Rais John Magufuli akimuapisha Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. | RAIS John Magufuli amewaapisha wakuu wa mikoa aliowateua hivi
karibuni kwa ‘kuwatwisha’ majukumu mazito ambayo amewaambia ilimradi
wameyakubali na kusaini, wameingia kwenye mtego. Magufuli ambaye baada ya kuwaapisha alitoa hotuba; utaratibu ambao haukuzoeleka, miongoni mwa majukumu aliyowataka wakayatekeleze ni pamoja na kukabili tatizo la wafanyakazi hewa kwa kutoa siku 15 kwa halmashauri na taasisi zote za serikali kuhakikisha wanawaondoa. Majukumu mengine waliyopewa, ni kukabili ujambazi hususan wakuu wa mikoa ambayo imekuwa ikikabiliwa na tatizo la utekaji magari kiasi cha serikali kuamua kuweka utaratibu wa polisi kuyasindikiza. Aidha, wametakiwa kukabili watu wazembe, watendaji wanaowanyanyasa wananchi, njaa, kodi za mazao, migogoro ya ardhi na kuhakikisha wanasimamia na kufanikisha mpango wa elimu bure. Aidha, katika hotuba yake ametoboa siri ya kuchelewa kufanya uteuzi kwa kusema alitumia muda mwingi kujiridhisha kwanza kama watu atakaowateua watamudu kazi hiyo wanayokwenda kuifanya. Katika hotuba hiyo ambayo aliwaambia wakuu hao wa mikoa kazi yao si kutangaza siasa, aliwasisitiza wawajibike na wamwakilishe vyema kutatua kero za wananchi ambao alisema wanakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo mateso na manyanyaso. Ni Mtego Alisema ameamua kuwateua wakuu hao wa mikoa kwa sababu anaamini watamuwakilisha vizuri watakapokuwa kwenye mikoa hiyo na kuwaomba watakaporipoti kwenye vituo vyao, kwa kuwa wao ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye mikoa hiyo, wakatimize wajibu wao bila kuogopa. “Sikutarajia kuzungumza chochote kwa sababu mara nyingi ni kawaida ukishaapisha mnaondoka lakini nimeona…,” alisema na kuwapongeza huku akiwataka wamsamehe kwa kuwa kabla ya uteuzi hakuwauliza. “Kwa bahati mbaya sikuwauliza, hilo ndilo mnaweza mkanisamehe,” alisema. “Nilitegemea wengine mngekataa kuja kuapishwa. Lakini kwa sababu mmekubali na kusaini, mmeshaingia kwenye mtego wa kufanya kazi. Nawapa pole kwa sababu mnakwenda kufanya kazi,” aliwaambia. Aliwataka wakasimamie ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwasisitiza kwamba, haiwezekani Waziri Mkuu, Mawaziri, Makamu wa Rais au yeye, afike kwenye maeneo yao na kukuta kero inajulikana wakati mkuu wa mkoa yupo. Alisema ikitokea hivyo, itadhihirisha kwamba ameshindwa kufanya kazi. Ujambazi, utekaji magari Akiwasisitiza kuwajibika, alisema ameona awaambie hayo tangu mwanzo wafahamu kwamba wanakwenda kutatua kero za wananchi. Alitoa mfano wa maeneo ya mipakani na kusema, pamekuwa na mazoea ya magari ya abiria kusindikizwa na polisi kutokana na hofu ya majambazi. Alisema kitendo cha kusindikizwa na polisi maana yake ni kwamba, hakuna usalama. Alisema ndiyo maana aliteua watu wenye uzoefu na masuala ya ulinzi ili sasa mikoa hiyo wananchi wasiendelee kusindikizwa na polisi na watembee kwa usalama. “Ukienda Kagera, kama ni msafiri wa basi lazima usindikizwe na polisi. Geita hivyo hivyo, Katavi hivyo hivyo, Kigoma hivyo hivyo, haiwezekani nchi ambayo imejitawala kwa miaka 50, raia wanaposafiri lazima wasindikizwe na polisi,” alisema. Alisisitiza, “Nimeteua viongozi watakaosimamia watu wasiendelee kusindikizwa na polisi. Watu watembee katika nchi yao wakiwa salama Nitashangaa sana Meja Jenerali, Mustafa Kijuu uliyekuwa ukishughulikia masuala ya ulinzi nchi nzima, ukashindwa kusimamia mkoa wa Kagera na watu wakakaa bila amani. Najua uwezo huo unao.” Aliwataka wasimamie suala hilo ipasavyo Tanzania iwe na amani na wananchi wake, watafanyakazi vizuri. Makambi ya wavivu Aliwataka wakuu wa mikoa kusimamia maeneo yao kuhakikisha watu hususan vijana, wanafanya kazi. “Haiwezekani katika nchi hii kijana unamkuta anacheza pool saa mbili, saa tatu halafu walio mashambani ni wazee na akinamama. Watanzania wafanye kazi, kama hawawezi kufanya kazi kwa kuambiwa, wafanye kazi kwa lazima,” aliwaambia. Alisema endapo wamezoea kila siku ni kucheza, wakamatwe na kupelekwa kwenye makambi wakafanye kazi kwa nguvu kwani wakitoka huko watatambua umuhimu wa kufanya kazi. “Asiyefanya kazi na asile.” Dk Magufuli alisema anataka Tanzania katika awamu yake, asitokee mkuu wa mkoa au wilaya akaomba chakula cha msaada kwa ajili ya wananchi. Alisema kitendo cha mkuu wa mkoa kujiwahi kwenye vyombo vya habari akitaka chakula cha msaada, itadhihirisha kwamba wapo watu kwenye eneo lake ambao hawakusimamiwa vizuri. Uozo wa halmashauri Rais Magufuli ambaye alisema hakuna mahali ambako kuna uozo kama ilivyo kwenye halmashauri, aliwataka wakuu wa mikoa wazisimamie ipasavyo ikiwemo kukabili wimbi la wafanyakazi hewa. Alitoa mfano kwamba wapo watu waliotumwa Februari mwaka huu kufanya utafiti katika mkoa wa Singida na Dodoma ambako wamebaini kati ya wafanyakazi 26,900 waliolipwa mishahara Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu, kwenye halmashauri 14, wafanyakazi 202 ni hewa. Alichanganua wafanyakazi hewa hao waliokuwa wakilipwa mshahara na kusema, walioacha kazi walikuwa sita, waliofariki na kufungwa 27, waliofukuzwa wanane, wastaafu 158 na wenye likizo bila malipo watatu. Aidha, alisema wafanyakazi 3,500 hawakufanyiwa mchakato huo kwa sababu wengine walikuwa na ruhusa, masomoni, wanaumwa na wengine ni watoro. Alisema ikichukuliwa idadi ya halmashauri 180 zilizoko nchini na kufanya hesabu kwa kuzingatia hali hiyo ya halmashauri za Dodoma na Singida zilizofanyiwa utafiti, inamaanisha nchi imekuwa ikipoteza mapato ya takribani Sh bilioni 1.5 kwa mwezi. Wafanyakazi hewa “Sasa niwaombe ndugu zangu wakuu wa mikoa, najua mtakwenda kuwapa maagizo wakurugenzi na wakuu wa wilaya. Lakini niwape muda, ndani ya siku 15, wawe wamejumulisha wafanyakazi wote, wamewatoa wafanyakazi hewa,” aliwaagiza. Rais Magufuli alisema mshahara ujao, ikigundulika kuwapo wafanyakazi hewa kwenye orodha ya malipo, mkurugenzi husika ajihesabu hana kazi na atafikishwa mahakamani. Vile vile amewaambia mawaziri, hususan Waziri wa Fedha na Mipango aliyekuwapo kwenye hafla hiyo, wakawaeleze watendaji kwenye wizara zao na taasisi mbalimbali wahakikishe wanawaondoa wafanyakazi hewa ndani ya siku 15 na wasipotimiza agizo hilo hatua zitakuwa ni zilezile kwani sheria ni msumeno. Alisema inasikitisha kuona fedha zinazokusanywa haziendi kwenye miradi inayopangwa, badala yake sehemu kubwa inatumika kulipa mishahara ikiwemo hewa. Alisema kwa ujumla Serikali inalipa mishahara kila mwezi kwa watumishi wake wa umma jumla ya Sh bilioni 549 mpaka bilioni 550. “Lakini kwa hali ilivyo fedha nyingi zinaishia kwenye mishahara feki. Nawapa Ma-RC siku 15 mhakikishe Wakurugenzi wa halmashauri zote wamejumlisha idadi ya wafanyakazi wote waliopo na kuondoa wafanyakazi hewa katika halmashauri zao,” alisisitiza Rais Magufuli. Elimu bure Akiwasisitiza kusimamia mpango wa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, Rais Magufuli aliwataka wakuu wa mikoa kusimamia upatikanaji wa madawati na majengo. Alisema kumekuwapo na mwitikio mkubwa wa wazazi kupeleka watoto wao shule hali inayodhihirisha awali, hawakupelekwa kwa sababu ya michango yenye kero. Aliwataka wawe watumishi wa wananchi wakitambua kwamba Watanzania wanapata shida na wana mateso makubwa. Uteuzi kuchelewa Akieleza imani yake kwao kwamba watatekeleza majukumu hayo, Rais Magufuli alisema alichelewa kufanya uteuzi kutokana na kujiridhisha kwanza kama wahusika watamudu kazi hiyo wanayokwenda kuifanya. “…Ndiyo maana nilichelewa kuteua, nilikuwa nauliza…, siku nyingine unamfuta, siku nyingine unamrudisha, siku nyingine unakuta dhambi zake ni kidogo unajaribu kusamehe, sasa niwaombe mkafanye kazi,” alisema. Hamuendi kutangaza siasa Aliendelea kuwafunda akiwaambia hawaendi kutangaza siasa bali kutimizia wajibu. Aliwapa moyo kwamba akisema wapo watakaowalaumu lakini wanapaswa kuchapa kazi. “Wapo watakaowalaumu, ninyi chapeni kazi, msituangushe, ” alisema. Alisema katika uchaguzi, aliahidi mengi lakini anawaamini wakuu hao wa mikoa watatimiza wajibu wao na kutumia fursa zilizopo kwenye mikoa hiyo na kuwanufaisha wananchi. Aliwahimiza kuzingatia utawala wa sheria utakaowezesha wananchi kufuata sheria bila shurti. Alisema nchi ina fursa nyingi ambazo iwapo kila mkoa utaamua kuzisimamia, vijana wengi watapata ajira. Watendaji wanyanyasaji Rais Magufuli alikemea unyanyasaji unaofanywa na viongozi na watendaji dhidi ya wananchi akitolea mfano wa maofisa watendaji na makatibu tarafa na kuwapa ‘rungu’ wakuu wa mikoa kuwaweka ndani viongozi wa aina hiyo. “Watu wananyanyaswa, mtendaji wa kata au tarafa ananyanyasa watu wa chini, mkiona hali hii nawaruhusu sasa hivi mna fursa ya kumuweka ndani mtu kwa saa 48 wekeni hawa ndani, hata kama itakuwa ni kosa tutajua huko mbele, msiogope kuchukua maamuzi nitawalinda,” alisema na kutaja eneo lingine ambalo watu wamekuwa wakinyanyaswa ni pamoja na hospitalini. Migogoro wafugaji, wakulima Kuhusu eneo la matatizo ya migogoro ya ardhi, alisema Morogoro kuna migogoro mingi watu wanakufa na kusisitiza kuwa hayo ndio maeneo ya kufanyiwa kazi na endapo matatizo hayo yataendelea, viongozi wa maeneo hayo watawajibishwa. “Si mnaona kulichotokea kwa RC wa Morogoro haya sasa message sent.” Ujambazi Aliwataka wakuu hao wa mikoa kusimama kidete na kuhakikisha wanapambana na tatizo hilo hadi pale litakapomalizika na kusisitiza kuwa jitihada hizo zinawezekana. “Kwanini ujambazi hapa kwetu Tanzania usiishe? Mbona Rwanda hakuna ujambazi? Nawaomba mkajipange na muwaambie kabisa majambazi kuwa tayari mmeshajipanga,” alisisitiza. Vietnam Aliendelea kukumbushia kuhusu jitihada za nchi ya Vietnam katika kupambana na umasikini na sasa nchi hiyo imefanikiwa kujiinua kiuchumi wakati ni moja ya nchi zilizopambana katika vita kwa muda mrefu. “Hawa walichukua mbegu ya korosho, samaki na kahawa nchini kwetu, lakini leo hii ndio wanaongoza kwa kuzalisha korosho, sisi kule Mtwara uzalishaji unazidi kushuka tu. Bodi zilizopo kule ni za ajabu, wananchi wanadhulumiwa, jamani lazima tubadilike,” alisema. Alisema wakuu hao wa mikoa ndio wenye fursa nzuri ya kuibadilisha Tanzania kwa kuwasimamia ipasavyo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na makatibu tarafa. “Najua kwa sasa kwa vile ndio tunaanza wataumia kidogo lakini baadaye watashukuru. Mabadiliko siku zote mwanzo wake huwa mgumu.” Chnza HabariLeo. |
Tuesday, 15 March 2016
Tagged Under:
Ma RC mtegoni
By:
Unknown
On: 22:17
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment