Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi |
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za masika katika ukanda wa Pwani, zinazotarajiwa kuanza wiki hii, zitakuwepo kwa vipindi vifupi na zitakuwa kubwa zitakazoweza kusababisha mafuriko. Aidha, kwa wakati huo hali ya joto kali itaendelea kuwepo nyakati za usiku huku ikipungua nyakati za mchana.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi alisema hayo jana wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo na kueleza kuwa mvua za masika zimeanza kama ilivyotabiriwa huku ukanda wa Pwani zikianza wiki ya kwanza ya mwezi Aprili.
Dk Kijazi alisema ingawa maeneo hayo ikiwemo Jiji la Dar es Salaam, yanaonesha kuwepo mvua za wastani hadi chini ya wastani, lakini mabadiliko ya hali ya hewa yanafanya kuwepo vipindi vifupi vya mvua kubwa.
“Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo vipindi vifupi vya mvua kubwa wakati wa msimu huo wa masika na kuweza kusababisha hata mafuriko, ni vema wananchi kufuatilia utabiri wa hali ya hewa kwa vipindi vifupi,” alisema Dk Kijazi.
Alisema hali ya joto wakati huo wa mvua, inaonesha katika utabiri kupungua nyakati za mchana wenye kiwango cha juu cha joto huku usiku likiendelea kuwa kali kama ilivyo sasa licha ya kuwa kiwango chake ni cha chini.
Aidha, Dk Kijazi alisema kwa kutumia mtambo wa uchambuzi wanaotumia katika utabiri, utawezesha kutoa utabiri wa kimaeneo mara baada ya kuwa na vituo vingi vya hali ya hewa.
Alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam wana vituo viwili tu, lakini inatakiwa kuwa navyo 10 ili kutoa utabiri kwa maeneo na siyo kwa ujumla kwa kuchambua taarifa za kila kituo.
Akizungumzia mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi, alisema wanautumia kwa menejimenti na wafanyakazi kujadili maendeleo ya taaluma na kujadili bajeti yao kwa mwaka ujao ambayo wafanyakazi watashauri na kutoa vipaumbele.
Akizungumza katika mkutano huo, Mjumbe wa Bodi ya Mamlaka hiyo, James Ngeleja alitaka kutumia nafasi hiyo kujadili namna ya kuboresha utabiri wao kutoka usahihi wa zaidi ya asilimia 80 na kufikia asilimia nyingi zaidi.
Pia alitaka wafanyakazi kufanya kazi kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kila mmoja kutenda kazi kwa nafasi yake ili kuongeza ufanisi wa mamlaka.
Chanzo HabariLeo
0 comments:
Post a Comment