Raisi wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Othman
Makungu wakati wa sherehe za kumuapisha rasmi kuwa Rais zilizofanyika
kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Unguja jana.
RAIS Ali Mohammed Shein ameapa kuiongoza tena Zanzibar huku akiahidi kuunda serikali itakayowaunganisha Wazanzibari wote.
Uundwaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ni jambo
linalosubiriwa kwa hamu na wananchi, kuona kama Dk Shein baada ya
kushinda kwa zaidi ya asilimia 90, ataunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hiyo ni kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) ambacho ni chama kikuu
cha upinzani, kususia uchaguzi wa marudio uliompa ushindi wa kishindo Dk
Shein kwa kile wanachodai kuwa hawawezi kushiriki uchaguzi haramu ambao
matokeo yake ni kubakwa kwa demokrasia.
Lakini Dk Shein wakati amemaliza kuapa na kusomewa dua na viongozi
mbalimbali wa dini kutoka madhehebu ya Kiislamu, Wakatoliki na Anglikana
kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja jana, aliwahakikishia Wazanzibari
kuwa ataendelea kuulinda umoja wao kwa kushirikiana na vyama vya
upinzani ili kuiletea Zanzibar maendeleo.
“Vyama vya upinzani vimenipa imani kubwa hasa kutokana na maelezo yao
waliyoyatoa siku ya kutangazwa matokeo, ujumbe wao ni wa kuijenga
Zanzibar na mimi naahidi kuwa nitashirikiana nao bila ubaguzi wowote,”
alisema Dk Shein anayeongoza muhula wake wa pili na wa mwisho kikatiba.
Alisema serikali atakayoiunda itaheshimu misingi ya utawala bora,
haki za binadamu na hivyo aliwaomba wananchi wamuunge mkono kwa kufanya
kazi ili wajiletee maendeleo kwa kuwa uchaguzi tayari umeshaisha.
“Uchaguzi umeisha, sasa tushirikiane wote kuijenga Zanzibar yetu,
kila mtu akafanye kazi maana kila mtu mchango wake ni muhimu kwa ustawi
wa nchi yetu,” alisema Dk Shein.
Pia alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kuitunza amani iliyopo huku
akionya kuwa serikali yake ile ya Muungano haitakuwa na uvumilivu kwa
mtu au kikundi kitakachojaribu kuvuruga amani iliyopo.
Hata hivyo, aliahidi kutoa mwelekeo wa Serikali yake atakapokuwa
anazindua Baraza la Mapinduzi Zanzibar hivi karibuni. Hali ilivyokuwa
Amaan Jina la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim
Jecha ndilo lililoshangiliwa kwa nguvu na wafuasi wa CCM waliofurika
kwenye Uwanja wa Amaan wakati wa shughuli ya kumwapisha Dk Shein.
Jecha aliyejitokeza akiwa kwenye jopo la watu mashuhuri ambao
waliitwa kwenda kwenye jukwaa maalumu, lililoandaliwa kwa ajili ya Rais
Mteule kuapa, alishangiliwa kwa nguvu wakati anashuka kwenda jukwaa
hilo.
Jopo hilo lilihusisha Spika wa Baraza la Wawakilishi, Katibu wa
Baraza la Wawakilishi, Katibu Kiongozi, viongozi wa dini pamoja na
viongozi wengine liliongozwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman
Makungu.
“Jecha, Jecha, Jecha,” wananchi waliimba jina hilo mara kwa mara
wakati anaenda kwenye jukwaa hilo na wakati wanarudi baada ya kumaliza
shughuli za kumwapisha Rais Shein. Jina la Jecha limekuwa maarufu baada
ya kutangaza kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.
Tangu atoe tangazo hilo, hawakuwahi kuonekana hadharani hadi juzi
alipojitokeza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa marudio.
Kufutwa kwa uchaguzi huo, kumefanya kuwepo na mpasuko mkubwa wa kisiasa
visiwani hapa baada ya CUF ambacho ni chama kikuu cha upinzani kutangaza
kususia kushiriki marudio ya uchaguzi uliofanyika Machi 20, 2016.
Maelfu ya watu walifurika katika uwanja wa Aman kushuhudia tukio hilo
la kihistoria, lakini kwa bahati mbaya zaidi wengi wa watu hawakupata
nafasi ya kuingia ndani na hivyo kulazimika kubaki nje na kusikiliza
sherehe hizo kupitia vipaza sauti vilivyofungwa uwanjani hapo.
Kikundi cha Culture kilikuwepo kutumbuiza sherehe hizo. Nyimbo zake
za ‘aliyepewa kapewa, hapokonyeki, hata ukifanya chuki unajisumbua’ na
ule wa ‘unaomba radhi ya nini wakati uliyokusudia hayakuwa’, zilipamba
sherehe hizo na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi.
Sherehe hizo pia zilipambwa na gwaride la vikosi vya Jeshi la Ulinzi
wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Kikosi Maalumu cha Kuzuia
Magendo (KMKM), Mafunzo na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).
Vikosi hivyo vilichora herufi ya A ambacho ni kifupi cha neno la
Kigiriki la Alfa, ambalo maana yake ni mwanzo. Kuapishwa kwa Dk Shein
jana ni mwanzo wa kuiongoza Zanzibar kwa muhula wa pili akiwa Rais wa
Awamu ya Saba ya Zanzibar.
Marais wengine waliowahi kuiongoza Zanzibar tangu Mapinduzi ya mwaka
1964 ni Abeid Amani Karume, Aboud Jumbe, Ali Hassan Mwinyi, Abdul Wakil,
Salmin Amour na Amani Abeid Karume.
Chanzo HabariLeo.
Thursday, 24 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment