Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru uchaguzi wa meya na naibu meya
wa Jiji la Dar es Salaam, kufanyika leo kama ilivyopangwa.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Warialwande Lema alitoa uamuzi huo jana akijibu maombi
yaliyokuwa yamewasilishwa na walalamikaji, Suzan Massawe na Saad
Mohammed Kimji kupitia wakili wao, Elias Nawela dhidi ya Mkurugenzi wa
Jiji la Dar es Salaam.
Wakati Mahakama ikitoa uamuzi huo, Rais
John Magufuli amezitaka pande zinazogombea kiti cha umeya Dar es Salaam,
kukamilisha mchakato huo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika leo,
badala ya kuendeleza malumbano.
Rais alitoa kauli hiyo jana
Ikulu wakati akihakiki silaha zake. Alisema pande zote ziwe tayari
kupokea matokeo ya uchaguzi huo, ili meya apatikane na jiji liweze
kuendelea na mipango yake ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo.
“Mahali
tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali
tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, hiyo ndiyo demokrasia ya kweli,”
alisema Rais Magufuli.
Akitoa uamuzi wa Mahakama uliokuwa
ukisubiriwa kwa hamu na walalamikaji na walalamikiwa, Hakimu Lema
alisema Mahakama haikuona sababu za msingi kati ya zilizowasilishwa na
walalamikaji kuishawishi kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo.
“Siyo
busara kuendelea na sababu ambazo hazijathibitishwa,” alisema Hakimu
Lema alipokuwa akitoa uamuzi huo na kuongeza kwamba kwa kukosekana
orodha inayoonyesha majina ya wapigakura, haijulikani kama waleta maombi
ni miongoni mwa wapigakura au la.
Hakimu Lema alisema
walalamikaji hawakuwa makini tangu awali walipofungua shauri hilo,
Februari 5 kwani hawakutokea mahakamani hadi Februari 14, wakili wao
Nawela alipojitokeza na kuomba nakala ili awapelekee wajibu maombi jambo
linalofanya washindwe kuishawishi Mahakama kuwapa haki yoyote kwa kuwa
hawakufuatilia shauri lao tangu awali.
Mapema jana mchana,
wakili Nawela aliiomba Mahakama itoe zuio la kufanyika uchaguzi huo na
iamuru hali ibaki kama ilivyo hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa
na kutolewa uamuzi kwa madai ya kwamba walalamikaji katika shauri hilo,
hawajapewa haki yao ya kualikwa kushiriki katika uchaguzi huo.
Alidai kuwa iwapo uchaguzi huo utafanyika, basi maombi yao na kesi ya msingi yatakuwa hayana maana.
Akijibu
hoja hizo, wakili Jumanne Mtinange kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la
Dar es Salaam, aliiomba Mahakama kuyaondoa maombi hayo kwa madai kuwa
hayana msingi wowote.
Mtinange alidai hakuna uthibitisho wowote
au orodha ya wapigakura kuonyesha kwamba waleta maombi wamekosekana,
hivyo maombi ya kutaka hali ibaki kama ilivyo hayana uzito wowote.
Alisema
maandalizi ya uchaguzi yana gharama na kwamba ni mara ya tatu
umeahirishwa, hivyo kuomba uchaguzi wa leo uendelee kama kawaida.
Timu
ya mawakili wa Chadema wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, Omary
Msemo na John Mallya walikuwa muda wote wakifuatilia kesi hiyo
mahakamani hapo.
Kwa uamuzi huo, kinyang’anyiro cha kugombea
umeya sasa kimebaki kwa Isaya Mwita wa Chadema na Omary Yenga wa CCM
wanaowania nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika leo katika
Ukumbi wa Karimjee baada ya kuahirishwa mara tatu kwa sababu mbalimbali
ikiwamo zuio batili la Mahakama kabla ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Tamisemi), George Simbachawene kuiagiza uchaguzi huo ufanyike kabla ya
Machi 25.
Baadaye, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Sarah Yohana
alitangaza na kutoa barua kwa wajumbe husika juu ya wito wa kikao cha
Baraza la Madiwani kitakachokuwa na ajenda ya uchaguzi akisema wajumbe
163 watashiriki kupiga kura, kati yao 87 ni kutoka Ukawa na 76 CCM.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment