Serikali
imetenga jumla ya Sh bilioni 811 zitakazotumika kutekeleza ahadi ya
Rais John Magufuli ya kukipatia kila kijiji Sh milioni 50 kwa ajili ya
shughuli za maendeleo.
Imeelezwa
kwamba serikali imeshaanza kushirikisha wadau mbalimbali kupata maoni
ya jinsi ya kuendesha mpango huo kwa ufanisi na tija.
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) alisema
serikali itaanza kutoa fedha hizo kuanzia mwaka wa fedha ujao.
Alikuwa
akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki baada ya mkutano
wa wadau waliokuwa wanajadili rasimu ya mpango huo wa utoaji fedha kwa
ajili ya maendeleo.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa halmashauri za wilaya, Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), mabenki, mifuko ya
hifadhi ya jamii na vikundi mbalimbali.
“Kwa kuanzia, fedha hizo zitatolewa kwa awamu tatu katika kipindi cha miaka mitano,” alisema.
Alisema
fedha hizo zitatolewa kupitia benki kabla ya kutolewa kwa vikundi
mbalimbali kama Vicoba, Saccos na vikundi vingine kulingana na taratibu
zitakazowekwa.
Alisema
mpango utaanza na mikoa 10 iliyo nyuma katika kutumia huduma za kifedha
kwa kuzingatia taarifa ya utafiti ya Finscope ya mwaka 2013.
Mikoa hiyo ni Singida, Lindi, Mtwara, Mbeya, Shinyanga, Geita, Kagera, Dodoma, Rukwa na Ruvuma.
Akifungua
mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uhusiano ya
Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema mkutano
huo ulilenga kupata maoni ya wataalamu ya namna bora ya kuutekeleza.
Akizungumza
kwa niaba ya Waziri, Kaimu Mkurugenzi, Maendeleo ya Sekta Binafsi,
Uwekezaji na Uwezeshaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Victor Mwainyekule
alisema mawazo yaliyopatikana yatazingatiwa kuboresha mpango huo
unaolenga kupambana na umaskini.
Mkuu
wa Uendeshaji, Benki ya Wanawake (TwB), Zablon Yebete alisema mpango
huo ni uwekezaji mkubwa kwa Watanzania unaopaswa kuungwa mkono na vyombo
vya fedha na wadau wengine nchini.
“Tunatakiwa kuunga mkono mpango huu unaohusisha vyombo vya fedha katika utekelezaji wake kwa faida ya taifa,” alisema.
Kwa mujibu wa mpango huo, walengwa watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali kabla ya kupatiwa fedha hizo.
Credit;Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment