Pandu Ameir Kificho.
ALIYEKUWA Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa zaidi ya miaka 20 sasa,
Pandu Ameir Kificho, ameng’olewa katika nafasi hiyo baada ya kushindwa
katika kura za kuwania awamu nyingine ya uongozi wa baraza hilo.
Badala yake wajumbe wateule wa Baraza la Wawakilishi, wamemchagua
Zubeir Ali Maulid, kuwa Spika mteule wa baraza hilo, baada ya kupata
kura 55 na kumuacha kwa mbali Kificho aliyeambulia kura 11 katika
uchaguzi uliofanyika jana katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar.
Aidha katika uchaguzi huo ambao wawakilishi 72 walipiga kura, Janeth
Nora Sekihola ambaye ni hakimu mstaafu akipata kura 4 wakati kura mbili
ziliharibika.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuangushwa
katika uchaguzi huo, Kificho alisema amekubali kushindwa na yupo tayari
kutoa ushirikiano akitakiwa kufanya hivyo.
“Hiyo ndiyo demokrasia, nimekubali kushindwa na nipo tayari kutoa
ushirikiano mkubwa nikitakiwa kufanya hivyo kwa sababu ni ukweli kwamba
ninao uzoefu mkubwa katika nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 20,” alisema.
Naye Spika mteule wa baraza hilo, Maulid alisema anakabiliwa na
changamoto kubwa ya kuleta maendeleo na mabadiliko makubwa katika chombo
hicho ambacho ni moja ya mihimili ya dola katika utekelezaji wa
majukumu yake.
Amesema atatumia uzoefu alioupata kufanya kazi katika taasisi za
kutunga sheria, kwa ajili ya kuleta mabadiliko hayo kwa kuhakikisha
kwamba Baraza la Wawakilishi linafanya kazi inayotakiwa ya kuisimamia
Serikali kwa mujibu wa Katiba.
“Nimekuwa Mwakilishi Shauri Moyo na Waziri mwaka 2000, pia nimekuwa
Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa miaka miwili na nusu kwa
hivyo uwezo wa kufanya kazi katika mabunge ya Jumuiya ya Madola ninao
mkubwa,” alisema.
Aliwaomba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wateule kumpa kila aina ya
ushirikiano utakaomwezesha kutekeleza na kutimiza majukumu yake kwa
mujibu wa Katiba, kwani chombo hicho ni moja ya mihimili ya dola.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliozungumza na gazeti
hili, wamesema kwamba mabadiliko hayo ni ishara na ujumbe tosha kwa Rais
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwamba wawakilishi wanataka
mabadiliko makubwa kwa Serikali kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.
“Mabadiliko makubwa tuliyoyafanya sisi wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kwa kumchagua Zubeir Ali Maulidi kuwa Spika mteule mpya, ni
dalili tosha kwamba sasa tunataka mabadiliko makubwa ndani ya Serikali
kwa kuwa na viongozi watakaowatumikia wananchi moja kwa moja,” alisema
Rashid Ali Juma mwakilishi mteule wa jimbo la Amani.
Kificho ameweka historia kuwa Spika wa Kwanza katika Baraza la
Wawakilishi la mfumo wa vyama vingi kuanzia mwaka 1995, ambapo kabla ya
kuchaguliwa kushika wadhifa huo, alikuwa mwakilishi wa Jimbo la
Makunduchi kuanzia 1988.
Zubeir Ali Maulid mwaka 2000 alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Shauri
Moyo kwa tiketi ya CCM na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na
Uchukuzi, chini ya Serikali ya Rais mstaafu Amani Abeid Karume, ambapo
alidumu katika wadhifa huo kwa miaka mitatu.
Mwaka 2005, Zubeir alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kwamtipura kwa tiketi
ya CCM ambapo akiwa bungeni katika kipindi cha miaka miwili na nusu,
alikuwa Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na kuongoza vikao
mbali mbali kwa kusaidiana na spika na naibu spika.
Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, amemteua Said Hassan Said, kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Uteuzi huo
ndio wa kwanza kufanyika, tangu Rais Shein alipokula kiapo cha kuongoza
Zanzibar kwa miaka mitano ijayo Alhamisi ya wiki hii.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 26 March 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment