.
Mshindi wa pili wa matokeo ya kura za urais ni Hamad Rashid Mohamed
aliyeambulia kura 9,734 sawa na asilimia 3. Akizungumzia hatma ya SUK,
alisema serikali hiyo itaendelea kuwepo kwani Rais aliyepo madarakani
lazima ateue watu kutoka kwenye vyama vya upinzani kuunda serikali hiyo.
Alisema kwamba yeye ana matumaini makubwa kuwa Dk Shein atamteua yeye
awe makamu wa kwanza wa rais kwa sababu katiba inaelekeza kuwa mshindi
anayefuatia kwa kura za urais ndiye mwenye sifa. Mwanasheria wa ZEC,
Issa Khamis alisema kwamba Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho
inafafanua kuwa mgombea aliyepata kura sio chini ya asilimia 10 ndiye
ataingia kwenye serikali hiyo na akaongeza kuwa Katiba hiyo iko kimya
kama sifa hiyo haitakuwepo.
Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo kuundwa kwa Serikali hiyo
kutategemea na maamuzi na utashi wa Rais aliyeshinda kwenye uchaguzi
huo. Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
alikiri kuwa kwa kuwa hakuna chama ambacho kimefikisha asilimia 10 ya
kura za urais isipokuwa CCM kama inavyotamkwa na Katiba ya Zanzibar.
Vuai alisema serikali ya kitaifa inaundwa kikatiba na kama hakuna
chama ambacho kina sifa za kuingia kwenye serikali hiyo ni wazi kuwa
hapo uundwaji wake unategemea busara na maamuzi ya Rais aliyepo
madarakani. “Katiba ya Zanzibar inasema chama chenye sifa ya kuingia
kwenye serikali ya umoja wa kitaifa kimewekewa kifungu maalum kuwa ni
lazima kipate kura za urais walau asilimia 10 kwa matokeo ya leo hakuna
chama kilichopata asilimia hiyo isipokuwa Chama Cha Mapinduzi.
“Kwa hiyo kwa haraka haraka unapata majibu hiyo maana yake nini na
huko mbele katiba hiyo inasema kama hujapata hiyo asilimia 10 basi upate
viti vingi kwenye baraza la wawakilishi, lakini katika uchaguzi huu
viti vyote vimechukuliwa an CCM. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mtungi
alipoulizwa kuhusu maoni yake kama kwa matokeo hayo nini hatima ya
Serikali ya Umoja wa Kitaifa alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo.
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar, Awadhi Said,
alisema suala la uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni la kikatiba na
kwamba muundo na uwepo wake umeidhinishwa kikatiba. Akizungumza jana
kwa simu, alisema katiba inatamka wazi matakwa ya atakayekuwa Makamo wa
Kwanza wa Rais lazima apate asilimia 10 ya kura za urais na huo ndiyo
msingi wa awali na sio kusubiri busara ya Rais.
Muundo wa SUK Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) imetamkwa katika
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Toleo la 2010 Kifungu cha 9(3). Kifungu
hicho kinasema “ Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa
Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake, utafanywa katika utaratibu
utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia
demokrasia”. Katiba hiyo ilianzisha cheo cha Makamu wa Kwanza wa Rais na
Makamu wa Pili na kufuta wadhifa wa Waziri Kiongozi.
Kwa mujibu wa Marekebisho ya 10 ya Katiba, Makamo wa Kwanza wa Rais
atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama cha siasa kilichopata
nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa Rais.
Kifungu cha 39(3) cha Katiba hiyo kinasema kuwa Makamo wa Kwanza wa
Rais atatakiwa awe na sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa
Baraza la Wawakilishi ; na atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na
chama kilichopata nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa
Rais, kama chama hicho kilichopata nafasi ya pili katika matokeo ya kura
ya uchaguzi wa Rais, kitapata asilimia kumi ya kura zote za uchaguzi wa
rais.
Katiba hiyo inasema Makamu wa Pili wa Rais atateuliwa na Rais kutoka
miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka katika chama cha
siasa anachotoka Rais.
Chanzo HabariLeo
Monday, 21 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment