Aliyekuwa Murugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhard Tito
(kushoto) na wenzake, Kanji Mwinyijuma na Emmanuel Masawe wakiwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.
MABOSI watatu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania
(RAHCO), wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi
mabaya ya madaraka na kuisababisha serikali hasara ya dola 527, 540 za
Marekani.
Washitakiwa hao waliosimamishwa kazi na Rais John Magufuli mwishoni
mwa mwaka jana, walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba na kusomewa mashitaka manane.
Wakili wa Serikali, Thimos Vitalis aliwataja washitakiwa hao kuwa ni
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Mhandisi Benhard Tito, Raia
wa Kenya anayedaiwa kuwa dalali wa zabuni, Kanji Mwinyijuma na aliyekuwa
Katibu wa kampuni hiyo, Emmanuel Massawe.
Akisoma mashitaka, Wakili Vitallis alidai kuwa kati ya Septemba mosi
2014 na Septemba 30, 2015, Dar es Salaam, washitakiwa kwa pamoja
walikula njama ya kutenda kosa. Vitalisi alidai katika mashitaka
yanayomkabili Tito, Februari 27, mwaka jana katika ofisi za kampuini
hiyo zilizopo Ilala Dar es Salaam, alitumia vibaya madaraka baada ya
kuidhinisha kampuni ya Rothschild (South Africa) Property kuwa mshauri
katika mpango wa ujenzi wa Reli ya Kati, bila kuidhinishwa na Bodi ya
Zabuni ya Kampuni hiyo.
Alidai Machi 12, mwaka jana katika ofisi za Rahco, Tito na Massawe
walisaini barua ya kuikubali kampuni ya Rothschild (South Africa)
Property kutoa huduma ya ushauri wa kifedha katika ujenzi wa Reli ya
Kati bila kuidhinishwa na bodi.
Aidha, wanadaiwa kati ya Machi 12 na Mei 20, mwaka jana wakiwa
ofisini kwao, waliacha majukumu yao kwa kushindwa kuwasilisha mkataba wa
Kampuni ya Rothschild kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Wanadaiwa pia Mei 20, walitumia madaraka yao vibaya kwa kusaini
mkataba na kuingia makubaliano na kampuni hiyo katika masuala ya
ushauri. Katika mashitaka mengine, inadaiwa kati ya Mei 20 na Juni 20,
mwaka jana, walishindwa kuwasilisha nakala za mkataba wa makubaliano wa
kampuni hiyo na kampuni ya Rahco, kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
Mkaguzi wa ndani na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wakili Vitalis alidai kati ya Machi Mosi na Septemba 30, mwaka jana
kwa pamoja walikubaliana kuidhinisha makubaliano ya kampuni hiyo katika
masuala ya kiushauri na kusababishia kampuni hasara ya dola za
Kimarekani 527, 540, ambazo zilishalipwa kiwango cha awali benki.
Aliendelea kudai kuwa Agosti 18, mwaka jana, Tito alitumia madaraka
yake vibaya kwa kutoa zabuni ya upendeleo kwa kampuni ya Ujenzi wa Reli
ya China Construction Corporation. Inadaiwa katika zabuni hiyo, kampuni
ilipewe kazi ya ujenzi wa reli ya kilometa mbili yenye kiwango cha
kisasa kuanzia Soga ikiwa na thamani ya dola za Marekani 2, 312, 229.39
bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya Reli.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu mashitaka yao kwa kuwa mahakama hiyo
haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo na upande wa jamhuri ulidai
upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Washitakiwa walirudishwa rumande
na Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, mwaka huu kwa ajili
ya kutoa uamuzi kama washitakiwa watapewa dhamana.
Chanzo HabariLeo.
Monday, 14 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment