Raisi John Magufuli akifanyiwa uhakiki wa silaha na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Neema Laizer, Ikulu Dar es Salaam
jana ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda la kuhakikiwa silaha kwa wakazi wote wa jiji wanaomiliki silaha.
RAIS John Magufuli amekuwa mtu wa kwanza kutekeleza agizo la Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuhakiki silaha baada ya bunduki
zake mbili aina ya Shot gun na bastola kuhakikiwa nyumbani kwake Ikulu,
Dar es Salaam.
Uhakiki huo umefanywa na maofisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon
Sirro. Akizungumza baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Rais Magufuli
alimpongeza Makonda na Jeshi la Polisi kwa kuendesha uhakiki wa silaha,
na alitoa mwito kwa watu wote wanaomiliki silaha nchi nzima kuhakikisha
zinahakikiwa.
Makonda juzi alitoa miezi mitatu kwa wenye silaha kuhakiki silaha zao
na muda huo utamalizika Julai Mosi mwaka huu. Rais Magufuli pia
alilitaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na watu
wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ili kutokomeza kabisa vitendo
hivyo.
“Ni aibu kumuona askari Polisi mwenye silaha ananyang’anywa silaha,
ni aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi akunyang’anye silaha na
wewe una silaha?” Amehoji Rais Magufuli.
Naye Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna
Sirro alimshukuru Rais Magufuli kwa kuunga mkono kazi hiyo na alisema
Polisi imejipanga kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa mafanikio.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametaka pande zinazogombea kiti
cha Umeya katika Jiji la Dar es Salaam, kukamilisha mchakato wa kumpata
Meya katika uchaguzi uliopangwa kufanyika leo badala ya kuendelea
kulumbana.
Dk Magufuli alisema upande wowote uwe tayari kupokea matokeo ya
uchaguzi huo ili Meya apatikane na Jiji liweze kuendelea na mipango yake
ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo.
“Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini
mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio demokrasia
ya kweli,” aliongeza Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mwandishi Wetu, Flora Mwakasala anaripoti kuwa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali ombi la kuzuia uchaguzi
wa umeya na unaibu meya wa Jiji la Dar es Salaam unaotarajiwa kufanyika
leo, na kuamuru uchaguzi huo ufanyike kama ulivyopangwa.
Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, kwa kuwa
Mahakama imeona hakuna sababu zozote za msingi zilizowasilishwa na
walalamikaji kuzuia uchaguzi huo.
Maombi ya kuzuia uchaguzi huo yaliwasilishwa jana mchana na Suzan
Massawe na Kumjhi Mohammed kupitia kwa Wakili wao Elias Nawela dhidi ya
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Katika maombi yao, waliiomba Mahakama itoe zuio la kufanyika uchaguzi
huo pia iamuru hali ibaki kama ilivyo hadi kesi ya msingi
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi, kwa kuwa walalamikaji katika kesi
hiyo, hawajapewa haki yao ya kualikwa kushiriki katika uchaguzi huo.
Akisoma uamuzi huo, Hakimu Lema alisema Mahakama haioni sababu za
msingi zilizowasilishwa na walalamikaji kuzuia kufanyika kwa uchaguzi
huo pia hawajaleta uthibitisho kama wao siyo miongoni mwa wapiga kura.
Aidha alisema, kulikuwa na kasoro nyingi ikiwemo kukosekana kwa
orodha inayoonesha majina ya wapiga kura, jambo lililosababisha Mahakama
kutokujua kama waleta maombi ni miongoni mwa wapiga kura.
Chanzo habarileo.
Monday, 21 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment