Raisi John Magufuli akiwasalimia waumini huku akisikilizwa na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri, Dk Alex Malasusa na Mchungaji Charles Mzinga baada ya
Ibada ya Pasaka katika kanisa la KKKT Azania Front jijini Dar es saalam.
RAIS John Magufuli amewataka Watanzania waendeleze upendo na
mshikamano walionao ili kuendelea kuilinda amani ya nchi na wasibaguane.
Akizungumza wakati wa Ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Azania Front, Dar es Salaam
jana, Rais Magufuli alisema Watanzania wanapaswa kutokubaguana kwa dini,
rangi wala makabila na washirikiane katika umoja wao.
Rais Magufuli alisema wakati taifa likiadhimisha sikukuu hiyo ya
kufufuka kwa Yesu Kristo, wananchi wanapaswa kusherehekea kwa kufanya
kazi ili taifa lisonge mbele.
“Niwaombe Watanzania wenzangu wakati tunaadhimisha Sikukuu hii ya
kumbukumbu ya kufufuka kwa Yesu Kristo tufufuke naye katika upendo wake
lakini tufanye kazi kweli kweli kwa sababu vitabu vinasema asiyefanya
kazi na asile,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, alisema endapo Watanzania kwa umoja wao wakiamua kufanya kazi
kwa bidii, Taifa halitakuwa masikini na kuacha kutegemea misaada ya
wahisani wa nje. Alisema kuwa Tanzania ni nchi iliyojaaliwa neema kwa
kuwa na rasilimali nyingi na hivyo wananchi wanatakiwa kusimama imara
ili iweze kuja kuwa Taifa litakalokuwa likitoa misaada kwa mataifa
mengine ya nje.
Rais Magufuli aliwaomba Watanzania kutochoka kuliombea Taifa pamoja
na yeye ambaye ana jukumu gumu na zito lakini kupitia maombi ya wananchi
anaamini atatimiza yale aliyotakiwa kuyatimiza.
“Naomba Watanzania tusichoke kuliombea Taifa letu, na mimi
nawashukuru kwa kuendelea kuniombea. Jukumu hili ni gumu, zito na ni
msalaba lakini najua kwa sala zenu, kwa maombi yenu nitatimiza yale
ninayotakiwa kuyatimiza,” alieleza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani,
Dk Alex Malasusa aliyeongoza ibada hiyo, aliwakumbusha wananchi
kurejesha maadili ndani ya nyumba zao yaliyoanza kupotea kwa kumrudia
Mungu.
Askofu Malasusa alisema kuwa fmilia nyingi siku hizi zimeparaganyika,
ndoa nyingi zimekuwa hazidumu kwa sababu watu wameacha kufanya ibada na
hivyo maadili tena katika nyumba yamepotea. “Tufufue maisha ya uadilifu
ndani ya ndoa zetu.
Siku hizi baba na mama wanazikimbia nyumba zao kwa sababu maadili
yamepotea ndani ya nyumba, turudishe maadili kwa kufanya ibada,” alisema
Dk Malasusa. Aidha, Askofu Malasusa aliwataka Watanzania kwa imani zao
kuacha kumsifu Rais Magufuli kwa kupiga makofi na badala yake kila mmoja
kwa imani yake asimame na kumuombea kwa kuwa sasa taifa limeanza kuwa
na matumaini mapya na nuru kwa kumpata kiongozi aliye mwadilifu.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 27 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment