Askari
wa Kikosi cha Zimamoto, Manispaa ya Shinyanga wamenusurika kipigo
kutoka kwa wananchi wa mtaa wa Banduka, kata ya Ndala mjini hapa, baada
ya kuchelewa kufika kwenye tukio la nyumba kuungua moto ikiwa na watoto
ndani yake.
Baadhi
ya mashuhuda walidai kuwa moto huo ulianza kuwaka kwenye nyumba ya
Azizi Abdallah, saa 2:00 asubuhi na uliunguza baadhi ya vitu kwenye
nyumba hiyo ambayo wanaishi wapangaji pekee kwa kile kinachosadikiwa
kuwa ni hitilafu ya umeme ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.
Mmoja
wa walioshuhudia, Onesmo Shija, alisema wapangaji wote walikuwa
wamekwenda makazini na kubaki watoto ambapo saa 2:00 aliona moshi
ukifuka kwenye madirisha huku watoto wakipiga kelele, ndipo
walipokusanyika na kuanza kuuzima na kuwanusuru kifo watoto hao.
Shija
alisema baada ya wananchi kutoa taarifa mapema kwa kikosi hicho,
walichelewa kufika na walipofika tayari moto ulikuwa umeshazimwa ndipo
wananchi walipopandwa hasira na kuanza kuokota mawe na kuwashambulia
lakini mwenyekiti wa mtaa aliwazuia.
Mwenyekiti
wa mtaa huo, Terege Nyankangara alisikitishwa na kikosi cha Zimamoto
kuchelewa kufika eneo la tukio na kueleza uchelewaji huo ulitaka
kuhatarisha amani. Hata hivyo, Nyankangara aliwaasa wananchi wake kuacha
tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Askari
wa kikosi cha Zimamoto, Omari Magea alikiri wananchi hao kutaka
kuwashambulia kwa mawe na alishukuru Mwenyekiti wa mtaa kuwezesha
kurejesha amani. Alisema kilichowachelewesha ni uhaba wa vitendea kazi.
Aidha
msimamizi wa nyumba hiyo, Daudi Nyanda alisema nyumba hiyo wanaishi
wapangaji 10 na hakuna aliyepata madhara zaidi ya mali zao kuteketea.
Alisema thamani bado haijafahamika.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment