Waziri wa Habari, Vijana na Michezo Nape Nnauye akionesha gezeti la Habarileo kuwa ni gazeti makini. |
KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali, Tanzania Standard Newspapers (TSN) Limited imepongezwa kwa hatua ya kuzingatia weledi na kiwango cha juu cha taaluma wakati wa uchapishaji wa habari.
Pongezi hizo zilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati wa kikao cha kutambuana baina ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
TSN ni wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo. Waziri Nape alisema magazeti yanayochapishwa na TSN yamekuwa yakichapisha habari bila upendeleo, huku habari zake zikitoa nafasi kwa pande husika kutoa maoni, akisema ni taasisi ya habari inayopaswa kuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine.
Miongoni mwa watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao walitoa maelezo kuhusiana na taasisi zao mbele ya wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge ni pamoja na TSN, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TASUBA), Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Kampuni ya Filamu Tanzania.
“Kampuni hii inachapisha magazeti ambayo yanatakiwa kuwa mfano kwa magazeti mengine. Uandikaji wa habari unazingatia utoaji nafasi kwa pande zote, lakini pia ukizingatia kiwango cha juu cha taaluma ya habari,” Waziri Nape alisisitiza.
Alisema mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo katika kuboresha kampuni hiyo ya Magazeti ya Serikali yatachukuliwa kwa uzito mkubwa ili kuweza kuimarisha uendeshaji wake, likiwemo pendekezo lilitolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) kuhusu kuufanyia mabadiliko Muundo wa Menejimenti yake ili kuongeza ufanisi.
Zitto na wajumbe wengine wa Kamati hiyo katika mapendekezo yao walitaka Menejimenti ya TSN kuongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) ambaye atasimamia masuala ya kibiashara na pia kuwa na Mkuu wa Habari atakayesimamia masuala ya habari.
Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (CCM) alishauri TSN kuihuisha Maktaba yake kwenda katika mfumo wa kidigitali ili kuwa chanzo cha mapato. Hata hivyo tayari TSN ipo katika mchakato wa kuibadili Maktaba yake kuwa katika mfumo huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alizishauri TSN na TBC kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ikiwa ni pamoja na kujikita katika kutangaza habari mpasuko ili kutanua wigo mpana wa kuvuta wasikilizaji na wasomaji na hivyo kujiongezea mapato.
Mbunge wa Urambo Mashariki, Margaret Sitta (CCM) alipongeza uchapishaji wa vijarida, akitolea mfano wa jarida la Academy ndani ya gazeti la Daily News na jarida la Elimika ndani ya HabariLeo, akisema vijarida hivyo vinatoa mchango mkubwa katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment