Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Katoro mkoani Geita jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). |
UTUMBUAJI majipu umehamia katika wilaya anayotoka Rais John Magufuli, ambako Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kutokana na uzembe na ukiukaji wa maadili ya utumishi wa umma.
Maofisa waliokumbwa na rungu la Waziri Mkuu, Majaliwa ni Mhandisi wa Maji wa Wilaya, Peter Ngunula, Ofisa Ushirika Wilaya, Warioba Mwita na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya, Diones Mutayobya. Halmashauri ya Wilaya ya Chato iko mkoani Geita na ndilo Jimbo la Uchaguzi ambalo kwa miaka 20 lilikuwa likiongozwa na Dk Magufuli, kabla ya kujitosa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Aliposhinda uongozi huo wa nchi, aliwaahidi Watanzania kushughulikia matatizo mbalimbali nchini yakiwamo ya ufisadi katika staili aliyoeleza kuwa ni utumbuaji majipu. Tangu Serikali Awamu ya Tano ianze kazi, utumbuaji majipu huo umezikumba taasisi mbalimbali na juzi ilikuwa zamu ya Halmashauri ya Chato.
Waziri Mkuu, Majaliwa alitangaza kuwasimamisha watumishi hao katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Michezo na baadaye alizungumza na watumishi wa umma katika Ukumbi wa Mshikamano Saccos mjini hapa katika ziara yake mkoani Geita. Alitangaza kumsimamisha Mhandisi wa Maji Ngunula baada ya kubainika kung’olewa kwa mashine ya maji huku mhandisi huyo akituhumiwa kutoa maneno ya uongo kwa Waziri Mkuu alipouliza ukweli wa suala hilo.
Alipokuwa anaingia wilayani Chato, Waziri Mkuu alisimamishwa na wananchi wa kijiji cha Nyamirembe katika kata ya Kalebezo na kumlalamikia kuwa mashine yao ya maji imechukuliwa na kupelekwa Morogoro.
Kutokana na hali hiyo, alipofika mjini wakati wa kupokea taarifa ya Mkoa na Wilaya aliulizia suala hilo, na mhandisi huyo alidai ipo, na hata pale Waziri Mkuu alipohoji kama ni kweli ipo, Ngunula alisisitiza uwapo wa mashine hiyo.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu alituma ujumbe wake kwenda kijijini hapo kujiridhisha kama mashine ipo, na alipokuwa katika mkutano wa hadhara alimwita Diwani wa Kata ya Kalebezo kueleza ukweli wa mashine hiyo. “Mheshimiwa Waziri Mkuu pale Nyamirembe kuna pampu mbili, moja ya kutoa maji katika kina kirefu kupeleka katika pampu house na nyingine kutoka katika pampu house kupeleka katika tangi.
Ile ya kina kirefu kwenda katika pampu house haipo,” alieleza Diwani. Hali hiyo ilimfanya Waziri Mkuu kukasirika na kueleza kuwa serikali haiwezi kuvumilia watumishi waongo. “Hatuwezi kuwa na watumishi waongo ambao wanaweza kumdanganya Waziri Mkuu, nimeuliza mashine ipo anasema ipo. Hata kama Mwenyekiti (wa CCM Mkoa) asingesema, ningeondoka naye,” alieleza Waziri.
Kabla ya kupanda jukwaani, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ alisema Waziri Mkuu amedanganywa kwani mashine hiyo haipo na kumtaka kuondoka na mhandisi huyo wa maji. Waziri Mkuu aliamuru, “Kuanzia sasa akae pembeni, Takukuru na Polisi chunguzeni, na asitoke nje ya Chato hadi suala hili limepata uhakika.” Alitaka ichunguzwe ilipo mashine hiyo, mtu aliyeipeleka na sababu za kufanya hivyo.
Aidha, aliagiza kurejeshwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Clement Berege ambaye amehamishiwa wilayani Iramba mkoani Singida, ili kusaidia uchunguzi wa suala hilo. Akizungumza na watumishi, alisema inasikitisha kuona mtumishi huyo wa umma anamdanganya Waziri Mkuu mbele ya vyombo vya habari, jambo ambalo ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma.
Baada ya hapo, aliwageukia watumishi wengine akiwamo Ofisa Ushirika, Mwita na Ofisa Maendeleo ya Jamii, Mutayobya na kuwasomea tuhuma zao kabla ya kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo zikiwamo za rushwa.
Mwita anatuhumiwa kuchota takribani Sh milioni 90 kutoka katika Saccos mbalimbali pamoja na kukopa zaidi ya Sh milioni 70 kutoka vyama vya ushirika na kuahidi kuzirejesha, lakini bila kufanya hivyo hadi sasa.
Alisema alikopeshwa Sh milioni 15 kutoka Mwambao Saccos, Sh milioni 15 nyingine kutoka kwa Teachers Saccos na pia kukopa Sh milioni 20 nyingine. Mbali ya hizo, Waziri Mkuu alisema mkuu huyo wa Idara ana tabia ya ubabe, vitisho huku akimtaja zaidi kuwa ni ‘mzuri sana kwa kuchukua chukua vihela toka pembeni.’
Aidha, anatuhumiwa kumnyanyasa kijinsia mmoja wa watumishi waliokuwa chini yake ambaye baadaye alifanyiwa uhamisho kwa kumtumia rafiki yake aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji. Kwa upande wa Mutayobya, alimtuhumu kuchukua mashine nne za kufyatulia matofali na kuhusika kula Sh 500,000 za vikundi vya ushirika, na anatuhumiwa kuomba fedha kwa vikundi anavyovikopesha.
“Hili hatuwezi kuvumilia…karibuni tutaleta fedha Shilingi milioni hamsini na hapa kuna vikundi 115. Na Ofisa Maendeleo ya Jamii na Ushirika ndio watakaokuwa wanahusika na fedha hizo za ujasiriamali. “Sasa hilo halijaanza tayari hali iko hivi, zikija hali itakuwaje.
Mambo ya ovyo hayawezi kuvumiliwa na serikali hii,” alieleza Waziri Mkuu. Aliongeza, “Takukuru na Polisi nikitoka hapa (juzi usiku) hawa wachukueni, kuanzia sasa wakae pembeni, hawaruhusiwi kutoka Chato. Kama mko safi mtarudi. Mniletee ripoti ofisini kwangu, nami nitaangalia ushauri wenu.”
Waziri Mkuu alikuwa na ziara ya siku mbili mkoani Geita kuanzia juzi akizuru wilaya za Chato na Geita. Kabla ya kuzuru Geita, alikuwa mkoani Kagera ambako pia aliwasimamisha baadhi ya watendaji kwa kushindwa kuwajibika katika maeneo yao na tuhuma za ubadhirifu.
Chanzo Habarileo.
0 comments:
Post a Comment