Friday, 11 March 2016

Tagged Under:

Rais Magufuli Kuzindua Ujenzi wa Mitambo Ya Umeme Wa Gesi Ya Kinyerezi II Wiki Ijayo....Mitambo hiyo Itazalisha Megawati 240 Kutokana na Gesi Yetu Asilia

By: Unknown On: 21:15
  • Share The Gag

  • Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ataweka jiwe la msingi katika ujenzi wa  kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi II chenye uwezo wa kuzalisha megawati 240 unaotokana na gesi asilia iliyogundulika nchini.

    Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam , Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo alisema Rais Dkt Magufuli anatarajiwa kuweka jiwe la msingi wiki ijayo  machi 16, na ujenzi wa mradi huo umeanza  mwezi Machi mwaka huu na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 28.

    Prof. Muhongo alifafanua kuwa mwanzoni mwaka 2018 ,kituo cha Kinyerezi II kitaanza kuzalisha umeme wa megawati 240 ambapo kati ya hizo megawati 180 zitatokana na Gesi asilia na megawati 60 zitatokana umeme utakaozalishwa kutokana na joto litakalotokana na kuendesha mitambo ya kituo hicho.

    ” Mtambo huu ni wa kisasa zaidi kwani hakuna kitakachopotea, lile joto litakalokuwa linatoka kutokana na kuendehsa mashine litazalisha umeme , tofauti na ilivyokuwa kwa Kinyerezi I ambapo joto hupotea bure,” alisema  Profesa Muhongo.

    Alisema kuwa kituo hicho kitagharimu Dolla za Kimarekani milioni 344 hadi kukamilika kwake na tayari Mkandarasi  atakayejenga kituo hicho amekwisha lipwa fedha zake ambazo ni fedha kutoka Serikali ya Tanzania na mkopo  wa bei nafuu kutoa Serikali ya Japan.

    Pia Profesa Muhongo alitumia ziara hiyo kuuleza umma kuwa  kwa sasa Serikali inaondokana na miktaba ya malipo ya ziada ya mtaji  kwa kampuni zinazoiuzia umeme (TANESCO) ( Capercity charge)

    Sambamba na hilo alisema kuwa kinachofanyika sasa ni kupitia upya mikataba iliyopo na kufanya mazungumzo na kampuni husika ili kuondoa gharama zisizo za lazima.

    Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la umeme nchini (TANESCO) Mhandisi Felchesim Mramba alisema mwishoni mwa mwezi huu kituo cha umeme cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi I kitaongeza uzalishaji wa umeme wa megawati 80 na hivyo kufanya kituo hicho kuzalisha jumla ya megawati 150 kama inavyokusudiwa.

    Mramba aliongeza kuwa  mwanzoni mwa mwezi April, Mkoa wa Dar es salaam  utakuwa unapata umeme moja kwa moja kutoka Kinyerezi I tofauti na ilivyokuwa hapo awali ilikuwa ikitegemea kupata umeme kutoka kituo cha ubungo pekee.

    Mramba alisema kukamilika kwa kiasi hicho cha umeme kutapunguza kabisa tatizo la kukakatika umeme mara kwa mara nchini.

    Katika ziara hiyo Profesa Muhongo alitembelea Kituo cha umeme cha City Center pamoja na cha Mikocheni ambavyo vitaliwezesha jiji la Dar es salaam kuondokana na nyaya za umeme zinazopita juu.

    Akifafanua mbele ya  waziri Mhongo, meneja mwandamizi wa miradi ya usafirishaji na usambazaji Mhandisi Gregory Chegere, alisema miundombinu ya umeme  katika kituo hicho itapita chini ya ardhi na hivyo kuondoa adha ya kukata miti pamoja na kuangushwa kwa nguzo kutokana na mvua zitakazokuwa zinanyesha kwa jiji la Dar Es Salaam.

    Mhandisi Chegere alisema kituo hicho kitaanza kazi mwezi April na kuuwezesha Mkoa wa Dar es salaam kuwa na umeme wa uhakika na usiokatika.
    Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akipata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa mitambo hiyo.
    Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akiendelea na ukaguzi wa mitambo ya Kinyerezi II  jijini Dar es salaam.
     
    Credit;Mpekuzi blog

    0 comments:

    Post a Comment