Saturday, 26 March 2016

Tagged Under:

Tz ‘inavyobeba’ bomba la mafuta la Uganda

By: Unknown On: 22:31
  • Share The Gag
  • Waziri wa nishati na madini wa Tanzania Professa Sospeter Mhongo  na Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni wakibadilishana nyaraka baada ya kutia saini Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda mpaka bandari ya Tanga march 17 nwaka huu.

    WAKATI mjadala kuhusu wapi panastahili kupita bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda, kwa ajili ya kuuzwa kimataifa kuanzia 2018 ukiendelea, gazeti hili limepata taarifa za ndani kuhusu ubora wa Tanzania kupitisha bomba hilo katika ardhi yake, kuliko nchi nyingine yoyote.
    Wiki hii kuliibuka majadala kuhusu wapi bomba hilo litapita, baada ya serikali za Tanzania na Uganda pamoja na kampuni ya Total E&P Uganda na Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC), kutia saini Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji wa mradi huo.
    Utiaji saini huo uliofanyika Alhamisi ya Machi 17, mwaka huu, ulitokana na agizo la kikao cha Rais John Magufuli wa Tanzania na Rais Yoweri Museveni wa Uganda; ambao walikubaliana kuanza haraka ujenzi wa bomba hilo kutoka pembezoni mwa Ziwa Albert, eneo la Hoima Uganda mpaka Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

    Baada ya utekelezaji wa agizo hilo kufikia hatua ya mkataba katika muda mfupi, Jumatatu wiki hii mjadala huo ulipata kasi baada ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kukutana na Rais Museveni, kujaribu kuangalia uwezekano wa bomba hilo kupitia Kenya kwenda Lamu, ambako taarifa zinasema hakuna bandari iliyo tayari.
    Katika kutafuta kiini cha mjadala huo, ndipo gazeti hili likafanikiwa kupata taarifa za ndani zilizonesha namna ardhi ya Tanzania na Bandari ya Tanga, ilivyo na mazingira bora, nafuu na yenye ufanisi kwa utekelezaji wa mradi huo, mbali na kutokuwepo tishio la ulinzi na usalama wa miundombinu kama ilivyo Kenya.

    Uzoefu
    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika mradi huo Tanzania ndiyo yenye uzoefu wa muda mrefu na wa hivi karibuni wa ujenzi, uendeshaji, ulinzi na uelimishaji jamii katika miradi ya bomba la mafuta.
    Uzoefu wa muda mrefu unatajwa kuwa ni wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama) tangu mwaka 1968, likitoka Dar es Salaam mpaka Ndola Zambia.
    Bomba hilo lenye kipenyo cha nchi 8 mpaka 12 na urefu wa kilometa 1,710; kati ya hizo kilometa 860 zipo kwenye ardhi ya Tanzania na limekuwa likipitisha mafuta tani milioni 1.1 kwa mwaka.
    Tanzania pia ina sifa ya uzoefu wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa bomba la gesi kutoka Songo Songo mpaka Dar es Salaam, lenye kipenyo cha nchi 12 na urefu wa kilometa 25 kutoka kisiwa cha Songo Songo mpaka Somangafungu.

    Pia kuna bomba lingine la urefu wa kilometa 207 na kipenyo cha nchi 16, kutoka Somangafungu mpaka Ubungo Dar es Salaam, mbali na bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara mpaka Kinyerezi Dar es Salaam lenye zaidi ya kilometa 490. Lipo pia bomba la gesi linalotoka Mnazi Bay kwenda Mtwara, urefu wa kilometa 27 na kipenyo cha nchi 8, ambalo limeanza kutumika tangu 2006.
    Uzoefu wa kazi
    Katika ujenzi na uendeshaji wa mabomba hayo kwa miaka mingi, Tanzania imejijengea uzoefu wa kazi ya kupata ardhi kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya bomba, tofauti na ugumu uliopo kwa nchi shindani ya Kenya na kusimamia masuala ya kimazingira.
    Tanzania pia imefanikiwa katika kusimamia wakandarasi wa kimataifa na matarajio ya umma wakati wa ujenzi na uendeshaji wa miradi hiyo na hata katika ulinzi wa miundombinu hiyo ambao umeshirikisha jamii.

    *Utayari Bandari ya Tanga
    Sifa nyingine iliyochangia Tanzania kukubalika zaidi katika mradi huo kwa kiwango cha kusaini mkataba wa utekelezaji tofauti na Kenya, ni utayari na mazingira wezeshi ya asili ya Bandari ya Tanga. Wakati Kenya wakijadili namna bomba hilo litakavyotumia bandari ambayo haijajengwa ya Lamu, kwa ajili ya kuuza mafuta, Bandari ya Tanga yenyewe iko tayari kwa kazi.
    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bandari ya Tanga imeshakamilisha Tathimini ya Athari za Kimazingira (EIA) na Upembuzi Yakinifu, wakati njia ya Tanga ya bomba hilo imekwisha ainishwa na haitapitia katika hifadhi za taifa wala mapori ya akiba.
    Bandari ya Tanga inayo fursa ya kutumika zaidi na mradi huo, kwa kuwa haina msongamano wa shughuli za bandari na tayari Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA), kwa mujibu wa taarifa hiyo, imeshatenga fedha za upanuzi utakaohitajika na eneo.

    Bandari hiyo pia imeunganishwa kwa reli na barabara za lami, zinazokwenda nchi za jirani na hivyo iko tayari kuanza kutumika kwa ajili ya kuingizia mizigo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
    Bandari ya Tanga pia ndiyo yenye kingo za asili zinazoruhusu shughuli za upakiaji mafuta kufanyika mwaka mzima bila kusimama,tofauti na bandari zingine ambazo kipindi cha mawimbi makali ya bahari, huwa na wastani wa siku 40 ambazo husababisha shughuli za upakiaji au upakuaji mizigo kusimama.

    Pia bandari hiyo inatumika na hivyo kuwa tayari kwa matumizi ya haraka kama ilivyo dhamira ya Rais Magufuli na Rais Museveni, na hata ujenzi wa boya la kupakia mafuta unatarajiwa kuchukua mwaka mmoja tu hivyo kukamilika Juni 2017, kabla ya muda uliowekwa na mwekezaji wa kuanza kuuza mafuta wa 2018.
    Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi mapipa 200,000 kwa siku kutoka Ziwa Albert nchini Uganda, hadi Bandari ya Tanga na ujenzi wake unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment