Katibu
Mkuu wa chama cha wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema
mikutano yake ya hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania, John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein haikuwa
na agenda yoyote ya kujadili hali ya kisiasa inayoendelea visiwani
Zanzibar.
Maelezo hayo ya Maalim Seif yanamaliza
minong’ono iliyopo nchini baada ya kutembelewa na Rais John Magufuli na
baadaye siku hiyohiyo na Rais Shein na kuzusha hisia kuwa huenda
kulikuwa na jambo zito la kisiasa hasa ikizingatiwa kwamba zilikuwa
zimebaki siku takriban 10 kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani
humo ambao kiongozi huyo wa upinzani ametangaza kwamba hatashiriki.
Maalim
Seif aliwaambia wanahabari jana kuwa Dk Shein alikwenda kumjulia hali
kibinadamu kama ilivyokuwa kwa Rais Magufuli na watu wengine wenye
mapenzi mema, hivyo hakuna haja kwa Wazanzibari kuwa na hofu yoyote.
“Tusingeweza
kuzungumza lolote wakati afya yangu siyo nzuri sana. Unapozungumza
mambo mazito kama hayo ya uchaguzi lazima uwe mzima kimwili na kiakili,”
alisema Maalim Seif baada ya kujuliwa hali na Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa.
Maalim ambaye alikuwa mgombea wa urais kwa
tiketi ya CUF katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka jana alisusia
uchaguzi huo wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20 na Mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha baada ya kuufuta
wa awali kutokana na kuvunjwa kwa taratibu na sheria.
Msimamo
huo ulipigiliwa misumari na Baraza Kuu la Uongozi la CUF lililoeleza
kuwa chama hicho hakitashiriki uchaguzi huo na kuitaka ZEC iondoe majina
ya wagombea wote wa chama hicho katika karatasi za kupigia kura.
Mbali
na CUF, uchaguzi wa marudio umesusiwa na vyama vya upinzani takriban 10
licha ya ZEC kusisitiza kuwa haitaondoa majina kwa kuwa taratibu za
kisheria za kujiondoa hazikufuatwa.
Maalim Seif amepumzika katika hoteli
ya Serena, Dar es Salaam baada ya kutoka katika Hospitali ya Hindu
Mandal ambako alilazwa kwa matibabu mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza
hotelini hapo jana, Lowassa alisema alikwenda kumjulia hali Maalim Seif
na ameridhika kuona afya yake inazidi kuimarika.
Pia,
mazungumzo yao na Lowassa ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita aligombea
urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, hakuyahusisha
masuala ya siasa wala uchaguzi huo wa marudio wa visiwani humo.
Credit;Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment