Spika wa Bunge, Job Ndugai.
WABUNGE na wanasiasa wametaka Bunge lichunguzwe kutokana na tuhuma
kwamba baadhi ya wabunge wakiwamo wenyeviti wa baadhi ya Kamati za
Kudumu za Bunge, wanahusishwa na upokeaji wa rushwa. Juzi Spika wa
Bunge, Job Ndugai alitangaza kufanya mabadiliko ya wajumbe 27 wa Kamati
za Kudumu za Bunge yaliyowang’oa wenyeviti watano.
Hata hivyo, Ofisi ya Bunge imesisisiza kuwa mabadiliko hayo,
hayajatokana na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya kamati hizo kama
inavyozushwa. Badala yake imesema ni ya kawaida na kwamba katika
mabadiliko, Spika hakuainisha dosari zozote katika utendaji wa kamati
hizo za Kudumu za Bunge.
Hata hivyo, licha ya kauli hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Maendeleo na Huduma za Jamii jana ilishindwa kufanya vikao vyake baada
ya wajumbe wengi kuingia mtini, kwa madai wanataka Spika atoe muongozo
kuhusu kujiuzulu kwa wenzao wawili waliofanya hivyo kutokana na uwepo wa
tuhuma za rushwa zinazoigusa kamati hiyo.
Kutokana na hilo, wabunge wametaka kufanyike uchunguzi ili kama kuna
wabunge waliokula rushwa wajulikane na kama hakuna, basi chombo cha
habari kilichoandika kuhusu madai hayo kichukuliwe hatua. Ratiba ya jana
ya kamati hiyo inayokutana Dar es Salaam ilikuwa ikutane na wizara tatu
za Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Elimu, Teknolojia
na Ufundi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Kukutana kwa wizara hizo, kulitokana na maagizo ya awali yaliyotolewa
wiki iliyopita kwenye kamati hiyo na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Dk
Raphael Chegeni kwamba wizara hizo tatu zikutane na kamati kwa pamoja
ili kila mmoja aeleze majukumu na mipaka yake kwa lengo la kuondoa utata
uliopo baina yao.
Hata hivyo, hiyo jana baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiwemo Dk
Ely Macha, Susan Lyimo, Juma Nkamia, Kasuku Bilago na Lucy Mlowe
walifika kwenye ukumbi wa kikao hicho cha kamati na kuwakuta baadhi ya
watumishi wa Bunge wa kamati hiyo ila kikao hakikuwepo.
Lyimo alisema kikao hakijafanyika kwa sababu ya baadhi ya wenzao
kujiuzulu akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto aliyemuandikia
Spika barua ya kujiuzulu kwake nafasi ya ujumbe ndani ya kamati hiyo ili
kupisha uchunguzi wa madai ya rushwa ndani ya kamati hiyo.
Aidha, Mjumbe mwingine aliyejiuzulu nafasi yake ni Mbunge wa Nzega
Mjini, Hussein Bashe. Akizungumzia hali hiyo, Lyimo alisema yeye na
baadhi ya wenzake walifika jana asubuhi kwenye ukumbi wa kikao ila
hakikufanyika na maelezo waliyopewa ni kutokana na kujiuzulu kwa wenzao
na hivyo wanasubiri amuongozo wa Spika. “Ni kweli tumekuja kwenye kikao
kama ratiba ilivyokuwa ila tumeona wenzetu wengi hawapo, tumekuja
wachache na hakuna kinachoendelea, tumeondoka hadi kesho(leo),” alisema
Lyimo.
Kwa upande wake, Bilago alisema ni kweli hawajakutana kutokana na
mambo mbalimbali yakiwemo tuhuma za rushwa zilizofanya baadhi ya wajumbe
kujiuzulu na wao wameomba uchunguzi ufanyike ili kubaini ukweli wake.
“Tumeomba uchunguzi ufanyike kama kweli wapo wajumbe waliokula rushwa
hatua zichukuliwe na kama madai hayo sio ya kweli, basi mwandishi na
vyombo husika vya habari vilivyoripoti tuhuma hizo vichukuliwe hatua,”
alisema Bilago.
Alisema pamoja na baadhi yao ndani ya kamati kujiuzulu kupisha
uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo, wao hawajajiuzulu ndio maana wameendelea
kuhudhuria vikao vya kamati hiyo na kwamba wanachokitaka wao ni
uchunguzi ufanyike ili ukweli uwekwe bayana.
Hoja ya wabunge hao iliungwa mkono na chama cha siasa cha ACT
Wazalendo ambacho kilimtaka Spika Ndugai kuitisha mara moja uchunguzi
kwa kamati zote zilizotuhumiwa ili ukweli ubainike na hatua za kisheria
zichukuliwe mara moja, kwani kuwahamisha kamati wabunge kamwe
hakutaondoa tatizo na kulirejeshea Bunge hadhi yake.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mwenyekiti,
Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa wa ACT Wazalendo, Yeremia Maganja
alisema ACT wamesikitishwa na uamuzi huo wa Spika kuwahamisha kamati
Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na wajumbe wa baadhi ya Kamati za Kudumu za
Bunge uliofanywa juzi. Maganza alisema kimsingi utamaduni huo unafifisha
mapambano dhidi ya rushwa na uwajibikaji kwa viongozi wa umma na
watendaji wa serikali.
Lakini taarifa ya Ofisi ya Bunge iliyotolewa jana na Kitengo cha
Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge kwa vyombo vya habari ilisema
msingi wa mabadiliko hayo umelenga kuzingatia mahitaji mapya na
changamoto zilizojitokeza baada ya kuundwa kwa kamati hizo Januari mwaka
huu na kwamba Spika alikuwa ameanza kufanyia kazi mabadiliko hayo tangu
mapema mwezi huu.
“Waheshimiwa wabunge wanaosakamwa kwa uvunjifu wa maadili kupitia
mitandao ya kijamii na magazeti, ni budi wakatendewa haki kwa sababu
Spika anazingatia sana utawala wa sheria. “Kama kuna mbunge yeyote
anayetuhumiwa kwa makosa ya jinai, mamlaka za kiuchunguzi zina wajibu wa
kutekeleza majukumu yao na pale inapobidi Bunge lenyewe kupitia Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inaweza kufanya uchunguzi kwa
Mamlaka ya Spika,” ilisema taarifa hiyo.
Awali, asubuhi akizungumza na kipindi cha Power Breakfast
kinachorushwa na redio ya Clouds FM Dar es Salaam, Spika Ndugai alisema
mpaka sasa hakuna mbunge yeyote anayechunguzwa kwa tuhuma za rushwa na
Bunge hilo, ingawa kuna uwezekano vyombo vya dola vikawa vinaendesha
uchunguzi kwa baadhi ya wabunge.
“Hakuna taarifa yoyote ya rushwa dhidi ya wabunge niliyonayo, hizo
taarifa za rushwa nimezisikia huko kwenye vyombo vya habari na
hazihusiani na mabadiliko haya ya wajumbe wa kamati,” alisisitiza
Ndugai. Imeandikwa na Halima Mlacha, Mroki Mroki na Oscar Mbuza.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 23 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment